Watakaorasimishwa walinde wanyama ili wawe endelevu

20Jan 2019
Beatrice Shayo
Nipashe Jumapili
Muungwana Lazima Nilonge
Watakaorasimishwa walinde wanyama ili wawe endelevu

SERIKALI imefanya jitihada mbalimbali katika uhifadhi wa wanyamapori kwa lengo la kuendeleza na kulinda  rasilimali hiyo inayoongoza kuvuta watalii kuja nchini.

Wanyama hao wanaishi kwenye hifadhi za taifa ambazo ni maeneo  muhimu yanayotegemewa kwenye  kulinda wanyama hao, wanahitaji  ulinzi ambao ni jukumu la kila mmoja  badala ya kuiachia serikali pekee.

Moja ya jitihada za serikali kulinda maliasili za porini kwa miaka ya hivi karibuni ni pamoja na   kupamabana na ujangili na  kuutokomeza. Changamoto hiyo kwa asilimia kubwa imedhibitiwa kwani wanyama kama tembo, faru na siimba walikuwa mbioni kutoweka.

Itakumbukwa kuwa  ujangili katika kipindi cha miaka michache iliyopita  kabla ya kudhibitiwa  uliiletea sifa mbaya Tanzania na kilio cha kukatiza uhai  wa wanyama kilitikisa watu na taasisi mashuhuri duniani, ikiwamo familia ya kifalme ya Uingereza.

Moja ya  mikakati ya kutokomeza tatizo hilo na kuhakisha wanyamapori wanakuwa salama ni pamoja na ulinzi madhubuti na ushirikishwaji jamii na wadau mbalimbali kuwazuia na kuwadhibiti majangili.

Kukamatwa kwa majangili pamoja na kuimarishwa kwa ulinzi katika hifadhi  nchini ni moja ya vitu ambavyo vimechangia kutokomeza changamoto hiyo na kuiletea Tanzania sifa mbaya.

Japo licha ya kuwapo jitihada hizo, lakini  jambo ambalo serikali inatakiwa kuliangalia kwa jicho la pekee ili lisihatarishe maisha ya wanyama .

Wananchi wadhibitiwe kufanya ujenzi au uwekezaji wa aina yoyote  katika hifadhi. Hili ni  jambo ambalo serikali inatakiwa kuliangalia kwa upana kama ilivyotumia nguvu kubwa katika kupambana na ujangili.

Mbali na kuwepo kwa ongezeko la ujenzi wamekuwa wakilima ama kufuga mifugo ndani ya hifadhi jambo ambalo aidha,  linahatarisha usalama wa wanyamapori.

Mwingiliano huo wa wananyama na binadamu katika hifadhi  unahatarisha usalama wa rasilimali hiyo ikiwa ni  pamoja na uwezekano wa kusambaa  magonjwa na kuathiri wanyama pori na mifugo..

Ni vizuri wizara zinazoshughulikia vijiji 366 vilivyokuwa na mgogoro na hifadhi zikaliangalia jambo hili kikamilifu na kwa umakini ili kuzuia ujenzi wa nyumba au uwekezaji  katika hifadhi.

Wananchi licha ya kwamba wana haki yao   wanapoachwa na kuendelea na ujenzi bila kuwadhibiti huchangia kuwepo kwa ongezeko kubwa la watu katika maeneo ya hifadhi.

Kuwepo kwa mwingiliano huo kunachangia wanyama kushindwa kuhama kwenda eneo jingine na wengine hawatazaliana jambo ambalo linahatarisha ongezeko la wanayama pori.

Wanyama wanapohama na kwenda eneo jingine inasaidia ongezeko la wanyama wa kizazi tofauti na pia kuondokana na magonjwa.

Ni vizuri kuwa serikali imeona mgogoro baina ya wanavijiji na hifadhi, hivyo ni vyema pia kudhibiti shughuli za binadamu katika hifadhi kwani zinasababisha kuvuruga maisha na ikolojia ya wanyama .

Baada ya serikali kuagiza kumalizika migogoro ni vyema sheria ya kukataza kuwepo kwa shughuli za kibinadamu katika maeneo hayo zikasisitizwa na wananchi wakaelimishwa umuhimu wa ulinzi na usalama wa wanyama.

Katika jitihada hizo serikali ije na mkakati ambao utasaidia  kulinda hifadhi  ili zisiendelee kuvamiwa na mipaka ya vijiji ikishatambuliwa wananchi waheshimu na kuthamini rasilimali hiyo.

Ni vyema kuangalia maeneo la shoroba ambako wanyama hupata ili kuyapa ulinzi kwani yamewavimiwa na wananchi na wengine wamefanya shughuli za ujenzi ingawa  kuna sharia za kulinda sehemu hizo.

Katika mkakati wa kurasimisha vijiji 366 ni vyema serikali ikachukua hatua kwenye  maeneo ya hifadhi pamoja na shoroba ili kuhakikisha kuwa zinakuwa salama  kuwawezesha wanyama kuhama kwenda katika eneo jingine ili kuwezesha kuongezeka kwa viumbe hao  katika hifadhi.

Ni vyema wananchi wakaelimishwa kikamilifu ili wawe walinzi, hii itarahisisha upatikanaji na utoaji wa  taarifa ili kuchukua hatua na kuepusha athari kwa wanyamapori ambao ni  rasilimali  muhimu kwa taifa na tegemeo la kiuchumi pia.