Watumiaji wa methadone wabadilishe mazingira

10Jul 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Watumiaji wa methadone wabadilishe mazingira

MATUMIZI ya dawa za kulevya yamo katika orodha ya matatizo ya kitaifa, yanayoendelea kuikumba jamii, huku waathirika wakubwa wakiwa ni vijana. Ni taabu, kwani hao kimsingi, ndiyo wanaotegemewa nguvu kazi ya taifa.

Hata hivyo, serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali zikiwamo za uanzishaji msako dhidi ya wauzaji na waingizaji dawa hizo, ikiwa njia ya kukomesha matumizi ya dawa hizo nchini.

Mbali na hilo, imeanzisha nyumba za kutunza waathirika wa dawa hizo na pia kuanzisha vituo maalum, ambavyo waathirika wanaenda kunywa dawa za kuwawezesha kuachana na ‘uteja’ na wanapofikia nafuu, wanarudi nyumbani.

Hata hivyo, huenda juhudi hizo za serikali zisizae matunda kama inavyotarajiwa, kutokana na hali halisi inayowakabili 'mateja', hasa kuendelea kuishi kwenye mazingira yaliyosababisha wakajiingiza katika tatizo hilo.

Wengi wao ni wale walioshawishiwa kwenye vijiwe vyao na kujikuta wakutumia dawa hizo, na sasa wameamua kuacha na kuanza kutumia dozi ya dawa za kulevya, hivyo ni vyema wakaishi mazingira mengine.

Ninaamini kwamba kuendelea kuishi katika mazingira ya awali ni rahisi kushawishiwa kurudia matumizi ya dawa za kulevya, ambayo ni hatari kwa maisha yao.

Ipo haja ya kujenga nyumba nyingi kwa ajili ya watumiaji wa dawa hizo na walioamua kubadilika, ili wasiendelee kuishi katika mazingira ya awali, yanayoweza kuwarudisha kwenye hatari.

Pia, jukumu la kudhibiti vijana kujitumbukiza kwenye matumizi ya dawa, linaanzia katika ngazi ya familia, pia jamii haina budi kushirikiana katika kuelimisha, kuzuia, kurekebisha na kuwaponya waathirika wa dawa hizo.

Njia hiyo na ile ya kuwaondoa katika mazingira awali ni jambo muhimu kwa ajili ya kuwarejeshea utu na heshima yao kama binadamu ndani ya jamii, hasa wale wanaoamua kujitenga na uteja.

Ikumbukwe, mtu anapotumia dawa za kulevya na kisha akanywa methadone, ni rahisi kupoteza maisha, kwani hiyo ni kwa mujibu wa wataalamu wa afya wanaowatibu waathirika wa dawa hizo.

Dawa zote ni za usingizi, hivyo aliyeacha uteja akaitumia kisha akarudi ‘kijiweni’ na dawa za kulevya, anajiongezea usingizi mara mbili, hali ambayo ni hatari kwa uhai wake.

Hivyo wakati huu ambao serikali imefanikiwa kudhibiti matumizi ya dawa hizo nchini, kuna haja ya kuhakikisha wale ambao wameacha dawa hizo hawapati mwanya wa kurudia tena, bali wawe mabalozi wema kwenye jamii.

Pamoja na hayo, wale ambao wamekuwa wakitafuta mbadala wa dawa hizo wadhibitiwe ili warudi kwenye mstari, badala ya kuhangaika huku na huko kwa lengo la kuendelea na uteja.

Ninasema hivyo, kwa sababu baadhi ya vijana wanadaiwa kutumia gundi na dawa tiba zenye asili ya kulevya kama njia mbadala ya dawa za kulevya, ambazo kwa kiasi kikubwa zimedhibitiwa nchini.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana, Sera na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, anasema hayo wakati akizungumza na wana habari katika Siku ya Maadhimisho ya Kupiga vita Dawa za Kulevya.

Anasema, tatizo la dawa za kulevya katika jamii ni mtambuka, linalohitaji ushirikiano wa sekta mbalimbali kwa ajili ya kupambana nalo, kwa vile udhibiti wa dawa hizo, umesababisha watumiaji kuhamia kwenye bhangi, mirungi, gundi na dawa tiba zenye asili ya kulevya.

"Matumizi ya gundi ni eneo ambalo limewekewa mkakati maalumu; tumegundua watoto wanatumia, kimsingi tunaangalia uwezekano wa kuweka utaratibu ili matumizi ya gundi yadhibitiwe na isitumike kinyume," anasema.

Lakini inaelezwa kuwa Tanzania inakadiriwa kuwa na jumla ya waathirika wa dawa za kulevya kati ya 200,000 hadi 350,000, kwamba, kati yao waathirika takribani 30,000 wanatumia dawa hizo kwa kujidunga.

Wiziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu ndiye anayesema hayo wakati akizindua kituo cha muda cha kutoa huduma ya Methadone kwa waraibu wa dawa aina ya heroin mkoani Tanga.

Kwamba, kuna makadirio ya asilimia 35 ya kiwango cha maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) kwenye jamii ya waathirika hao, hivyo hiyo yote ni dalili tosha kuwa ipo haja ya kuchukua hatua zaidi kuokoa waathirika.