Wanayanga sasa wamejua uongo hupanda kwa lifti, ukweli kwa ngazi

19Apr 2021
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wanayanga sasa wamejua uongo hupanda kwa lifti, ukweli kwa ngazi

INAWEZEKANA kuna baadhi ya watu ndani ya Yanga walifanya hivyo kwa makusudi ili kuuchelewesha ukweli. Lakini hii haikuwa kwa manufaa ya klabu, bali yao binafsi.

Mwanamuziki Koffi Olomide kwenye moja kati ya mamia ya nyimbo zake, anasema uongo hupanda lifti, lakini ukweli hupanda ngazi. Hii ina maana uongo utawahi kufika kabla ukweli. Na ndivyo ilivyo kwenye maisha ya walimwengu.

Watu huuamini sana uongo. Na ndiyo unaoaminika zaidi kuwa ukweli. Hata hivyo, siku zote ukweli ambao hupanda ngazi, hata kama ni baada ya miaka 100, utafika tu.

Hapa duniani ukweli utajulikana tu na uongo lazima ujulikane, hata kama vyote vilifichwa kwa miaka gani. Ndiyo maana waswahili wana msemo wao wa 'panapo ukweli, uongo hujutenga.

Kuna watu Yanga walificha ukweli ambao kwa sasa umeanza kudhihirika. Imetumika nguvu nyingi na gharama kuuficha ukweli huo. Wamejitahidi sana. Lakini kama ilivyo kanuni za ukweli na uongo. Ni kwamba ukweli ni lazima utajulikana tu, haijalishi ni miaka mingapi.

Baada ya usajili kuna watu walio ndani ya Yanga waliwaaminisha wanachama na mashabiki kuwa wamesajili wachezaji bora, mahiri na wenye viwango vya juu kuliko timu yoyote ile nchini.

Ligi ilianza kama kawaida. Yanga ilianza kushinda. Lakini si kwa vile ambavyo waliambiwa kutokana na viwango vya wachezaji walioambiwa. Wale watu wanatengeneza propaganda kuwa timu bado haina muunganiko. Timu iliendelea kushinda, lakini bila kiwango kilichotarajiwa, yakatengenezwa mazingira kuwa kocha Zlatco Krmpotic hana uwezo, akatimuliwa.

Kiwango cha uchezaji kikawa ni kile kile. Wakati mwingine timu inashinda, wakati mwingine inasuasua. 'Wachawi' sasa wakawa waamuzi na tamko likatoka kuwashutumu kuwa wanainyonga Yanga. Baadaye tena ikahama kutoka kwa waamuzi, sasa lawama zikapelekwa kwa Shirikisho la Soka nchini (TFF) na Bodi ya Ligi yake.

Lakini wakati lawama zikipelekwa huko, Yanga ikamtimua kocha mwingine Cedric Kaze, hali iliendelea kuwa ile ile. Panapo ukweli uongo hujitenga. Minong'ono sasa ikaanza kutoka kwa Yanga wenyewe kuwa baadhi ya wachezaji waliosajiliwa, hawakupaswa kuichezea timu hiyo.

Huu ndiyo ukweli mchungu ambao Yanga ilipaswa kuuzungumza awali kwa ajili ya kujenga timu, lakini walikuwa wanakwepa. Zile lawama zilipokuwa zinakwenda huku na huko ilikuwa ni kupoteza lengo. Sasa kila mmoja anaongea hilo.

Kiungo wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua, amewataka viongozi wa Yanga kuangalia upya mfumo mzima wa usajili kwenye klabu hiyo ili kuleta wachezaji wenye uwezo mkubwa na tija kwenye timu.

Chambua aliyetamba na Yanga kuanzia katikati ya miaka ya 1980 hadi mwanzoni mwa miaka ya 1990 amesema imefika wakati sasa viongozi kuwatumia watu sahihi ikiwamo wachezaji wa zamani kufanya usajili kuliko ilivyo hivi sasa.

Kiungo huyo amekuwa ni mmoja kati ya wanachama, wachezaji wa zamani na mashabiki wa Yanga kulalamikia uwezo wa wachezaji timu hiyo baadhi yao ni mdogo kwa timu kubwa kama hiyo kiasi cha kuifanya isifanye vizuri.

Aliungana na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro, ambaye anafunguka na kusema Yanga ina baadhi ya wachezaji ambao hawajitumi na wengine hawana uwezo wa kuichezea timu hiyo.

Muro ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga, alishangazwa kuona timu kubwa kama Yanga kuwa na mastraika ambao wana miezi mitano na wengine mwaka bila kufunga bao, na akaongeza kuwa hiyo siyo kama anayoijua yeye ya 'kampa kampa tena.'

Beki wa zamani wa klabu hiyo, Bakari Malima 'Jembe Ulaya' naye pia aliibuka na kudai anachokiona ni kwamba kila siku zinavyozidi kusonga mbele ndiyo viwango vya wachezaji wa Yanga vinaonekana kuzidi kuporomoka.

Huu ni ukweli mchungu ambao Wanayanga walipaswa kuusema mapema, licha ya kwamba kuna baadhi ya wachezaji hao walipokewa kwa mbwembwe kubwa Uwanja wa Ndege.

Kwa sasa wamechelewa, hivyo wasubiri ligi imalizike, wawaondoe baadhi ya wachezaji mizigo kwenye klabu yao hata kama walishangiliwa na kubebwa kuanzia Uwanja wa Ndege hadi klabuni.