Watoto waliolelewa kikamilifu ni tija kitaifa

25Feb 2020
Gwamaka Alipipi
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Watoto waliolelewa kikamilifu ni tija kitaifa

ZAIDI ya nusu ya idadi ya Watanzania ni watoto. Hivi sasa, kuwekeza kwa watoto kunanufaisha si familia nyingi pekee bali jamii na ni kwa mustakbali wa Tanzania

Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 inadhihirisha kuwa Tanzania ina idadi ya watu milioni 45, kati yao asilimia 44 ni wenye umri chini ya miaka 15.

Ili kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati inawezekana iwapo watoto wetu watakuwa na afya, wenye kupata lishe bora, elimu bora na kulindwa dhidi ya vurugu, udhalilishaji na unyonyaji.

Kila nchi iliyofikia kuwa na maendeleo ya kiuchumi ya kipato cha wastani imewekeza kwa watoto kwa kiwango kikubwa.

Hivi sasa kuwekeza kwa watoto kwenye elimu bora, huduma za afya zilizoboreshwa na kuwalinda watoto dhidi ya vurugu na udhalilishaji huzaa matunda yanayosababisha kuwapo kwa uchumi imara, kupungua kwa uhalifu na kuwapo kwa familia zenye afya bora na zilizolelewa kwenye maadili bora.

Vilevile endapo serikali ikianzisha utaratibu wa kuhakikisha kila mtoto anayezaliwa anafunguliwa bima ya afya itasaidia kwa kiasi kikubwa kumwezesha mtoto huyo kukua katika afya iliyo bora na malezi mazuri.

Maendeleo makubwa yanaweza kupatikana kwa kuzihamasisha jamii zetu, kuongeza uwajibikaji na uwazi na kuhakikisha kuwa sheria ya watoto inatekelezwa kikamilifu ili kuwalinda watoto wetu.

Matumizi mazuri ya rasilimali zilizopo kwa kuboresha huduma muhimu na kuimarisha fursa kwa watoto kutaziwezesha familia nyingi kujitoa katika umaskini.

Kwa mujibu wa taarifa za Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto Duniani (Unicef) zinaeleza vifo vya watoto vimepungua nchini kwa asilimia 25, na Tanzania inaendelea vizuri kuelekea kwenye lengo la maendeleo ya milenia kuhusiana na uhai wa watoto.

Hata hivyo zaidi ya watoto 445 waliochini ya umri wa miaka mitano hufariki kila siku, na zaidi ya watoto 140 kati yao ni watoto walio na umri chini ya mwezi mmoja.

Kadhalika, kila saa moja kuna mwanamke anayefariki kwa kutokana na matatizo ya mimba au kujifungua, hivyo serikali inapaswa kuwekeza kwenye huduma za afya nafuu ambako kutaokoa maisha ya maelfu ya wananchi.

Serikali inahitajika kuweka mfumo bora zaidi wa afya utakaokuwa na wafanyakazi zaidi, vituo vya afya vyenye vifaa vya kutosha, ufuatiliaji na usimamizi mzuri na uwajibikaji mkubwa, sera, sheria, miongozo na miundo yote inayohusiana na afya, itoe kipaumbele kwa wanawake na watoto.

Matukio ya ukatili dhidi ya watoto yamekuwa yakishamili kila siku, tumekuwa tukiyasikia kupitia vyombo vya habari, mara mtoto kachomwa moto mikono au mara utasikia kafichwa kwenye boksi kwa miaka mine.

Jamii inapaswa kutambua na kujua uthamani wa mtoto kwa kuwalea na kuwatunza vizuri, kwani ukimlea mtoto kimaadili leo, kesho atakuwa hazina yako.

Watoto wengi wenye ulemavu wananyimwa haki ya kupata elimu, wengi hufungiwa ndani na kuwekwa katika mazingira ya kikatili.

Sheria zinazohusiana na watu wenye ulemavu zinapaswa kukamilishwa na kutekelezwa, wahisani washirikishwe ili kuhakikisha kunakuwapo na bajeti kwa ajili ya utekelezaji, ikiwa ni pamoja na kuundwa kwa chombo cha uratibu.

Upatikanaji wa huduma maalumu za watoto wenye ulemavu unapaswa kuzidishwa, ikiwa ni pamoja na mipango ya jamii ya kuwawezesha kuishi maisha ya kawaida, vituo vya huduma vya matibabu mahususi na kuwa na wafanyakazi waliopatiwa mafunzo ili watoto wote wenye ulemavu waweze kupatiwa huduma muhimu za kuwawezesha kuishi maisha ya kawaida, pamoja na vifaa wanavyovihitaji.

Aidha, serikali inapaswa kukumbuka kuwa ule msemo usemao mtoto ni taifa la kesho umepitwa na wakati, bali mtoto ni taifa la sasa na mtoto umleavyo ndiyo akuavyo.