Watakaofeli kidato cha sita watazamwe

21Jul 2020
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Watakaofeli kidato cha sita watazamwe

MITIHANI ya kidato cha sita imekamilika wiki iliyopita baada ya serikali kuwaruhusu wanafunzi kurejea tena darasani miezi mitatu baada ya likizo ya corona iliyoanza Machi 17, 2020.

Miezi mitatu kukaa nje ya darasa si kazi ndogo na kuna uwezekano wa wanafunzi wengi kushindwa kufanya vizuri kwenye mitihani hiyo. Hatuliombei hilo lakini, ni jambo la kutazamwa kwa jicho la pili.

Mitihani iliyomalizika inayoandaliwa na Baraza la Taifa la Mtihani (NECTA), licha ya kulenga kupima uelewa, ujuzi na stadi mwanafunzi alizopata baada ya kukaa darasani kwa kipindi cha miaka miwili, imefanyika wakati ambao wanafunzi ‘walivurugwa’.
Walitatizwa na corona kutoka na ukweli kuwa hata kusoma wakiwa nyumbani ilikuwa ni jambo gumu.

Haikuwa rahisi kwa wengi kutulia nyumbani na kusoma, lakini serikali ilipiga marufuku masomo ya ziada na mikusanyiko ambayo ingetishia maisha ya wanafunzi hao.

Watoto hao walishindwa kujifunza kwa dhati na huenda walikwamishwa na kutokujua hatima ya masomo kwa vile hawakufahamu ni lini wangerejea tena shuleni.

Kwa kawaida kiwango cha uelewa na hata ufaulu hutofautiana kutoka mwanafunzi mmoja na mwingine, jambo linalochangiwa na mambo mengi yakiwamo ya kimaumbile, mazingira ya shuleni na ya nyumbani pamoja na fursa zilizopo.

Wengi wanaamini kuwa uwezo wa akili unaweza kuwa ni urithi mtu anaopata kutoka kwa wazazi wake, mazingira anayosoma kama uwepo wa walimu, upatikanaji wa vifaa vya kufundishia, ikiwamo vitabu, maabara na utaalamu.

Walimu wa kutosha waliona ujuzi na morali wa kufundisha inaweza kuwa kati ya sababu ya mwanafunzi kufanya vizuri.

Nafasi mfano, muda wa kutosha wa kujisomea, kujumuika na wenzake kufanya mijadala ili kuongeza uelewa baada ya muda wa masomo wa darasani yote hayo husaidia kufaulu. Kupewa kazi nyingi hasa mabinti badala ya kusoma kunaweza kuchangia kuwakwamisha kufaulu.

Inawezekana wakati wa corona wengi hawakupata nafasi ya kutosha ya kujisomea na pia walichanganyikiwa kutokana na mambo yalivyokuwa hasa hofu, hivyo huenda wakapata alama za chini.

Kutokufaulu kunamaanisha kuwa inawezekana wakaachwa kwenye nafasi za vyuo vikuu hasa kupata mikopo ya elimu ya juu.

Changamoto hii haiwahusu wanafunzi ambao wazazi na walezi wao wanao uwezo wa kuwalipia na kuwapeleka popote kwa ajili ya masomo ya vyuo vya elimu ya juu.

Kuna wasiwasi kuwa huenda mabinti wakafeli kutokana na ugumu wa maisha ya mazingira yanayowazunguka. Kwa hiyo ingekuwa vyema kama watakaokosa fursa wakasaidiwa wasiachwe kupoteza kila kitu kutokana na changamoto za maisha waliyokutana nayo wakati wa corona.

Ni vyema mabinti ambao mara nyingi huwa waathirika wakapata mbadala wa kuwasaidia hata kama watakuwa wamefeli kwenye masomo ili kujiendeleza kwa kuwa corona imekuwa na athari nyingi kielimu.

Kufikiria suala mbadala kwa wasichana ni jambo jema kwa kuwa corona ilisababisha wanafunzi kukaa nyumbani miezi mitatu ambao ni muda mrefu.

Ikumbukwe kuwa kufeli mtihani kunaweza kuwa na sababu nyingi, pengine wakati huo, mwanafunzi hakuwa sawa kisaikolojia kutokana na yaliyomfika wakati wa likizo ya corona. Wapo walionyanyaswa kijinsia, kuna waliopewa mimba na wakati mwingine kutumikishwa kazi kupindukia hasa vijijini na watoto wanaotoka katika familia maskini.

Kwa hiyo, serikali, wadau na watetezi wa haki ya mtoto kuna haja ya kuanza kutafakari jinsi ya kuwasaidia wanafunzi watakaofeli kwenye matokeo ya mtihani wa kidato cha sita kwa kuwa ulifanyika katika mazingira ya changamoto.

Kuwa na namna ya kuwasaidia wanafunzi hakumaanishi kuwa kila atayeanguka, anahusika sivyo. Msaada uwahusu wale waliokuwa na maendeleo ya juu na jitihada kubwa lakini ‘wakavurunda’ kutokana na baadhi ya changamoto ambazo hazikukwepeka.
Msaada huo unaweza kuwa fursa ya kuwawezesha kujipanga tena na kufanya vizuri katika masomo yao na wanafunzi.