Wapenyeza vilainishi visivyo na ubora wasiachwe watambe

13May 2016
Jackson Kalindimya
Nipashe
Mjadala
Wapenyeza vilainishi visivyo na ubora wasiachwe watambe

TAHADHARI iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Joseph Masikitiko kwamba, kwa sasa hali ni mbaya nchini, kutokana na kukithiri kwa vilainishi visivyo na ubora,...

Vilainishi hivyo ni hatari kwa wamiliki wa magari na mitambo vinahatarisha kushusha uchumi wa mtu mmojammoja na taifa kwa ujumla, linatakiwa kuchukuliwa kwa uzito mkubwa na kila mtu anayelitakia mema taifa hili Miongoni mwa mikoa iliyotajwa kukithiri kwa vilainishi hivyo ni Arusha, Mwanza, Kilimanjaro na Dar es Salaam ambayo ndiyo yenye idadi kubwa ya watu, viwanda, mitambo, magari na shughuli nyingi za uzalishaji mali.Vilainishi hivyo hutumiwa katika mitambo na mashine hizo.

April 5 , mwaka huu, TBS lilitangaza ongezeko kubwa la vilainishi hivyo sokoni, ambavyo hutumika katika magari na mitambo mbalimbali huku wadau tofauti wakiwamo wazalishaji, waagizaji , taasisi na mamlaka za serikali walikutana ili kutoa maamizio ya pamoja kuhusu njia vipi wanadhani zinafaa kuchukuliwa ili kukabiliana na mwenendo huo usiofaa.

Huhitaji kuwa mtaalamu uliyebobea mwenye shahada za juu kabisa kutambua kuwa, matumizi ya vilainishi hivyo bandia katika miktambo na mashine vina uwezekanao mkubwa wa kuharibu mitambo na mashine hizo, hata kusababisha kushuka au kusimamisha uzalishaji, watu kupunguzwa kazi, bidhaa kuadimika sokoni na uchumi kuvurugika kwa kiwango ambacho hakikadiriki.

Hivyo kukithiri kwa vilainishi hivyo katika mikoa hiyo maana yake ni kuathirika kwa uchumi kwa kiasi kikubwa ikiwemo kuathiri maisha yao kwa namna ambayo haiwezi kukadirika kwa vipimo vya kawaida.Kwa nini turuhusu hali iwe hivyo?

Mikoa iliyotajwa kuwa imekithiri kwa vilainishi hivyo yawezekana ikawa sio hiyo tu.Tatizo linaweza kuwa kubwa zaidi kwa kusambaa katika maeneo mengine nchini ambayo hayajafanyiwa uchunguzi wa kina.Inachotakiwa ni kila mtu kuwa macho zaidi.

Haiwezekani watu wachache wenye uroho wa kupata utajiri wa haraka, kwa njia haramu wakaachwa hivihivi tu wafanye watakavyo kama vile nchi hii haina sheria au watu makini wanaoweza kudhibiti mienendo isiyofaa, kwa maslahi ya taifa na watu wake.

Lazima tuchukue hatua za kujenga mazingira ya udadisi na mashaka kwa kila vilainishi vilivyopo mitaani kwamba je vimeingizwa kwa njia halali au vina ubora unaotakiwa?

Ikidhirika kwamba kuna mwanya fulani unaotumiwa na wajanja wachache kinachotakiwa kufanywa haraka ni kukusanya ushahidi wa kutosha na kuchukua hatua za haraka kuwasiliana na mamlaka zinazohusika zitaarifiwe ili zichukue hatua za kufuatilia kwa kina ,kupima na kujiridhisha kuwa ukweli uko wapi.Kutoa taarifa sahihi ni hatua muhimu ya kuunga mkono utokomezwaji wa bidhaa hizi haramu.

Hebu fikiria, kama kila mtu atachukua hatua za kuwa mlinzi wa kufuatilia na kuchunguza kwa kila vilainishi vilivyopo tutakuwa na ulinzi kiasi gani hapa nchini hata kutufanya tuchezewe na wahalifu hao wachache?

Katika kuhakikisha kuwa, mwenendo huo usioridhisha unachukuliwa hatua stahiki za kudhibitiwa kikamilifu, Wizara ya Viwanda na Biashara, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati, Maji na Mafuta (EWURA),Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) walikutana na kuweka maazimio ya pamoja ya kuwataka wazalishaji nchini na waagizaji wa bidhaa hiyo nje ya nchi, kusajiriwa kabla ya bidhaa hizo kuingizwa sokoni kisha kuchukuliwa hatua za kisheria.

Kama maazimio hayo yatafanyiwa kazi na kusimamiwa kikamilifu ni kwamba, yatasaidia sana kutoa welekeo mzuri wa kuhakikisha kunakuwa na udhibiti wa bidhaa hiyo tofauti na hali ilivyo sasa.

Siamini kabisa kuwa wahalifu hao wachache wataachwa watambe kwa kuushinda umma unaoamua kujilinda kwa kutumia nguvu za umoja na ushirikiano hadi kumuangamiza adui wa mwisho kabisa.

Kila mtu achukue hatua katika kuhakikisha kuwa changamoto hii ya kiuchumi inapatiwa kinga madhubuti.Wafanyabiashara wafanye biashara halali watapata faida na sio kuachwa watumie njia za mkato na kusababisha madhara makubwa kwa watu wengine ambao hawana hatia.

Kinachotakiwa ni kwa kila mtu kutambua kuwa wahalifu hao wakiachwa wauvuruge uchumi wa nchi hii kupitia mitambo na mashine ni kwamba, waathirika wakubwa ni watu wote wakiwemo maskini, ambao uchumi wao ni wa kuunga unga na hivyo unapoongezwa mzigo mwingine wa kero ambazo zinaweza kuepukika, maisha huwa magumu zaidi hata kuwafanya washindwe kufurahia maisha inavyotakiwa. Kila mtu achukue hatua sasa.