Wapinzani jitafakarini, migogoro hadi lini?

20Mar 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wapinzani jitafakarini, migogoro hadi lini?

HISTORIA inaonyesha kuwa Chama cha Wananchi CUF kilianzishwa mwaka 1993 kutokana na muungano wa vyama vya Zanzibar United Front (ZUF) na Chama cha Wananchi Tanzania (CCWT) cha Tanzania Bara.

James Mapalala, alikuwa ni mwenyekiti wake wa kwanza na makamu mwenyekiti alikuwa ni Maalim Seif Sharif Hamad, huku Katibu Mkuu akiwa Shaaban Mloo ambaye sasa ni marehemu.

Miaka michache baadaye tangu kuanzishwa kwa chama hicho, Mapalala alifukuzwa ndani ya CUF baada ya kutofautiana na wenzake na kwenda kuanzisha Chama cha Haki na Ustawi (Chausta).

Wakati mwanasiasa huyo mkongwe anatimuliwa ilikuwa pia ni miaka michache tangu serikali kuruhusu Tanzania kuingia kwenye mfumo wa siasa za vyama vingi, ulioanza mwaka 1992.

Baada ya Mapalala kuondolewa, baadaye Profesa Ibrahim Lipumba, alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho, CUF ikaendelea na shughuli za siasa na kuonyesha upinzani kwa vyama vingine.

Lakini miaka 22 baadaye CUF ikaingia tena kwenye mgogoro ulioanza mwaka 2016 baada ya Prof. Lipumba kutangaza kurudi katika nafasi hiyo alioiacha miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Ilikuwa ni takriban mwaka mmoja tangu alipojiuzulu nafasi ya uenyekiti na kuwa mwanachama wa kawaida, lakini aliporejea kukalia kiti hicho, alikutana na upinzani mkali, lakini Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ikatangaza kumtambua kama mwenyekiti halali wa chama ndipo mgogoro ukazuka.

Aliibua mgogoro kwa sababu aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Self Sharif Hamad, hakukubaliana na uamuzi huo, hali ambayo ilisababisha uhasama hadi kuwapo kwa CUF mbili ya Maalim na Prof. Lipumba.

Wafuasi wa CUF hizo mbili walikuwa na uhasama miongoni mwao, kila upande ukiona mwingine kama adui na walifikia kutishiana na hata kuumizana

Mgogoro huo uliodumu kwa zaidi ya miaka miwili, ulifikishwa mahakamani, ambapo Jumatatu juzi,ulihitimishwa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kubariki uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa wa kumtambua Profesa Ibrahim Lipumba kuwa mwenyekiti wa chama hicho taifa.

Baada ya uamuzi huo wa Mahakama, Maalim aliamua kujitoa CUF kujiunga na chama cha ACT- Wazalendo ili kuendelea na harakati za kisiasa.

Amekaririwa na vyombo vya habari wakati akitangaza kuhama na kusema: "Shusha tanga pandisha tanga, safari inaendelea,” huku akiwataka mashabiki wake wote kuungana naye katika chama cha ACT-Wazalendo.

Wakati Maalim akisema hayo, mashabiki wake kwa upande wa visiwa vya Zanzibar, nao walikaririwa na vyombo vya habari wakisema Prof. Lipumba amechukua chama siyo wanachama.

Kauli hiyo inaonyesha kwamba huenda kukawa na mpambano mkali wa kunyang'anyana wanachama kati ya vyama hivyo viwili na hatimaye kusababisha kimojawapo kuyumba.

Hii ni kwa sababu baada ya Maalim kutangaza uamuzi wa kuhamia chama cha ACT-Wazalendo, baadhi ya bendera za CUF zilishushwa katika ofisi mbalimbali za CUF nchini.

Miongoni mwa ofisi hizo ni za visiwani Zanzibar, ambako inaaminika kwamba ilikuwa ni ngome kuu ya CUF wakati huo chama kikiwa hakina mgogoro wa kiuongozi uliosababisha Maalim na Prof. Lipumba kutengana.

Prof. Lipumba amemudu kumuondoa Maalim Seif, je, ataweza mikikimikiki ya kisiasa akiwa na chama kilichogawanyika vipande viwili?
Ikumbukwe kuwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, kwa mara ya kwanza CUF ilipata wabunge wengi bara, huku mkoa wa Lindi ukiongoza na wabunge wanne ikiwa imegawana idadi sawa na CCM.

Wakati akiwa mwenyekiti wa kamati ya muda ya uongozi CUF, Julius Mtatiro, aliwahi kukiri kuwa chama hicho kilipata wabunge wengi kwa sababu ya kuwa ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Bila ushirikiano wa vyama vingine ataweza kuivusha CUF ikapata mafanikio kama ya mwaka 2015? Moja ya mambo muhimu ambayo wanasiasa wanapaswa kukumbuka ni kwamba umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu.

Maalim ni 'muumini' wa Ukawa na ametangaza kushirikiana na umoja huo ili kuendeleza harakati za kisiasa, lakini hasimu wake, Prof. Lipumba tangu mwanzo hakuonekana kuukubali umoja huo.

Lengo la chama cha siasa ni kushika dola, lakini pia ni muhimu kwanza kishike mioyo ya wananchi wengi ambao ndio watakipigia kura na kukipa ushindi na kukiingiza madarakani kupitia sanduku la kura.

Pengine ni vyema vyama vya siasa hasa vya upinzani kujitathmini iwapo migogoro inaweza kuvifikisha kwenye hatua ya kushika dola kama si kuvisambaratisha.