Wanasiasa kumbukeni umoja ni nguvu

28Jun 2017
Sabato Kasika
Nipashe
Mjadala
Wanasiasa kumbukeni umoja ni nguvu

NENO upinzani katika siasa za Tanzania lilianza kupata nguvu baada ya nchi kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi vya siasa na kila uchao limeendelea kusikika kutokana na jinsi wanachama wa chama tawala na wale wa upinzani wanavyotofautiana.

Utofauti wa wanasiasa wa makundi hayo mawili unatokana na sera, mitizamo, hoja na mambo mengine yanayohusu siasa, ambayo yamekuwa yakisababisha wakati mwingine kuwapo malumbano makubwa miongoni mwao.

Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu toleo la pili (TUKI), upinzani maana yake ni hali ya kupingana, kubishana au kukinzana.

Ndani ya mfumo huu wa vyama vingi kumekuwa na mtindo wa 'kushambuliana' kwa maneno kati ya wanasiasa wawe wa chama tawala au upinzani, huku kila upande ukijiona kuwa ni bora kuliko mwingine.

Kuanzia kwenye majukwaa, mikutano hata bungeni, Watanzania wamekuwa wakiwashuhudia wanasiasa jinsi wanavyoonyesha umahiri wa kupingana.

Imekuwa kawaida kwa wanasiasa kusikia wakibezana kwamba wenzao hawana sera.
Kwa mfano ni kawaida kwa wanasiasa wa upinzani kupinga kila kitu kinachofanywa na chama tawala.

Nionavyo mimi malumbano ya aina hii hayana tija kwa Watanzania, hivyo wanasiasa wanatakiwa kupingana, kubishana au kukinzana kwa hoja zinazoweza kusaidia taifa kusonga mbele kimaendeleo.

Siamini kwamba upinzani ni kupinga kila kinachofanywa na chama tawala wala siamini kwamba upande wa upinzani unapopinga jambo huwa hauna hoja ya maana.

Kutofautiana katika mtazamo, hoja, sera ni jambo la kawaida ambalo linaweza kuwafanya wanasiasa wakajadili kile wanachotofautiana na mwisho wake wakaibuka na matokeo mazuri.

Lakini wanasiasa wakiendelea kushikilia msimamo wao kwa 'kushambuliana' kwa maneno huku kila upande ukijiona ni bora kuliko mwingine, watakuwa hawawatendei haki Watanzania.

Napenda kutumia nafasi hii kuwaambia wanasiasa kuwa wawe na utamaduni wa kuweka maslahi ya taifa mbele kuliko vyama vyao, kwani inaonekana wazi kuwa malumbano na majina wanayoitana yanatokana na kuegemea kwenye itikadi za vyama zaidi.

Wawe tayari kushauriana, kukosoana na kuzipokea hoja za msingi badala ya kubishana tu huku kila upande ukitaka kuonyesha umahiri wa kutukana au jinsi unavyojua kuliko upande mwingine.

Wanasiasa wa vyama vya upinzani wawe tayari kukosolewa pale wanapokosea na kubadilika, vivyo hivyo wale wa CCM pia wawe tayari kukosolewa pale wanapokosea kwani hakuna binadamu aliyekamilika.

Inawezekana wapo Watanzania wasio na vyama ambao wanaamini kwamba kuwa upinzani ni ukorofi na uhuni.

Vilevile inawezekana wapo wanaoamini mtu kuwa katika vyama vya upinzani ni kuwa adui wa chama tawala, kitu ambacho sicho.

Kimsingi kinachokuwapo ni tofauti ya kiitikadi, kimtazamo na mambo mengine ya kisiasa, lakini inatakiwa kuwa kitu kimoja linapokuja suala linalohusu umoja wa kitaifa au maendeleo ya nchi.

Kuna wanasiasa wanaodhani kwamba ndani ya CCM hakuna jipya na kwamba viongozi na wanachama wake hawapaswi kuaminiwa tena na Watanzania, mawazo ambayo nionavyo ni potofu kabisa.

Hizi ni propaganda, ambazo zipo pande mbili, yaani kwa chama tawala na upinzani, hivyo ni vyema zikaachwa ili wanasiasa washirikiane kuchangia mawazo kwenye mambo ya msingi kwa ajili ya maendeleo ya nchi hii badala ya kubezana tu.

Ninaamini kwamba wanasiasa na hasa wabunge wakizingatia wajibu wao na kuacha malumbano ambayo wamekuwa wakiyafanya bungeni watasaidia nchi hii kusonga mbele.

Ikumbukwe hata Rais John Magufuli amekuwa akisisitiza kila mara kuwa maendeleo hayana vyama, hivyo wabunge wasijiweke pembeni katika suala la maslahi ya umma.

Hawapaswi kugeuka kuwa wawakilishi wa serikali, ambayo wanawajibika kuishauri na kuisimamia.

Kuishauri na kuisimamia serikali siyo usaliti kama ambavyo baadhi ya wabunge wamekuwa wakidhani na kujikuta wakishambuliana kwa maneno, eti kwa sababu ya kushindwa kuwa kitu kimoja kwa maslahi ya umma.