Watu wengi wanaweza kuwa vimelea vya TB bila kuugua

12Jun 2016
Jackson Paulo
Nipashe Jumapili
Afya
Watu wengi wanaweza kuwa vimelea vya TB bila kuugua

KIFUA kikuu (TB) ni ugonjwa wa kuambukiza ambao mara nyingi hushambulia mapafu. Maradhi haya husababishwa na bakteria wajulikanao kama Mycobacterium tuberculosis (MTB).

Vimelea hawa waenezao ugonjwa wa TB husambaa kutoka kwa mgonjwa kwenda kwa mtu mwingine kupitia chembe ndogo za maji maji ya mwili ambayo mgonjwa hutoa wakati akikohoa au kupiga chafya.

Ikumbukwe kila mtu ambaye ama ana ukaribu au amekutana na mgonjwa, vimelea vya TB vinaingia mwilini, lakini si lazima kuugua kwani tatizo hutokea pale kinga ya mwili inaposhuka.

Zama hizi kiwango cha maambukizi ya ugonjwa huu kinaongezeka kwa kasi tofauti na hapo awali kutokana na kuwapo na kusambaa kwa ugonjwa wa Ukimwi unaosababishwa na Virusi Vya Ukimwi (VVU) vinavyodoofisha kinga ya mwili na kusababisha ushindwe kupambana na bakteria wanaoeneza TB.

Dalili za kifua kikuu

Katika hali ya kawaida, mwili wa binadamu huhifadhi bakteria wa kifua kikuu pasipo kuonekana madhara yoyote kwa kuwa kinga ya mwili huzuia uwezekano wa ugonjwa kutokea.

Kwa maana hiyo zipo aina mbili za ugonjwa wa kifua kikuu;
Aina ya kwanza ni ile ambayo bakteria wa kifua kikuu wanaishi mwilini lakini hawasababishi dalili yoyote au ugonjwa.

Kitaalamu huitwa Latent T au Inactive TB. Aina hii ya kifua kikuu haiwezi kuambukiza kutoka mtu mmoja kwenda mwingine.

Hata hivyo, huweza kubadilika na kusababisha dalili za ugonjwa kujitokeza kwa hiyo matibabu ni muhimu kwa mtu mwenye aina hii ya ugonjwa ili kuudhibiti.

Aina ya pili ya ugonjwa huu ni ile ambayo mtu huugua na ugonjwa kusambaa kitabibu huitwa Active TB.

Hali hii hujitokeza majuma machache tu baada ya mtu kukutana na bakteria hawa au huweza kujitokeza baada ya miaka kadhaa.

Dalili

Zipo dalili mbalimbali za kifua kikuu ambazo hujitokeza mara tu mtu anapoanza kuugua.

Mojawapo ni kukohoa kwa kipindi cha wiki tatu au zaidi, kukohoa damu, maumivu sehemu ya kifua wakati wa kupumua au kukohoa, kupungua uzito ghafla, kujihisi uchovu mara kwa mara, homa kali, kutokwa jasho nyakati za usiku pamoja na kukosa hamu ya kula.

TB huathiri sehemu nyingine pia za mwili ikiwamo figo, uti wa mgongo au ubongo. Lakini ugonjwa wa kifua kikuu unapojitokeza sehemu nyingine nje ya mapafu dalili huwa za tofauti kulingana na kiungo kilichoathirika.

Kwa mfano, ikiwa uti wa mgongo ndio ulioathirika basi mgonjwa hupata maumivu ya uti wa mgongo na ikiwa figo zimeathirika basi tatizo ni kupata haja ndogo yenye damu.

Lini ni wakati wa kumwona daktari?

Unapaswa kumwona daktari iwapo unapatwa na homa, kupungua uzito kusikoeleweka, kutokwa jasho nyakati za usiku, pamoja na kikohozi kisichokomaa (bila makohozi).

Hizi ni dalili kuu za kifua kikuu japokuwa viashiria hivi huweza pia kujitokeza kutokana na tatizo jingine mwilini ndiyo maana hali ya ugonjwa hubainika mara baada ya kufanyiwa vipimo maalum.

Lipo kundi la watu ambao wapo katika hatari zaidi ya kupata TB na hivyo hupaswa kufanyiwa vipimo mara kwa mara ili kubaini maambukizi.

Kundi hili ni pamoja la watu wenye maambukizi ya VVU, wanaotumia dawa za kulevya kwa kujidunga sindano, wenye ukaribu na mgonwa wa kifua kikuu pamoja na wanaowahudumia.

Chanzo cha Kifua Kikuu

TB husababishwa na bakteria ambaye husambaa kutoka kwa mtu mmoja kwenda mwingine kupitia chembe ndogo ndogo za majimaji ambazo humtoka mtu kwa njia ya hewa.

Kusambaa kwa ugonjwa huu hutokea pale mtu mwenye ugonjwa anapokohoa, kuzungumza, na anapopiga chafya, kucheka, kutema mate au kuimba .

Kifua Kikuu na VVU

Tangu kugundulika kwa ugonjwa wa Ukimwi mnamo miaka ya 198, idadi wagonjwa wa kifua kikuu wameongezeka kwa kasi kutokana na ongezeko la maambikizi ya VVU.

Maambukizi ya virusi vya Ukimwi husababisha kushuka kwa kinga ya mwili na kufanya vigumu kwa mwili kuwa na uwezo wa kudhibiti bakteria wanaosababisha kifua kikuu.

Kwa maana hiyo watu wenye maambukizi ya HIV wapo katika hatari kubwa zaidi ya kuugua kifua kikuu, hii ina maana kwamba hata kama hajapata maambukizi kutoka kwa mgonjwa wa kifua kikuu bakteria wa TB waliopo mwilini humsababishia maradhi.

Kifua kikuu usugu
Aina nyingi za bakteria waenezao kifua kikuu ni amabo wameshajenga usugu dhidi ya dawa zinazotumika kutibu ugonjwa huu, kwa hiyo mtu mwenye TB lazima atumie dawa za aina nyingi na kwa kipindi cha miezi kadhaa ili kutokomeza maambukizi na kuzuia uwezekano wa bakteria kujenga usugu dhidi ya dawa.

Sababu kubwa inayosababisha ugonjwa wa kifua kikuu kuendelea kuangamiza watu wengi ni kuongezeka kwa aina nyingi za bakteria wenye usugu dhidi ya dawa.

Tangu dawa ya kwanza ya kifua kikuu kugundulika na kuanza kutumia miaka zaidi ya 60 iliyopita, baadhi ya bakteria wamejijengea uwezo wa kustahimili sumu ya dawa na vimelea hawa kuendelea kueneza usugu huu kwa vizazi vyao.

Itaendelea