Wasiojua ndio wanaomshangaa Salamba

27May 2019
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wasiojua ndio wanaomshangaa Salamba

AMA kweli ukishangaa ya Mussa utayaona ya Firauni. Kwenye dunia hii tunayoishi kuna kizazi kiliwahi kuishi bila kuona teknolojia ya televisheni wala simu za mkononi.

Hapa Tanzania Bara tu, kwenye miaka ya 80' hakukuwapo na televisheni wala simu za mkononi, hivyo walioishi miaka hiyo kwenda nyuma walikufa bila kukutana na teknolojia hiyo.

Kuna kizazi kingine, ambacho ndicho hiki chetu. Hiki kimewahi kuishi wakati hakukuwa na televisheni wala simu, lakini teknolojia hii imewakuta.

Kizazi hiki ndicho kilichopata bahati ya kuishi kwenye mazingira yote mawili, kipindi hicho ambacho hakukuwa na mambo hayo, lakini kipindi hiki ambacho kuna utandawazi na kuangalia TV, pia kumiliki au kuwa kwenye dunia ya watu wanaomiliki simu za mkononi.

Pia kipo kizazi cha sasa ambacho chenyewe kimezaliwa moja kwa moja na kukuta teknolojia hii.

Na hawa ukiwaambia jinsi watu walivyokuwa wakiishi zamani bila kuangalia TV wala kuwa na simu wa mkononi wanashangaa na kuona hawa watu walikuwa wanaishije? Pia wanaona kama maisha ya watu hao yalikuwa magumu bila vitu hivyo.

Cha ajabu ni kwamba kuna baadhi wa kizazi hiki hiki cha teknolojia wana mawazo kama ya wale ambao waliishi enzi ambazo hakuna TV wala simu.

Baada ya mechi ya kirafiki kati ya Simba na Sevilla ya Hispania, kuna kitendo kilifanywa na mchezaji wa Simba, Adam Salamba kumuomba mchezaji nyota kabisa nchini Argentina anayeichezea klabu hiyo, Ever Banega kiatu alichochezea mechi hiyo, kimefanywa kama ndiyo tukio kubwa kuliko mechi yenyewe.

Hapa sina hata haja ya kufafanua ni kwa nini Salamba aliomba kiatu kwa sababu inaeleweka kabisa kuwa alicheza na mchezaji mkubwa kabisa duniani na kwake ni ndoto kucheza na mtu kama huyo, hivyo alihitaji kumbukumbu yake na hata kuwawekea wajukuu zake wapate tambua kuwa babu yao alikuwa mchezaji wa kiwango kikubwa kiasi cha kucheza na mchezaji huyo.

Ninachoshangaa mimi ni kwa nini baadhi ya mashabiki wa kizazi hiki wameifanya inshu hiyo imekuwa kubwa wakati wao kila wiki wanaangalia mechi za Ligi Kuu mbalimbali nchini Ulaya na Dunia kwa ujumla wakati vitu hivi ni vya kawaida sana na vinaonekana huko kwa wenzetu?

Nisingepata shida kama wangekuwa wanajadili hili ni wale ambao waliishi enzi ambazo hakuna TV wala simu za mkononi, lakini kwa kizazi cha sasa ni aibu kubwa kujadili kitu au kumsema vibaya Salamba kwa kufanya alivyofanya kwa sababu ni jambo ambalo tunaliona hata huko kwenye nchi zilizoendelea.

Nilitegemea baada ya mechi hiyo kitakachojadiliwa, achilia mbali matokeo ya mechi ni kuwauliza wachezaji wa Simba kama wameshafanya mazungumzo na wachezaji wa Sevilla kuwauliza kama wao wanafanyaje ili kuwa kwenye ubora walionao, kuanzia mazoezi yao, chakula na vitu vingine vinavyowafanya wenzetu wacheze soka kwa muda mrefu, huku viwango vyao vikiwa pale pale.

Badala yake watu wanakwenda kujadiliana au kuzungumzia suala ambalo hata wale wa kizazi cha miaka ya 60', 70' hadi 80' ambako nchini kulikuwa hakuna TV wala simu za mkononi wasingeweza kukaa na kulifuatilia kama ni jambo la ajabu sana.

Nina uhakika kama kuna Mhispania mmoja akafuatilia mijadala hii na kutafsiriwa kwa Kiswahili angeshangaa sana na kutuona kuwa ama baadhi ya mashabiki wa soka nchini wamechelewa sana, au ni washamba wa masuala ya soka.

Suala hili la kubadilishana jezi, viatu na vitu vingine vya kimichezo ni utamaduni wa wanamichezo, hasa wachezaji na mashabiki ambao wao wanachofanya ni kwenda kuweka kumbukumbu kwenye maisha yao ya soka.

Sijajua tatizo hasa ni nini? Utani, ushabiki, wivu, au kufuata mkumbo, kwa sababu hakuna cha ajabu ama kigeni chochote ambacho Salamba amekifanya.

Wamemuandama kijana wa watu mpaka ameomba radhi kwa kitu ambacho kilifaa apongezwe kwa kuwa muungwana yaani 'fair play'. Ningeungana nao kama Salamba angemchezea rafu mbaya isiyokuwa na sababu yoyote mchezaji huyo kwa sababu angekuwa si muungwana, lakini kwa hili hapana.

Kizazi cha teknolojia, kinachoona mambo yote laivu yanayofanyika Ulaya hadi huku Bongo, leo kushangaa jambo hilo ni ajabu na kweli ni aibu pia.

Je, hilo lingetokea kwa wachezaji wa wa Simba kugombea viatu hivyo kama ambavyo wachezaji wa Raja Casabalanca ya Morocco walivyogombea na kugawana kiatu kimoja kimoja cha Ronaldinho, pindi walipocheza na Barcelona mechi ya kirafiki miaka iliyopita, sijui ingekuwaje? Mashabiki tubadilike.