Wanaoishi mabondeni msisubiri virungu vya polisi

19Mar 2017
Sabato Kasika
Nipashe Jumapili
Muungwana Lazima Nilonge
Wanaoishi mabondeni msisubiri virungu vya polisi

TAARIFA iliyotolewa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa wanahabari inasema kuwa mvua iliyonyesha Jumatatu wiki hii iliua watu wawili waliosombwa na maji kwenye baadhi ya sehemu za jiji hili.

Kwa mujibu wa Kamanda wa kanda hiyo, Kamishna Simon Sirro, miili ya watu hao iliopolewa kutoka katika Mto Msimbazi.

Baada ya tukio hilo, wakazi wa mabondeni wanatahadharishwa kuhama mara moja ili kuepuka kuondolewa kwa nguvu itakayofanywa na jeshi hilo.

Polisi inasema kuwa jukumu lao ni kulinda usalama wa raia na mali zao, hivyo watawachukulia hatua wale wote watakaokaidi kwa kuendelea kuishi katika makazi hayo hatarishi ya mabondeni.

Binafsi ninaunga mkono juhudi hizo kwani zinalenga kuwanusuru na kuwahakikishia usalama wa raia hawa na mali zao na si kuwaacha wakiendelea kuishi katika mazingira hatari kama hayo.

Nakumbuka mafuriko yaliyolikumba Dar es Salaam mwishoni mwa mwaka 2011 yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 10 huku yakiharibu miundombinu mbalimbali ikiwamo ya barabara.

Mafuriko hayo yalipaswa kuwa fundisho kwa wakazi wa mabondeni, lakini ajabu ni kwamba wapo wanaoendelea kuishi huko kana kwamba hakuna tatizo linaloweza kuwapata.

Baada mafuriko makubwa ya mwaka 2011, serikali iliwahamisha baadhi ya wakazi wa mabondeni huko Mabwepande ingawa baadhi yao walikaidi na kubaki kwenye maeneo hayo huku wengine wakirudi kutoka kule walikopelekwa.

Safari hii mafuriko 'yamewabipu', hivyo ni vyema wahusika wakatii maelekezo ya Jeshi la Polisi badala ya kusubiri hadi washurutishwe huku wakijua kwamba kinachofanywa ni kwa ajili ya usalama wao.

Wakati huu ambao mvua za masika zinaendelea kunyesha na jinsi zilivyoleta madhara Jumatatu iliyopita, zingetosha kuwakumbusha kuwa wanatakiwa kuondoka mabondeni haraka iwezekanavyo.

Limekuwa ni kama jambo la kawaida kila unapoanza msimu wa mvua za masika, ambapo viongozi wa serikali huwa wanawahimiza wakazi mabondeni kuhama kutokana na ukweli kwamba wanaishi katika maeneo hatarishi kwa maisha na mali zao.

Pamoja na hilo, bado baadhi ya wameendelea kukaidi huku wengine wakihoji waende wapi kwa vile hawana pa kwenda, lakini ni bora wakajiepusha na hatari hiyo kuliko kuhoji.

Ninajua kwamba inawezekana baadhi yao hawana sehemu ya kwenda na ndio maana swali la tuhamie wapi limekuwa likiulizwa mara kwa mara wahusika wanapotakiwa kuhamishwa, lakini pia wanatakiwa kujiongeza wenyewe ili kuokoa maisha yao.

Serikali iendelee kuwahamisha wakazi wote wa mabondeni huku ikitafuta jibu la swali hilo la tuhamie wapi kwa lengo la kuhakikisha hakuna tena mtu atakayerudi huko.

Umefika wakati sasa wa kuacha kusubiri mvua zinyeshe ndipo watu wahimizwe kuhama mabondeni, badala yake iwe kiangazi ama msimu wa mvua, watu hao wanatakiwa kuhama.

Ninasema hivyo kwa sababu mara nyingi kauli za kuwahimiza watu waishio mabondeni kuhama huwa zinatolewa kwenye msimu wa mvua za masika tu, zikishamalizika maisha yanaendelea kama kawaida!

Serikali ilione tatizo hili na kulifanyia kazi wakati wote kwani binadamu tumeumbiwa kusahau, ndiyo maana inapokaa kimya baadhi ya watu hudhani kwamba mambo yamekwisha.

Ikiwezekana, serikali iweke utaratibu maalumu wa kuhesabu nyumba zote zilizojengwa mabondeni, na kupiga marufuku kujengwa mpya katika maeneo hayo, baada ya hapo ihakikishe inapima viwanja sehemu zinazokubalika.

Baada ya hapo ianze kuwagawia viwanja hivyo kwa bei ya serikali, hatua hii itasaidia kuharakisha juhudi za kuwaondoa wale wote wanaoishi katika mazingira hatarishi na hasa hayo ya mabondeni.

Hatua hiyo, itasaidia hata wale ambao hawana uwezo wa kununua kiwanja kwa bei ya 'kutupwa' kupata eneo na hivyo kuepuka kukimbilia mabondeni ambako inaelezwa kuwa wamekuwa wakinunua viwanja kwa bei nafuu.