Wanasiasa kumbukeni dhana ya asiyekubali kushindwa...

06Nov 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wanasiasa kumbukeni dhana ya asiyekubali kushindwa...

WAKATI nchi ikielekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, Chama cha ACT- Wazalendo, kimetamba kupokea wanachama wapya 98 waliojiunga na chama hicho mwishoni mwa mwezi uliopita.

Kwa mujibu wa kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe, wanachama hao wapya wametokea katika vyama vya CCM na CUF waliojiunga kutoka maeneo mbalimbali ya jijini Dar es Salaam.

Sababu kubwa inayoelezwa na Kabwe ni kwamba wamekimbia kutokana na kutoridhishwa na mchakato wa kura za maoni ndani ya vyama vyao wa kupata wawakilishi katika uchaguzi wa serikali za mitaa.

Zitto anasema, wenyeviti 38 wa zamani wa mitaa na wajumbe wao wametoka chama cha CUF, wakati wenyeviti wa zamani 52 wa mitaa wamejiunga wakitokea CCM.

Kiongozi huyo anasema, sifa ya chama bora ni kile ambacho kina idadi kubwa ya wanachama wakiwamo wageni wengi na kwamba wingi huo wa wanachama unaashiria kukua na kukomaa kwa chama chake.

Pamoja na kwamba Zitto anataja sababu za wageni hao kujiunga na chama chake, lakini kuna haja ya kutafakari hamahama hiyo ambayo imekuja wakati huu wa kuelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.

Kwanza kabisa ieleweke kuwa katiba na sheria za nchi, chini ya mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, uwapo wa vyama vya upinzani ni takwa la kikatiba, na hakuna kosa mtu kuhama chama kimoja kwenda kingine.

Kujiunga na chama chochote kile pia ni hiari, hakuna sheria, ambayo inamlazimisha mtu kuwa mwanachama wa chama chochote isipokuwa kama anataka kuwania nafasi ya uongozi wa kisiasa, sharti awe na chama.

Hivyo suala la kuhama chama ni hiari ya mtu kutokana na atakavyoona na utashi wake mwenyewe, lakini kuna haja ya kuangalia sababu ambazo zimekuwa zinatajwa na wale wanaohama.

Lakini ni vyema kujadili kidogo jambo hili, kwani inaonekana baadhi ya wanasiasa wanadhani kuwa uongozi ni haki yao, vinginevyo wasipochaguliwa wanaona kama wameonewa na kuamua kuhama.

Mfano mmojawapo ni wa hao waliojiunga na ACT- Wazalendo wakidai kutotendewa haki kwenye kura za maoni, katika mchakato wa kupata wawakilishi wa chama kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.

Wanasahau kwamba asiyekubali kushindwa siyo mshindani! Kwanini wasikubali na kuungana na wale waliopendezwa? Kwanini wakimbie chama baada ya kushindwa katika kura za maoni?

Kwanza nieleweke kwamba sipingani na suala la kuhama chama, ila ninapingana na sababu zao, ambazo kimsingi zinaonyesha hawatambui kuwa asiyekubali kushindwa siyo mshindani.

Zipo sababu za msingi, ambazo ninaamini kwamba hasa kwenye imani ya chama kama mtu anaona imani hiyo inakwenda kinyume na kile unachoamini, basi hana budi kuondoka kutafuta imani hiyo kwingine.

Vilevile sera za chama zinaweza kumfanya mtu akaamua kuhama chama kimoja kwenda kingine.

Kama atakuwa ni kiongozi, basi atakuwa alishajaribu kushawishi vinginevyo kupitia vikao husika bila mafanikio, na kulazimika kuachia ngazi na kuhama chama chake cha awali.

Wakati kwa viongozi ikiwa hivyo, kwa wanachama wa kawaida, wao kwa kawaida huwa wanaangalia kama anavutiwa na sera na imani ya chama au la na mwishoni wa siku wanafanya maamuzi.

Iwapo imani ya chama ni tofauti na jinsi mwanachama anavyoamini, basi atakuwa hana uwezo wa kushawishi mabadiliko juu ya imani hiyo, na kitakachofuata ni kuhama chama hicho tu.

Mwanachama anapofanya uamuzi wa kuhama chama kutokana na mazingira ya aina hiyo, haimaanishi kwamba amekisaliti, bali imani yake haiendani na sehemu aliyopo, hivyo hana budi kwenda kwingine.

Lakini mchezo wa kuvizia kwenye kura za maoni na kushindwa, kisha kukimbia chama kwa madai ya kuonewa katika mchakato wa kura za maoni, ni sawa na mtu asiyekubali kushindwa.