Wauzaji vyakula vituo vya daladala wazingatie afya za walaji

11Jul 2017
Jenifer Julius
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wauzaji vyakula vituo vya daladala wazingatie afya za walaji

UKIPITA kwenye maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam hasa nyakati za asubuhi, utawaona kinamama na kinababa wanauza vyakula vya aina mbalimbali kwa ajili ya kifungua kinywa au vyovyote vile.

Miongoni mwa vyakula nyakati za asubuhi mara nyingi ni vitafunwa kama vile maandazi, mihogo ya kuchemsha, sambusa, bagia, magimbi na mengineo ambavyo huuziwa wapita njia, wafanyabiashara na abiria wanaoshuka kwenye magari na kujikuta katika harakati za kupata kifungua kinywa ili kuikabili siku mpya ikiwa bado mapema.

Ukiacha vitafunwa hivyo pia kuna vyakula vya aina nyingine kama vile samaki wa kukaanga, uji wa ulezi, juisi na vinginevyo.

Uzoefu unaonyesha kuwa, mara nyingi nyakati za mchana huuzwa vyakula kama vile wali, ugali, pilau na mboga za aina mbalimbali ambazo hupakuliwa na kuuzwa kwa wateja vikiwa vimehifadhiwa kwenye ndoo na vyombo vinginevyo.

Wazo la kuuza vyakula ni zuri kwa sababu huwasaidia wale wenye kipato kidogo au wenye haraka zao kupata chakula, hasa kwenye maeneo ya katikati ya mji kama vile Posta ambako vyakula huuzwa kwa bei ya juu kwenye migahawa.

Pamoja na hayo yote kwa namna ambavyo vyakula hivi vinavyohifadhiwa kwenye vyombo vinavyouzwa, kwa namna yoyote ile inatisha na kukatisha tamaa.

Tunafahamu kwamba linapokuja suala la usalama wa afya ya mtu, kwa namna yoyote ile kunatakiwa kuwe na uangalizi na utayarishaji wa hali ya juu wa vyakula ili kuhakikisha kuwa afya inalindwa.

Ukweli uko bayana kwamba, kitu chochote kinachoingia katika kinywa cha binadamu kinatakiwa kuandaliwa vizuri kwa kuzingatia kiwango cha juu sana cha usafi.

Hii ni pamoja na kupikwa kwenye mazingira safi, kuhifadhiwa sehemu safi na hata kinapopelekwa kuuzwa kwa namna yoyote ile inatakiwa kuwekwa katika sehemu safi.

Ninaamini kuwa, vyakula vinavyouzwa kwenye vituo vya mabasi ikiwamo kituo cha Mnazi mmoja, Baridi, Posta mpya na Feri vimepikwa na kuandaliwa katika mazingira safi ambayo hayawezi kuleta madhara kwa mlaji.

Lakini vyakula hivyo vinapofikia kwa ajili ya kuuzwa ndipo panatia shaka. Maana yangu hapa ni kwamba, usafi wa kutosha hauzingatiwi vyakula hivi vinavyohifadhiwa ili walaji wavione na kuvinunua wakiwa wamejiridhisha kuwa mambo ni safi.

Kwa wale waliobahatika kupitia maeneo hayo na kuona jinsi vyakula hivyo vinavyohifadhiwa watakubaliana na mimi kwamba si sehemu salama kwa afya ya mlaji hasa mlaji makini anayejali afya yake.

Ukweli ni kwamba, vimewekwa wazi kiasi cha kuvutia wadudu waenezao magonjwa ya kuambukiza, kama vile inzi, wanaorandaranda na kutua katika vyakula hivyo kwa uhuru mkubwa wa kutafuta kile wanachokitafuta, hali ambayo ni tishio kwa usalama wa mwili wa mlaji.

Licha ya kung’ong’wa na inzi pia hupulizwa na vumbi linalotibuliwa na wapita njia pamoja na magari yanayopita pembeni ya vyakula hivyo.
Kwa namna yoyote ile, hali hiyo inasababisha maradhi kama vile kipindupindu kwa mlaji kutokana na kula uchafu unaotokana na vijidudu vinavyopatikana katika vumbi hilo.

Moshi unaotokana na magari yanayosimama karibu na vyakula hivyo, ukienea kwenye vyakula hivyo, pia husababisha maradhi kama vile ya kukohoa mlaji anapopitisha kwenye kinywa chake.

Ukiacha vumbi na moshi pia kuna takataka nyingi zinazoweza kuingia kwenye chakula hicho ikiwamo, zinazotoka juu ya miti, vijidudu vinavyotoka kwenye kinywa cha muuzaji anapokohoa, kinyesi cha ndege na wadudu walio juu ya miti ambao wauzaji hao wamekaa na mengine mengi.

Kuna haja ya kuzingatia usafi katika vyakula ili kujikinga na maradhi ya kuharisha na kutapika hasa janga la ugonjwa wa kipindupindu unaolikumba jiji la Dar es Salaam mara kwa mara.

Tunafahamu kwamba, ugonjwa huu ukizuka huua na kuwaacha wengine kadhaa wakiwa hoi hospitalini wakipatiwa matibabu na kupigania maisha yao.

Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni, Aziz Msuya aliwahi kuthibitisha kuwa watu watatu kufa kwa ugonjwa wa kipindupindu katika wilaya yake. Pamoja na idadi ya wagonjwa kuongezeka kutoka 34 hadi kufikia 43.

Kutokana na utafiti sababu zinazochangia hali hiyo ni kutozingatia usafi wa mazingira, vyakula visivyoandaliwa katika hali ya usafi, maji, pamoja na kinga dhidi ya ugonjwa hatari wa kipindupindu husababisha kurejea mara kwa mara katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania.

Shime kwa wanaouza vyakula hivyo barabarani na sehemu nyingine za wazi kuzingatia usafi kwa kufunika vyakula vyao, ili kuvikinga na vijidudu vinavyoleta maradhi kwa walaji. Badala ya kuviweka kwenye masinia na kuviacha wazi ni vyema waviweke kwenye vyombo vyenye mifuniko.

Kwa kufanya hivyo, kutaviweka vyakula kwenye hali ya usalama hata kuwavutia walaji wengi ambao hawanunua vyakula hivyo kutokana na mazingira yake kutowaridhisha.

Pia wale wanaouza vyakula kama wali nyakati za mchana ni vyema wakahifadhi vyakula hivyo kwenye vyombo visivyopoza ili kumfikia mlaji kikiwa cha moto.

Kwa upande wa walaji nao wawe mstari wa mbele katika kujali afya zao. Wasikubali kununua vyakula ambavyo havijahifadhiwa sehemu salama ili kulinda afya zao. Pia kama itamlazimu kununua basi hana budi kukupasha pale inapobidi ili kula kikiwa cha moto au kunywa na chai ya moto.

Tukumbuke kuwa, hakuna mtu aliyeajiriwa kukinga afya zetu dhidi ya maradhi ya kuambukiza yanayoepukika ni jukumu kumu letu wenyewe hivyo hatuna budi kupaza sauti zetu tunapoona muuzaji anahatarisha usalama wa afya zetu.

Kama umemweleza haelewi nenda kanunue sehemu nyingine kwa mtu ambaye biashara yake inajali afya ya walaji.

Kinga ni bora zaidi kuliko tiba hivyo sote tuwajibike kukinga afya zetu na za vizazi vyetu.