Wauguzi na wakunga, mkasa huu una maana mwenzio akinyolewa…

27Jan 2021
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wauguzi na wakunga, mkasa huu una maana mwenzio akinyolewa…

KAZI ni wito na iko kama zingine. Hivyo, inatakiwa mtu asipende kazi yake kwa sababu ndio mtaji wa maendeleo yako.

Tunafanya kazi, lakini tunatofautiana aina ya kazi hizo. Hiyo haijalishi kila mfanyakazi yeyote kupitia kazi yake, anaweza kubadilisha maisha na kupiga hatua yoyote ya kimaendeleo.

Inatakiwa mtu uipande kazi inayokufanya wewe upate ugali na familia yako. Hapo, unaposema kuipenda kazi, tunamaanisha hata wanaokuzunguka katika kazi unayoifanya inatakiwa nao uwapende.

Kama mtu unaipenda kazi yako unapaswa nao kuwapenda wenzako na kama tunashindwa kuwapenda wenzako, basi hautaweza kufanya kazi vizuri.

Pia si busara kuchukua hatua yenye sura ya vipigo kwa vibao mama mjamzito ni kosa kisheria.

Hivi karibuni kumetokea tukio la mtumishi wa kituo cha afya alimpiga mama mjamzito aliyefika kupata huduma nyeti katika kituo hicho.

Ni hali iliyozaa makuu, mhusika kachukuliwa hatua za kisheria.

Nimependa namna Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, limechukua hatua mara moja katika kituo cha Afya Mazwi, muuguzi alilalamikiwa kwa kosa la kumpiga mhitaji wa huduma ya kujifungua kituoni, mwezi huu.

Mwenyekiti wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, Abner Mathube, alisema Baraza limemtia hatiani mlalalamikiwa chini ya Sheria ya Uuguzi na Ukunga.

Mathube anasema, Baraza lilichambua maelezo ya mlalamikiwa, mlalamikaji pamoja na mashahidi kuhusu kosa la kwanza la kumpiga mgonjwa, jambo ambalo dhahiri ni kinyume na Sheria ya Uuguzi na Ukunga Tanzania.

Katika kosa la kwanza  lililotolewa ushahidi, ulithibitisha kuwa mlalamikiwa alimpiga mlalamikaji na mtuhumiwa alikiri kumpiga mlalamikaji.

Ni aina ya madai yalimfikisha mlalamikiwa katika kosa la kushindwa kusimamia maadili na weledi wa kitaaluma. Ilithibitika kuwa mtuhumiwa  alishindwa kufuata utaratibu wa utoaji huduma za uuguzi na ukunga kwa mlalamikaji.

Pia ni madai yaliyoenda mbali kwa kushindwa kuchukua na kuhifadhi taarifa za vipimo vya mgonjwa, kushindwa kufuatilia mwenendo wa uchungu wa mgonjwa wakati wa kumpokea katika kituo cha kutoa huduma na kuruhusu mtu ambaye sio mtaaluma kumpima mlalamikaji (mgonjwa).

“Kwa kuzingatia utetezi wa mlalamikiwa na ushahidi uliotolewa na mlalamikaji na mashahidi, umethibitisha mashtaka yote kama alivyoshtakiwa na mlalamikaji,” anasema Mwenyekiti wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania na anaendelea: “Muuguzi huyo alipaswa kumuhudumia kwa kwa weledi na upendo mkubwa.”

Mwenyekiti katika ufafanuzi wake, kwamba mhusika ameadhibiwa kwa kuondolewa kwenye orodha ya wauguzi na wakunga nchini, kwa mujibu wa sheria zilizopo na ametakiwa kurejesha vyeti na leseni  za uuguzi kwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa anayetakiwa, kuziwasilisha kwa Baraza.

Nadhani hapo kuna mawili ninayotathmini, kwamba bado kuna upande mmoja ni kiashiria kuna ‘makandokando’ ndani ya huduma ya uuguzi yenye mafanikio makubwa sasa na upande wa pili, ni onyo kwa wenye tabia ukiona mwenzio ananyolewa, wewe tia maji’.