Watanzania tusilalamike, tuna cha kujifunza Afcon

29Jun 2019
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Watanzania tusilalamike, tuna cha kujifunza Afcon

BAO la dakika ya 80 lililofungwa na Michael Olunga liliwanyong'onyesha Watanzania wote waliokuwa wakifuatilia mechi ya fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019 zinazoendelea kuunguruma nchini Misri.

Olunga huyu huyu ambaye misimu mitatu iliyopita alikuwa akigombewa na Klabu za Simba na Azam, lakini Gor Mahia ikamuuza Ulaya, ndiye alikuwa mwiba kwenye safu ya ulinzi ya Taifa Stars.

Kilichowaumiza zaidi Watanzania ni kwamba hadi mapumziko Stars ilikuwa inaongoza kwa mabao 2-1 na kwa jinsi soka lilivyokuwa likitandazwa, ilitegemewa kutoka na ushindi kwenye mechi hiyo.

Ushindi ulikuwa bayana kwa sababu Harambee Stars, timu ya Taifa ya Kenya, haikuwa ya kutisha sana kama ilivyokuwa kwa Senegal. Hawa ni majirani, lakini pia aina ya soka linafanana.

Hiyo yote haikuwa dawa, mwisho wa siku, Stars ilikubali kichapo cha mabao 3-2, na kuwa ni kipigo cha pili kutoka kile cha kwanza cha mabao 2-0 dhidi ya Senegal.

Kumekuwa na maneno mbalimbali kama kawaida ya Watanzania kutoka huku na kule, kila mmoja akieleza kwa namna yake sababu za kufungwa. Lawama kama kawaida hazikosekani.

Pamoja na yote haya yanayotokea nchini Misri, Watanzania wanapaswa kujua kuwa Taifa Stars inacheza michuano hiyo kwa mara ya kwanza baada ya miaka 39. Mara ya mwisho ilikuwa ni 1980, fainali zilizofanyika nchini Nigeria, baada ya kufuzu mwaka 1979, miaka 40 iliyopita.

Hii inaonyesha kuwa Stars ilikuwa bado changa kwenye michuano hiyo kuweza kufanya vizuri.

Kuna nchi ambazo ni kawaida yao kutinga hatua za fainali, lakini zina miaka kibao hazijachukua ubingwa na badala yake zinatolewa mapema tu kwenye michuano hiyo, sembuse Tanzania ambayo imetinga baada ya miaka mingi kupita?

Kucheza tu hatua hii kwa Taifa Stars inapaswa kupongezwa na wala si kubezwa na kinachotakiwa hapa ni kuchukulia kama changamoto kwa kile kilichotokea.

Kwa serikali na Shirikisho la Soka nchini (TFF), wanapaswa kujifunza kwanza kuwa soka kwa sasa ni kazi kama kazi zingine na si burudani baada ya kazi. Na wala hakuna siasa katika hili.

Wachezaji wetu wanapaswa watengenezewe mazingira ya kutoka kwenda kucheza nje ya nchi na si kuweka kanuni za kuwazuia wageni ili kupata Stars inayotokana na klabu za Simba, Yanga na Azam.

Ukiangalia hata wachezaji wa Stars wanaocheza nje ya nchi wanaonekana kuwa wako vizuri kuliko wachezaji wanaocheza ligi ya ndani. Ukimwangalia Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu, Simon Msuva na sasa Farid Mussa, wanaonekana kabisa kuna vitu adimu kabisa tofauti na wenzao.

Hata Kenya ambao ni majirani zetu wana idadi kubwa ya wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi kuliko Tanzania.

Badala ya kulalamikia kwa nini tumefungwa, nani kasababisha timu ifungwe, inapaswa kuandaa michuano mingi ya vijana, na wale watakaoonekana wana vipaji, basi serikali na TFF ibebe jukumu la kuwaombea kwenda kwenye academy za nchi marafiki kwa ajili ya kutunzwa, kufunzwa soka na kusomeshwa ili waweze kuikomboa nchi miaka ya mbele na si wachezaji kubaki hapa hapa na kukaa mitaani, kitu ambacho kinasababisha viwango vyao kushuka na maisha yakishakua magumu wanaacha soka na kufanya shughuli zingine za kujikimu kimaisha.

Ukiziangalia timu nyingi zenye wachezaji wanaocheza nje ya nchi, kama vile Senegal, Nigeria, Cameroon, pamoja na kwamba wana miili mikubwa na nguvu, si kwamba wana vipaji sana, ila wana misingi mizuri ya kukuzwa kisoka na wanatumia miili na akili zao vizuri zaidi kuliko wachezaji ambao wanatoka tu mitaani. Tunaondoka Afcon, lakini tuondoke na kitu tulichojifunza.