Wapinzani ‘wasilewe’ kwa kasi ya Magufuli

11May 2016
Mashaka Mgeta
Nipashe
Mtazamo Yakinifu
Wapinzani ‘wasilewe’ kwa kasi ya Magufuli

NI wazi kwamba kazi zinazofanywa na serikali ya Rais John Magufuli, zinakubalika miongoni mwa watu wa kada ya chini.

Inawezekana hali ikawa hivyo kwa wale wa daraja la kwanza, yaani wenye utajiri wa kutupwa, mali na mfumo wa maisha yanayowafanya waishi kama wapo peponi.

Katikati ya watu wa kada hiyo, wapo walioifikia hali hiyo kutokana na njama, hujuma, hila na janja dhidi ya mali za umma, wakafikia kuwa matajiri wanaoheshimiwa kwa namna iliyo haramu.

Lakini wapo matajiri wenye mali na wanaoishi maisha bora, ikiwa ni matunda ya kazi halali wanazozifanya.

Hivyo utendaji kazi wa serikali ya Rais Magufuli unapodhihirika katikati ya kada hizo, walio masikini katika mioyo na mali za duniani, wanapata furaha kuu.

Kwa maana utendaji kazi huo umefikia hatua ya kuwaadhibu ‘vigogo’ na ‘magwiji’ wa uporaji mali za umma, waliouhalalisha uovu huo na kuifanya kuwa sehemu ya fursa za kujitwalia kila walichokitaka, hata kama kiliulenga umma.

Rais Magufuli yupo katika hatua nzuri ya kurejesha nidhamu mahali pa kazi hasa kwenye ofisi za umma, ingawa hatua nyingine anazozichukua zinakosolewa, nitajadili baadaye.

Wanaoishi maisha duni yanayochagizwa na umasikini unaochangiwa na kutonufaika na rasilimali za nchi wanaifurahia hali hiyo, kwamba Rais anathubutu, anaweza, anatimiza.

Kwa mtazamo wa haraka, mioyo ya Watanzania kwa mamilioni, iliyonyong’onyea na kukata tamaa, inaunganishwa na moyo wa Rais Magufuli wenye utashi usiowaonea haya ‘wanyang’anyi’ na wahujumu uchumi. Kwa sehemu kubwa wanakuwa wamoja katika mwendo wa vita vya kutumbua majipu.

Kilio cha wapenda amani ya kweli, ile inayohanikizwa na hitaji ya uhakika wa maisha bora, haki na usawa, kinaelekea kwenye mwelekeo wa kupata jawabu linalotokana na utendaji kazi wa serikali ya Rais Magufuli.

Hali hiyo haina maana kwamba serikali za marais zilizopita hazikufanya mambo mema, la hasha. Zilifanya. Na pia zilihusika katika yaliyo maovu, kwa maana ni serikali zilizotokana na watu.

Ndivyo itakavyokuwa kwa serikali ya Rais Magufuli, kwamba pamoja na mwelekeo mzuri wa kushughulikia kero na kadhia tofauti za kijamii, bado itateleza mahali kutokana na sababu za kibinadamu za watendaji wake.

Si rahisi akasafiri na watendaji wote kwa dhamira, utashi na kusudio linalofanana.

Mabadiliko ya utendaji kazi yanayofanywa na serikali ya Rais Magufuli, `akiyatumbua majipu’ yaliyo kwenye mifumo ya watawala, yanatafsiriwa kwa namna tofauti.

Wapo wanaoamini kwamba utawala wa Rais Magufuli ni mfano wa ‘mwarobaini’ wa matatizo yanayoikabili Tanzania na Watanzania.

Wapo wanaoamini kwamba utawala wa Rais Magufuli utarejesha hadhi na nidhamu ya utendaji kazi serikalini.

Miongoni mwa wanaoamini hivyo wamo kwenye vyama vya siasa vya upinzani, wengine wakifikia hatua ya kubashiri kwamba Rais Magufuli anauua upinzani.

Hata ndani ya wapinzani wenyewe, wapo wanaoamini hivyo. Haipaswi kuiishi imani hiyo na ile inayotokana na matukio niliyoyaainisha hapo juu.

Kwa leo nitajadili nafasi ya upinzani katika safari ya utawala unaojinasibu kwa ‘utumbuaji majipu’.

Pamoja na dhamira na utashi usiotiliwa shaka wa Rais Magufuli kuzishughulikia kero za jamii, si rahisi kuaminisha kwamba upepo unaotokana na nguvu za upinzani nchini, umechagia taifa kuwa hapa lilipo na bila shaka bado unahitajika ili kuifikia Tanzania halisi yenye neema ya kweli.

Upinzani una nafasi kubwa kutokana na ukweli kwamba kwa kadri unavyozidi kuungwa mkono hata kufikia hatua ya kuunda uongozi wa halmashauri muhimu kama ya jiji la Dar es Salaam, haupaswi `kulewa’ ama ‘kuleweshwa’ na kasi ya Rais Magufuli.

Kwa maana Rais Magufuli anapoyatekeleza hayo, wapo wasioridhishwa, wasiokubali na wanaomkosoa, wakiwamo walio ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Walio ndani ya CCM, serikali na taasisi nyingine walizoea kauli mbiu ya kuwa ‘CCM itadumu madarakani kwa zaidi ya miaka 100’.

Walipotamka hivyo, walio wengi hawakukusudia kuitumikia jamii, isipokuwa kuimarisha mifumo na mbinu za kupora rasilimali za umma na kuuhujumu uchumi wa nchi, ili waendelee kuishi kwa ‘miaka 100’ wakiwa kwenye neema tele!

Ndio maana hata walipozisikia taarifa za jina la Magufuli kuteuliwa kuwa mgombea urais na baadaye kushinda, iliaminika kwamba wakati wa kuendelea ‘kutawala kwa miaka 100’ umefika, kwa vile mtawala ametoka ndani ya ‘watawala wa mpaka miaka 100’.

Wakati ikiaminika hivyo, wana-CCM wenye nia ya kuiondoa Tanzania na Watanzania kutoka mikononi mwa wanyonyaji, wakajiondoa na kujiunga upinzani, hivyo kuibua ushindani unaoripotiwa kutokuwapo tangu Uhuru wa Tanganyika (baadaye Tanzania) wa Desemba 9, 1961.

Ndio maana, hata utendaji kazi wa serikali ya Rais Magufuli unaotafsiriwa pia kama unajibu hoja za wapinzani, ni kielelezo muhimu cha Tanzania kuendelea kuuhitaji upinzani wenye nguvu na mwelekeo wa kuleta ushidani wa kweli katika siasa za ndani.

Ndio maana ninaiona haja thabiti kwa upinzani kujiimarisha, kubuni mbinu na mikakati itakayowaweka hai katika ushindani dhidi ya mtawala anayeonekana ‘kutembea juu ya maneno yao.’

Itafaa sana kwa maslahi, ustawi na maendeleo ya nchi na watu wake.

Mashaka Mgeta ni mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii. Anapatikana simu namba +255754691540, 0716635612 ama barua pepe:mgeta[email protected] ama [email protected].