Wauguzi hawa mfano wa kuigwa kupunguza mimba za wanafunzi

13May 2021
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wauguzi hawa mfano wa kuigwa kupunguza mimba za wanafunzi

JANA ilikuwa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani, ambayo kitaifa yalifanyika mkoani Manyara, yakiwa na kaulimbiu: “Wauguzi sauti inayoongoza, Dira ya huduma ya afya”.

Maadhimisho hayo hufanyika Mei 12 kila mwaka, hapa nchini, zilifanyika shughuli mbalimbali ikiwamo za kuelimisha wanafunzi mada mbalimbali zinahusu utunzaji wa afya.

Miongoni mwa wanafunzi waliopata elimu hiyo, ni wa Shule ya Sekondarii Malamba-Mawili, jijini Dar es Salaam, ambao waliofundishwa na wauguzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wa Upanga na Mloganzila.

Wauguzi hao walikuwa katika shule hiyo juzi, wakifundisha fani ya uuguzi, athari za matumizi ya dawa za kulevya, jinsi ya kujikinga na mimba za utotoni na kufahamu njia za kujikinga na magonjwa ya kuambukiza.

Moja ya magonjwa hayo ya kuambukiza ni UKIMWI. Lakini wanafunzi hao, walifundishwa kuhusu kutambua mabadiliko ya mwili yanayotokana na ukuaji na madhara ya mimba za utotoni.

Walihamasisha pia wanafunzi kujiunga na fani ya uuguzi pamoja na jinsi ya kuboresha afya ya jamii, afya ya akili, afya ya uzazi, usafi na namna ya kutoa huduma ya kwanza shuleni.

Binafsi ninaamini kuwa hatua zilizofanywa na hospitali hiyo zinafaa kuigwa na kuzindeleza katika shule mbalimbali nchini, ili kusaidia kupunguza tatizo la mimba shuleni ambalo linaendelea kuwambuka wanafunzi.

Mkuu wa Wilaya Tunduru mkoani Ruvuma, Julius Mtatiro, alisema katika kipindi cha miezi tisa kuanzia Januari hadi Julai mwaka 2019 jumla ya wanafunzi 119 walikatisha masomo kwa kukumbwa na tatizo hilo.

Hiyo ni wilaya moja tu na kwa kipindi kifupi cha miezi tisa, hali kama hiyo inawezekana ipo katika wilaya zote nchini, na kama ndivyo, tatizo hilo ni kubwa ambalo linatakiwa kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu.

Mimba hizo katika Wilaya ya Tunduru, zilimfanya mkuu wa wilaya hiyo kuwaomba wazee washirikiane kikamilifu na serikali kwa ajili ya kutokomeza tatizo hilo.

Mtatiro anaeleza kuwa, sababu kubwa ya kuwapo kwa mimba wilayani mwake ni kukosa uangalizi wa wazazi, kwa kuwa jamii inawaacha watoto kujihudumia wenyewe.

Lakini pia anasema wazazi kutojali wanafunzi wanapopata mimba na mila na desturi hasa unyago, vinachangia kuwapo kwa ongezeko kubwa la tatizo hilo ambalo hukatisha ndoto za wanafunzi.

Kwa hali hiyo, ni wazi kwamba, elimu kama hiyo iliyotolewa na wauguzi inaweza kuwa na manufaa makubwa katika vita dhidi ya mimba shuleni au mimba za utotoni ambazo ni kero.

Pamoja na jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau wake, ipo haja pia kuwekwa mkakati wa kutembelea shule zote nchini mara kwa mara na kutoa elimu kama hiyo.

Wauguzi hao wametoa elimu hiyo wakati huu wa maadhimisho ya siku yao, baada ya hapo inawezekana wakasubiri hadi maadhimisho ya mwaka ujao, hali ambayo inaweza isizae matunda kwa kutokuwa endelevu.

Kwa maana hiyo, ingependeza iwapo wadau wote wataunga mkono kile ambacho wauguzi hao wamekianzisha na kukiendeleza kwa kuzunguka katika shule zote nchini mara kwa mara na kuwaelimisha wanafunzi.

Kimingi, wauguzi waliokwenda kutoa elimu ya afya katika Sekondari ya Malamba-Mawili, wamefanya jambo jema ambalo ni mfano wa kuigwa, ila na wasiishie hapo, uwe ni utaratibu endelevu katika shule mbalimbali.

Ikumbukwe kuwa mara nyingi huwa kuna taarifa za kuwapo kwa mimba shuleni, lakini suala la usalama wa afya zao halijulikani, hali ambayo ni wazi kwamba ipo haja ya kuwaelimisha ili waepuke pia madhara ya kiafya.