Wavamizi maeneo ya wazi walivyoisoma namba

16Jul 2017
Sabato Kasika
Nipashe Jumapili
Muungwana Lazima Nilonge
Wavamizi maeneo ya wazi walivyoisoma namba

WAKATI mwingine unajiuliza kwanini viongozi wanaosimamia matumizi bora ya ardhi walishindwa kuzuia kasi ya watu kujenga makazi na vitega uchumi kiholela ndani ya mitaa iliyopimwa au maeneo ya wazi?

Ukichunguza zaidi unajihoji hivi ni kweli serikali haikuwa na uwezo wa kusimamia na kukomesha hali hii, ambayo madhara yake ni mengi ikiwamo kuzuia magari ya zimamoto kufika baadhi ya mitaa, kutoa wagonjwa nyumbani na kukabiliana na madhara mengine yanayohitaji huduma za dharura?

Unapojiuliza maswali haya yote, unapata majibu yasiyopendeza yakiwamo uzembe wa baadhi ya watendaji wa serikali za mitaa, manispaa au hata wizarani kwa wanadaiwa walivutiwa na rushwa kuliko kutenda haki.

Rushwa hizi ndizo, ambazo huumiza watu wa kawaida na ukifika jijini Dar es Salaam na kutembelea maeneo machache yaliyopimwa, utashangaa kuona mitaa kadhaa imezibwa baada ya watu kujenga nyumba mpya za kuishi au za biashara.

Yapo baadhi ya maeneo yaliyowahi kukumbwa na hali hiyo yakiwamo Magomeni, Kinondoni, Mwananyamala, Mwenge, Ubungo, Ilala, Buguruni na Sinza.

Ukweli ni kwamba kasi ya uvamizi wa mitaa na maeneo ya wazi jijini ilikuwa ni kubwa, ikisababisha wasiwasi miongoni mwa wakazi hasa wale wanaothamini na kuheshimu utaratibu na utawala wa sheria.

Watu walikuwa wakishangaa kwa nini mambo haya yatokee wakati mfumo wa serikali unaanzia ngazi za mitaa, ambako ndiko 'madudu' hayo yalikuwa yakifanyika!

Lakini kwa sasa kasi ya ujenzi holela imeanza kupungua kwenye utawala huu wa awamu ya tano na kuwafanya wakazi wa jijini kuanza kupumua na ni vyema hali hii iendelee ili kurudisha heshima ya serikali.

Ilikuwa inashangaza zaidi kuona mtaa una njia za kupita ili kuunganisha na mwingine, lakini muda mfupi unaamka unakuta mtu ameziba kwa kujenga nyumba ya kuishi au biashara na hakuna hatua zinazochukuliwa.

Kwenye baadhi ya maeneo mambo kama hayo yalikuwa yakifanywa jirani na makazi au ofisi za serikali za mitaa, lakini bila wenye mamlaka kuchukua hatua dhidi ya wanaofanikisha uvamizi huo hivyo kuibua na kuendeleza manung'uniko kutoka kwa wananchi.

Hali hiyo pia ndiyo iliyosababisha baadhi ya watu kukosa imani na serikali na kufikia hali hiyo mengi yalitarajiwa ikiwamo watu wa kawaida kuipuuza.

Hapo ndipo watu walipojiuliza kuwa hivi ni nani miongoni mwa viongozi wa serikali mwenye mamlaka ya kuzuia vitendo kama hivyo visiendelee kufanywa, kwa vile kila mmoja alikuwa kimya?

Hali kama hii ingeachwa iendelee, madhara yake yangekuwa makubwa ikiwamo kuzuia uwezekano wa serikali kutumia maeneo ya wazi kwa shughuli za kijamii kama kujenga shule, vituo vya polisi au zahanati inapohitaji.

Kuzuia matumizi mabaya ya ardhi kunaweza kuokoa hasira au jazba za baadhi ya wananchi wenye tabia ya kutokuwa na subira na kujichukulia sheria mkononi jambo, ambalo ni hatari zaidi kwa amani ya nchi.

Sina mashaka na serikali ya awamu ya tano kwa jinsi inavyofanya kazi zake kwani hata wale waliokuwa na jeuri na kujenga nyumba zao kwenye maeneo ya wazi ni kama wamenywea kabla ya kuchukuliwa hatua.

Hivyo ni vyema hata wakazi wa jijini kuwataja wale ambao wamejenga kwenye maeneo ya wazi hata kama watakuwa wameruhusiwa na serikali za mitaa.

Ifike wakati watu wa aina hiyo wawe wastaarabu na waache uroho wa ardhi kwa kuacha mitaa na maeneo ya wazi yatumiwe na jamii kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwamo michezo.

Wakati mwingine unaweza kusema kuwa uvamizi wa maeneo ya wazi hufanyika katika sehemu zisizopimwa, lakini uvamizi huo ni vigumu kuonekana kwa haraka kwa sababu ya mazingira.