Wanawake bado walia na 50/50 muda ukiyoyoma

15Mar 2017
Salome Kitomari
Nipashe
Uchambuzi
Wanawake bado walia na 50/50 muda ukiyoyoma

KILA Machi 08, ni maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, ikiwa ni hatua mojawapo ya kupaza sauti dhidi ya matatizo mbalimbali yanayowakabili wanawake na namna ya kuyatatua.

Kwa namna tofauti wanawake wamefikisha ujumbe kwa kupaza sauti dhidi ya ukatili dhidi ya wanawake kama vipigo, kudhalilishwa, ndoa za utotoni, ukeketaji, unyanyasaji kiuchumi na kutoshirikishwa katika ngazi za maamuzi kuanzia ngazi ya familia hadi taifa.

Katika uongozi moja ya malengo ya milenia juu ya usawa wa kijinsia ifikapo 2030 ni kufikia 50/50 kwenye uongozi wa ngazi mbalimbali kama wa kuteuliwa, na kuchaguliwa, ili kuwa na ushiriki sawa katika ngazi za maamuzi ambayo yanagusa makundi yote katika jamii.

Moja ya ahadi za wagombea urais wa vyama mbalimbali waliweka nia ya kuhakikisha usawa wa kijinsia katika nafasi watakazopata, na Rais John Magufuli, alitoa ahadi hiyo kuwa suala la 50/50 ataliendeleza kuhakikisha ushiriki wa wanawake unakuwa mkubwa.

Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, alijitahidi kutekeleza usawa wa kijinsia kwa kuwapa nafasi wanawake wengi kwenye nafasi za uongozi na kwa mujibu wa takwimu za mtandao wa TGNP aliondoka madarakani kukiwa na uwakilishi wa asilimia 38 kuiendea 50/50.

Mwenyekiti wa TGNP, Vicensia Shule, anasema uwakilishi wa wanawake katika ngazi ya maamuzi serikalini umeshuka kutoka asilimia 38 awamu ya nne hadi 19 awamu ya tano.

Anasema Desemba ilishuka hadi asilimia 20 na hadi maadhimisho ya siku ya wanawake ilifikia asilimia 19 na itaendelea kushuka siku hadi siku, jambo linalotishia ustawi wa wanawake katika nyanja za maendeleo endelevu.

“Tanzania ni moja ya nchi zilizosaini mikataba ya kimataifa ya kuheshimu haki za wanawake, na uwakilishi katika ngazi ya maamuzi ni mojawapo ya haki za msingi ambazo zipo pia kwenye Katiba. Tunaomba nchi isipoteze sifa yake kwa kupunguza uwakilishi wa wanawake,” anabainisha.

Shule alisema zipo nchi zilizowapa nafasi ya uongozi wa juu wanawake na matokeo ya kimaendeleo yameonekana, na kutolea mfano wa nchi ya Sweeden ambayo mfumo wa utawala ni wa wanawake na imepiga hatua katika elimu na sekta nyingine za maendeleo.

“Hakuna hasara yeyote kwa dola kuhusisha wanawake katika maendeleo yake kwa kufuata matakwa ya Katiba, wanawake wasomi na wenye uwezo mkubwa wapo, lakini hawapewi nafasi kwa sababu ambazo ni za kibaguzi. Hatuwezi kuwa na Dola isiyoheshimu usawa wa kijinsia na kuwa na matarajioya kupiga hatua kimaendeleo,” alifafanua.

Anasema dhana ya 50/50 ni haki ya kila anayestahili na siyo namba na asilimia, kuwa kuwe na wanawake katika nyanja za maamuzi, na kwamba wanawake ni asilimia 51 ya Watanzania hivyo wanastahili kupewa nafasi kutokana na sifa zao.
Hali ikoje?

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma mwaka jana, bado kuna safari ndefu kufikia usawa wa kijinsia, kwa kuwa uwiano wa wanawake kwa wanaume serikalini ni 28:72 ikiwa ni wanawake 2,573 wenye nyadhifa mbalimbali na wanaume 6,674.

Takwimu hizo zinataja uwakilishi wa wanawake kuwa ni majaji asilimia 41, wakurugenzi wasaidizi asilimia 40, Naibu Katibu Mkuu asilimia 31 na wabunge asilimia 37.

Katika Bunge la Jamuhuri ya Muungano uwakilishi wa wanawake ni 141 na wanaume 236, ikiwa ni uhiano wa 37:63, na kati ya wanawake hao wa viti maalum vya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), vya rais ni 113, na waliogombea kwenye majimbo ni 26 ikilinganishwa na 21 miaka iliyopita.

Kati ya wanawake wa viti maalum wanne wameshachaguliwa na rais katika nafasi kumi alizonazo kikatiba.

Katika utawala wa rais Kikwete idadi ya wanawake katika nafasi mbalimbali ilikuwa ya kuridhisha, mfano asilimia 40 ya wakuu wa wilaya walikuwa wanawake ikilinganishwa na asilimia 16 ya walioteuliwa na awamu ya tano.

Pia, mabalozi walioteuliwa na rais walikuwa asilimia 36 ikilinganishwa na 21 kwa awamu ya sasa.

Kwa upande wa Baraza la Mawaziri, wakati wa utawala wa rais Kikwete Baraza lilikuwa na mawaziri 57 kati yake 52 mawaziri kamili na 25 manaibu waziri ikiwa ni wanawake 16 sawa na asilimia 28.

Katika Baraza la serikali ya awamu ya tano lenye jumla ya mawaziri 35 kati yake 19 ni mawaziri na 16 manaibu waziri, kati yao wanawake ni tisa sawa na asilimia 25.

Kwa mujibu wa mkataba wa jinsia na maendeleo mwaka 2008 wa nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), ambao umesainiwa na nchi 14 Tanzania ikiwamo, katika kipengele cha 12 kinazungumzia uwakilishi wa wanawake serikalini.

Mkataba huo unaeleza kuwa nchi hizo zinatakiwa kuhakikisha zinaondoa vikwazo katika kufikia usawa wa kijinsia katika nchi husika, na kuhamasisha kunufaika na haki za msingi kwa kila raia, na kila nchi inatakiwa kuwa na mikakati ya kufikia malengo hayo.

Kipengele cha 12 kinaeleza kuwa ifikapo 2015 uwakilishi wa wanawake kuwa 50/50 katika ngazi za maamuzi serikalini na sekta binafsi.

Lengo la tano la malengo endelevu ya milenia linaeleleza kufikia usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake na wasichana wote, likifafanua zaidi kuwa katika nchi 46 zilizosaini utekelezaji wa malengo hayo 17, Tanzania ikiwa mojawapo, asilimia 30 ya wanawake ni wawakilishi wa wananchi bungeni.

Katika maadhimisho hayo, taasisi ya Tanzania Data Lab iliyo chini ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), iliendesha mafunzo ya siku tatu kwa wanawake kutoka mashirika, taasisi na waandishi wa habari juu ya umuhimu wa kutumia takwimu kuwasilisha changamoto au kilio chao.

Baadhi ya wahamasishaji ni Mkurugenzi wa Shule Direct, Faraja Kota, akiwasilisha mada katika mafunzo hayo anasema matumizi ya takwimu katika kufikisha taarifa katika jamii yanamanufaa kwa kuwa huonyesha uhalisia wa jambo husika.

“Mwanamke anatumia takwimu kila siku kuanzia ngazi ya familia hadi kazini, lakini bado hajaweza kutumia takwimu za kitaifa kueleza matatizo yake katika njia itakayoeleweka kwa jamii inayomzunguka. Wanawake siyo vile watu wanavyotaka awe bali ni vile alivyo,” alisema Kota abbaye amewahi kuwa Mrembo wa Tanzania mwaka 2004.

Mkurugenzi mshauri wa Tanzania Data Lab, Dk. Godfrey Justo, anasema takwimu hazidanganyi hivyo wanawake wanapaswa kupaza sauti kwa kutumia takwimu kwa kuwa maneno yameshatumika kwa miaka mingi.

Anasema mradi huo unalenga kuongeza idadi ya wanawake wenye uwezo wa kueleza masuala mbalimbali kwa kutumia takwimu, na kuonyesha uhalisia kwa michoro mbalimbali na maelezo kidogo na jamii ikaelewa zaidi kuliko maneno matupu.

Naye, Mkurugenzi wa shughuli za kitakwimu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ireniw Ruyobye, anasema matumizi ya takwimu ni muhimu kufikia malengo ya 50 kwa 50 katika ngazi za maamuzi na malengo endelevu ya milenia (SDG’s).

“Matarajio yetu NBS ni mafunzo haya kuongeza matumizi ya takwimu katika kueleza suala la usawa wa jinsia, na kujenga mazingira sawa kwa wanawake kushiriki katika nafasi za maamuzi na kufikia lengo la dunia la uwakilishi wa wanawake 50/50 ifikapo 2030,” anasema.

Mkurugenzi huyo ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk. Albina Chuwa, anasema lengo la tano la SDG’s ni kufanikisha usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake na wasichana na kukiwa na misingi mikuu ya kumaliza namna yoyote ya ukandamizaji katika mnyororo wa maendeleo.

Aidha, anawataka wanawake hao kuwa mabalozi wa kusambaza elimu kwa wananchi hasa wanawake juu ya umuhimu wa kutumia takwimu katika kupaza sauti kupinga ukatili dhidi yao.