Watanzania mjue utamaduni unatufariki!

25Oct 2020
Joseph Kulangwa
Nipashe Jumapili
FIKRA MBADALA
Watanzania mjue utamaduni unatufariki!

KWA wale mliozaliwa mijini, hamtanibishia nikiwaambieni kuwa wakati mnazaliwa na kupata fahamu na kutambua hiki na kile, mlijikuta mkiwasiliana na wazazi wenu kwa Kiswahili. Anayebisha na anyooshe kidole nimuumbue mbele ya wazazi wake.

Na mpaka sasa baadhi yenu pamoja na kubalehe na kuvunja nyungo, hamjui hata lugha za baba na mama zenu, mnazungumza Kiswahili na kuokoteza neno moja moja la kilugha kutoka kwa wazazi hao. Sana sana wengi wenu mtajua kusalimia na kunyamaza na hata mkijibiwa hamwezi kurudishia. Nani anabisha?

Lakini pamoja na yote hayo hamjahoji kwa nini hamwelewi lugha za baba na mama zenu wa kuwazaa. Na wala hamshangai kwa nini. Ni kwa sababu mnapata kila mnachokitaka kwa kutumia lugha ya Kiswahili. Hamwoni tena umuhimu wa kujifunza lugha za jadi, kwa sababu mnaona hazikusaidieni.

Mnaona kabisa, kwamba Kiswahili kinakuunganisheni na jirani zetu, kinakuunganisheni shuleni, kinakuunganisheni vyuoni, makazini na hata vijiweni. Kama ndivyo sasa Kijita cha nini? Kihaya cha nini? Kisubi cha nini? Kisukuma cha kazi gani? Kizaramo kinakusaidieni nini?

Wanaotaka kujielimisha ndio wataanza kuuliza kwa nini hatuzungumzi kikwetu na badala yake tunazungumza Kiswahili 24/7? Wanaotaka kuelimisha watajibu kwa sababu Kiswahili ndiyo lugha iliyotuunganisha Watanganyika, na hatimaye Watanzania, wakati tunadai Uhuru. Kiswahili ndicho kinatufanya tudai haki zetu hata sasa.

Wafafanuzi watakwambia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere (PKA) na wenzake, walitumia lugha hiyo adhimu kutuunganisha katika kudai uhuru wa kujitawala, na hatimaye tukafanikiwa na hivyo kuendelea kukitumia kujiletea maendeleo tuliyonayo sasa na tunayoendelea kuyasaka.

Kwa muktadha huo huo, ndiyo sababu tunaupenda utamaduni wetu na kujivunia. Tutajiuliza utamaduni upi sasa? Wa makabila yetu au wa Kiswahili? Utajibiwa ni wa Kiswahili uliotokana na mchanganyiko wa makabila yetu. Je, ni kweli utamaduni wetu tunao na ni upi? Unajitanabahisha vipi? Kwa nyimbo, ngoma, mashairi, mavazi, chakula, muziki, mitindo? Jibu ni vyote.

Lakini wadadisi wakikaa chini na kuchunguza hicho tunachikiita utamaduni wetu, wanabaki na maswali mengi na wanapokosa majibu wanabaki kuduwaa. Tunaimba nyimbo gani sasa? Tunacheza ngoma zipi? Tuna mashairi yapi, kwani kuna waghani wangapi waliopo? Tunavaaje? Chakule chetu je ni kile? Wana mitindo wetu je, ni wa kitamaduni? Hapana! Ndilo jibu.

Zamani tulisikia nyimbo redioni, majukwaani na kwingineko zikihimiza Utanzania, kina Mzee Mwinamila, kina Mzee Makongoro wa Hiari ya Moyo? Ngoma za kina Nyunyusa ambazo sasa tunaona zinafanyiwa ‘remix’, mashairi yako wapi redioni? Hahahaaa, tunavaa kata-kei na vimini, tunakula chipsi na baga, tunacheza Bongofleva, mitindo ya Ughaibuni! Watanzania hao!

Miaka fulani hivi, tukaibuka usingizini na kuhanikiza kuja na vazi la Taifa. He! Tukaishia kukatakata Bendera ya Taifa na kujibandika viraka kwenye Kaunda Suti! Wengine wakabandika mifuko ya Bendera ya Taifa, wengine ukosi wa Bendera hiyo nakadhalika.

Enzi hizo tukipokea wageni wetu wa kitaifa kwa ngoma na nyimbo zetu za Kitanzania, zilizojaa maadili ya Mtanzania, zikionesha umoja, ushirikiano, ukarimu na amani ya nchi yetu kwa wageni. Nyimbo na ngoma za staha zaidi zilioneshwa.

Juzikati hapa nikashangaa mgeni wa kitaifa akipokewa kwa wimbo wa Bongofleva unaitwa Uno. Baadhi ya maneno yake yaliyosikika na yanayosikika hadi leo, ni eti “Uno linawaokoa makahaba…” Jamani, mgeni wetu kweli wa kitaifa, anaimbiwa wimbo huo na mwimbaji anakatika viuno mbele yake!!

Tukae tena tujiulize tunakosea wapi? Hatuna nyimbo za maana? Hatuna midundo na mikong’osio ya utamaduni wa Mtanzania kweli? Hivi ni lazima tuige midundo ya kigeni na kuingiza Kiswahili na kutamba eti tunatangaza utamaduni duniani? Tutafiti.

Kwa nini tulitelekeza Achimenengule ya John Komba (PKA)? Tuijenge Singeli basi, naona inanukia Kitanzania zaidi, mnaonaje wananzengo wenzangu? Alamsiki.