Wanawake watumie TEHAMA kupinga ukatili kijinsia

10May 2022
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wanawake watumie TEHAMA kupinga ukatili kijinsia

JUMAPILI Mei 8, ilikuwa siku tulivu kwa wanawake ambayo imepewa jina la Siku ya Mama –Mama’s day. Ulikuwa ni wasaa mwingine wa kuwapa kinamama mahaba, pongezi, kuwazawadia, kuwashika mikono na kufurahi pamoja nao kutokana na kazi kubwa wanazozifanya kwenye jamii kama kuzalisha vyakula ...

mashambani, kujenga uchumi wa taifa na wa familia na kutunza jamaa kuanzia watoto, wazee na wagonjwa.

Wakati kinamama wakifurahia, kujirusha na kufurahi pamoja na jamaa zao, ukweli ni kwamba wanahitaji kuwapo na juhudi zaidi kuwaondoa kwenye madhila mbalimbali yanayowazonga kama kutengwa kiuchumi kutokana na mifumo ya utoaji mikopo kuendeleza ubaguzi.

Siku ya Mama inapoadhimishwa baadhi ya taasisi za fedha zinapenda kuona matajiri wakikopa lakini si kinamama ambao huchukuliwa kuwa hawana cha kuweka reheni. Au ni vigumu kupata fedha na kurejesha mkopo wakiamini kuwa kipato na biashara zao si kubwa. Hata hivyo kinamama wa Tanzania wanaifurahia hatua ya kuwa sehemu ya wanufaika wa mikopo ya serikali wanayoipata kupitia halmashauri zao.

Changamoto nyingine inayowabana ni ushiriki mdogo katika masuala ya kisiasa na ya umma na hili linasababisha juhudi za kufikia uongozi wa usawa wa kijinsia wa 50/50 kwenye ngazi za uwakilishi, ujumbe kwenye mabaraza na kamati mbalimbali kuwa mdogo.

Si hivyo tu hata kwenye masuala ya uteuzi na uongozi wa kisiasa kama mawaziri, majaji, wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi wa taasisi za umma na binafsi, wakuu wa vyuo na wajumbe wa bodi na hata mabalozi kuendelea kuwa na idadi ndogo ya wanawake ikilinganishwa na wanaume.

Kinamama wengi kutokuwa na fursa za elimu kunakochangiwa na wasichana kushindwa kubakia shuleni kuanzia darasa la kwanza hadi vyuo vikuu, kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo mimba za utotoni, mila za kukataa kusomesha wasichana, umaskini kwenye familia na pia changamoto za maumbile kama kukosa jinsi ya kujisitiri wakati wa hedhi.

Masuala ya ukatili wa kijinsia na udhalimu dhidi ya wanawake yanaendelea kuanzia wanawake kutelekezwa na watoto, wanaume kukataa wajibu wa kutunza familia na kupenda kulelewa badala ya kulea, wanawake kuuawa na wenza wao kwa madai ya wivu wa mapenzi, kunyang’anywa mali na kudhulumiwa ndani ya familia zao.

Tatizo jingine ni kuwapo na utamaduni wenye madhara unaokumbatia mila za ukeketaji, kudharau hali ya ujauzito, wengine wakisema mimba si ugonjwa hata ng’ombe anazaa na kuwatumikisha wajawazito hali inayowaumiza kiafya pamoja watoto wao. Kuna unyago unaowafunza mafunzo ya kingono mabinti, vijijini na ngoma zisizo na maadili kama vigodoro.

Changamoto nyingine inayowatesa kinamama ni kutengwa kwa wanawake kwenye meza za mazungumzo iwe ni migogoro ya ardhi, mifugo, matatizo ya kukosekana amani kama ujambazi mitaani yote hayo yanazidi kuwaweka pembeni na kuwa watumwa wa unyanyasaji kijinsia, mathalani mahali pa kazi na mitaani.

Wakati Siku ya Mama ikiadhimishwa, dunia inatawaliwa na teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) hivyo ni wakati wa kupiga simu, kutuma ujumbe wa SMS, kutumia whatsap na twitter kueleza kila kiovu kinachofanywa dhidi yao.

Kutumia TEHAMA kuuhabarisha umma kunaweza kupunguza ukatili, unyanyasaji na dhuluma kwa wanawake na kuongeza ushiriki wao katika uchumi, siasa na masuala ya kijamii kwa kupambana na wale wanaokwamisha.

Wanawake watumie teknolojia kueleza kila uovu wanaofanyiwa kuwa kwamisha kwa sababu woga wao ndiyo ni mauti yao, teknolojia itumike hata kueleza habari za wanaume wanaowakwaruza viganja wakati wa kusalimiana.

Yote hayo yataondoa hisia za unyanyasaji wa kijinsia kuwa ni jambo la kawaida na kuwalazimisha kulikubali na kulitarajia.