Wapenda rushwa CCM wasome ishara za nyakati

23Oct 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wapenda rushwa CCM wasome ishara za nyakati

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeagiza kurudiwa kwa kura za maoni kwa wagombea wa uongozi wa serikali za mitaa ndani ya chama hicho katika maeneo yote yaliyolalamikiwa kwa kukiuka kanuni za uchaguzi

Miongoni mwa maeneo hayo ni mkoa wa Dar es Salaam, ambao unatajwa kuongoza kwa kukiuka kanuni za uchaguzi, na sasa wanachama wapo kwenye mchakato wa kurudia kura hizo.

Hatua iliyochukuliwa na chama hicho ya kuagiza kurudiwa kwa kura za maoni ni wazi kwamba inalenga kukomesha rushwa na kupata viongozi sahihi watakaosaidiana na wananchi kuleta maendeleo kwenye maeneo yao.

Ingawa wapo baadhi ya wanachama wanaoamua kuziba masikio ili wasisikie lolote kuhusu madhara ya rushwa, lakini ukweli rushwa ni adui wa haki na inapingwa katika ahadi za mwanachama.

Imani ya CCM ni kwamba binadamu wote ni sawa, kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake, ujumaa na kujitegemea ndiyo njia pekee ya kujenga jamii ya watu walio sawa na huru.

Ukienda kwenye ahadi za mwanachama, ile ya nne inasema: “Rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala kutoa rushwa.”
Ahadi ya tisa inawataka wanachama wawe waaminifu, lakini hilo nalo bado ni tatizo kwa baadhi yao.

CCM kupitia kwa Katibu wake Mkuu, Dk. Bashiru Ally, kinasema vitendo hivyo na madai ya upendeleo ni dalili za kupanga safu kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao wa Rais, wabunge na madiwani.

Kwamba malalamiko yaliyopokelewa makao makuu yanagusa uvunjifu wa kanuni kwa mtazamo wa rushwa au upendeleo au kupanga safu, lakini tayari mchezo huo umeshazuiwa.

“Napenda kusisitiza haki itendeke, malalamiko tunayoyapokea yanavunja uvunjifu wa kanuni, kwani kanuni za kuchuja wagombea hazikuzingatiwa kwenye baadhi ya maeneo,” anasema Dk. Bashiru.

Kimsingi hatua iliyochukuliwa na chama makao makuu ni dalili tosha kwamba kimedhamiria kupambana na vitendo vya rushwa, ambavyo vimekuwa vikikwamisha baadhi ya wanachama kupata haki.

Kwa mfano baadhi ya wanachama wa CCM wa kijiji cha Suguti, Musoma Vijijini, mkoani Mara, walidai kuuziwa fomu za kuomba uongozi kwa Sh. 20,000 na kusababisha baadhi yao kukwama kuzichukua.

Yanapokuwapo mazingira ya aina hiyo, ni wazi kwamba wasio nacho watashindwe kuwania uongozi ili wenye nia ya kupanga safu ya uongozi wapate upenyo, lakini bahati nzuri hilo limeshtukiwa na kuzimwa.

Hii yote inaonyesha aidha, wanafanya makusudi au hawajui kwamba CCM mpya ilishapiga marufuku michezo yote michafu kwa lengo la kuhakikisha kila mwanachama anashiriki katika uchaguzi iwe kuchagua au kuchaguliwa.

Hivyo ni vyema wapenda rushwa ndani ya CCM wakasoma ishara za nyakati na kutambua kwamba CCM mpya imejishajipambanua kwamba haitaki makandokando yakiwamo hayo ya rushwa.

Katibu Mkuu anasema kulikuwa na rafu za kuchomoa majina kwenye masanduku ya kura na masanduku kubomolewa na wengine wakitumia jina lake kuwa amewapa maelekeo ya kufanya walivyofanya.

Bashiru anasema tatizo lingine ni wasimamizi kuchelewa na kura za maoni kuanza kupigwa baada ya saa tisa alasiri, na sasa wagombea wote walioomba wanatakiwa kurudishwa ili wapigiwe kura.

Kura hizo ilikuwa zimalizike Oktoba 29 na sasa kimeongeza siku mbili hadi Oktoba 31, mwaka huu.

Niwakumbushe wanaCCM kuwa uhalali wa chama kuendelea kuongoza nchi unaweza kupimwa kwenye vipimo mbalimbali kuanzia utekelezaji wa ahadi na pia kumaliza makandokando yakiwamo hayo ya rushwa.

Ikumbukwe kuwa kuwapo kwa rushwa ndani ya chama ni kusababisha migogoro ambayo inaweza kukipasua, lakini nzuri viongozi wa juu wanapopelekewa malalamiko wanayafanyia kazi haraka ili yasilete madhara.

Lakini pamoja na hayo, bado kuna haja wanachama kuzingatia ahadi 10 za mwanachama ambazo ni msingi wa mwanachama kufanya shughuli za chama kwa uaminifu, vinginevyo malalamiko yataendelea kuwapo.