Watanzania wachache wanachangamkia hati fungani

13May 2016
Raphael Kibiriti
Nipashe
Mtazamo kibiashara
Watanzania wachache wanachangamkia hati fungani

KATIKA safu hii wiki iliyopita , tuliangazia fursa ya uwekezaji wa hati fungani zilizotolewa na benki ya NMB, kwa wananchi wa kada zote za maisha pamoja na wafanyabiashara.

Katika kukumbushana, tulisema benki ya NMB, imezindua uuzaji wa hati fungani kwa wananchi wote, ikilenga kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 20 hadi 25, itakazozitumia kutoa mikopo kwa Watanzania ili kuboresha shughuli zao za kiuchumi.

Shughuli ya kuanza kwa uuzaji wa hati fungani hizo ilizinduliwa wiki hii, Jumatatu na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo Ineke Bussemaker.

Kwa mujibu wa Bussemaker, hati fungani hizo zitauzwa kwenye matawi yote takriban 176 yaliyotapakaa pande zote nchini, lakini pia kupitia kwa Mawakala wa Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE), ambao pia wanapatikana katika mikoa yote.

Aidha Bussemaker alisema mwekezaji wa hati fungani hizo atakuwa akilipwa riba ya asilimia 13 kwa mwaka itakayokuwa ikilipwa kila baada ya miezi sita, katika kipindi cha miaka mitatu ya kuiva kwake.

Hivyo safu hii inahimiza wafanya biashara wa ngazi zote, lakini na wananchi wote kuichangamkia fursa hii ya uwekezaji, katika kipindi cha mwezi wa kuuzwa kwa hati fungani hizo.

Kwa mujibu wa Bussemaker, na kama tulivyoona wiki iliyopita kiwango cha chini cha mfanyabiashara ama mwananchi mwingine kushiriki kwenye ununuzi wa hati fungani hizi ni shilingi 500,000 na kuendelea.

Kilichonifanya niwahimize wapenzi wa safu hii kuzichangamkia hati fungani hizi, ni takwimu za ushiriki wa wafanyabiashara na Watanzania kwa ujumla, kwenye uwekezaji wa hati fungani mbalimbali nchini kwa hivi sasa.

Kwa mujibu wa Meneja Miradi na Maendeleo ya Biashara wa DSE, Patrick Msusa, ni asilimia moja tu ya Watanzania takribani milioni 50 wanaoshiriki kwenye uwekezaji wa hati fungani kwa hivi sasa.

Asilimia moja ya Watanzania milioni 50, ina maana tunaongelea watu 500,000 tu.

Kwamba idadi hiyo ya watanzania 500,000 inawajumuisha wananchi wa kada zote yaani wafanyabiashara, wafanyakazi, wakulima na watu wengine, wanaoitumia fursa hii ya uwekezaji kupitia hati fungani.

Msusa akasema, thamani ya uwekezaji wa hati fungani kwa sasa unafikia kiasi cha shilingi trilioni 4.7, ama bilioni 4,700, ambacho kimsingi ni kiasi kikubwa sana cha fedha.

Katika hesabu ndogo na ya kawaida ina maanisha kuwa, asilimia moja ya Watanzania wote ndio wanamiliki kiasi hicho chote kikubwa cha fedha, huku asilimia 99 ikiwa imeachwa solemba!

Sasa mojawapo ya sababu kubwa ya kuwapo kwa hali hii, ni ya wananchi wengi wakiwamo wafanyabiashara kutofahamu uwapo wa fursa za aina hii, pia faida ya kuwekeza katika aina hii ya uwekezaji.

Ukipiga hesabu ndogo juu ya takwimu hizo hapo juu za Watanzania 500,000, wanaofaidika na kiwango cha shilingi trilioni 4.7 za thamani ya hati fungani iliyoko sokoni sasa, mtu ataona namna wachache walivyochangamkia fursa hii, wakafaidika na wanaendelea kufaidika.

Na ndiyo maana safu hii inakuhimiza wewe mfanyabiashara na wananchi wengine kuchangamka sasa, kwani wakichelewa, ni hao hao wachache ndiyo watakazichangamkia.