Waweza kukiri tuhuma polisi ukazikata kortini

12Oct 2019
John Juma
Nipashe
Mionzi ya Sheria
Waweza kukiri tuhuma polisi ukazikata kortini

WENGI wetu tunajikuta tuko mbele ya polisi, watu wenye hasira kali au polisi jamii, kama mtuhumiwa umefikia hatua hiyo unaweza kukiri makosa katika kituo cha polisi au viongozi wa serikali za mitaa. Lakini kosa hilo ukalikataa unapopandishwa kizimbani kujibu mashtaka. Unaweza na yanatokea.

Mtuhumiwa anaweza kukubali au kukiri kosa fulani katika ngazi ya awali iwe kituo cha polisi au serikali ya mtaa ama polisi jamii ambako uvunjifu wa sheria umefanyika, lakini baadaye kukana mashtaka akiwa kizimbani.

Mshitakiwa licha ya kukiri makosa yake mara baada ya kufikishwa mahakamani anakataa kuhusika na uhalifu unaotajwa.

Ni kawaida sana tena mara nyingi mahakama zinashuhudia mshtakiwa mara baada ya kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi au hata wananchi wenye hasira kali hujikuta analazimika au analazimishwa kukiri kosa.

Anafanya hivyo kwa kutegemea huruma au ahuweni fulani, hata kama hakufanya kosa analoshutumiwa nalo. Zaidi sana, lengo ni kunusuru maisha yake kwa wakati huo.

Na kama haitoshi, wengine hufikia kukiri makosa hata kama hawajafanya kosa mara baada ya kuwa wameshapigwa sana wakati wa mahojiano katika mahabusu za polisi.

Hivyo basi, ni katika mazingira kama haya; mhusika hata awe jasiri kiasi gani anaweza kujikuta anakiri kosa ambalo kwa hakika hakukifanya na kupelekea kukataa kufanya hivyo mahakamani.

ANGALIZO

Ieleweke kuwa siyo jambo au atua nzuri sana mhusika kukiri kweli ametenda kosa, ili hali hajafanya hivyo itokee tu katika mazingira magumu, bila ya namna nyingine kuepuka mateso au mauti ikiwezekana.

Hii Kimsingi, wakati mwingine unaweza ukawepo ugumu wa kujinasua huko mbeleni, ukifikishwa mahakamani.

Mfano, katika kesi ya jinai namba 6/2017 kati ya Jamhuri dhidi ya Muhangwa Simon Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba chini ya Jaji I.C. Mugeta. iliyotolewa maamuzi hivi karibuni Septemba 25, 2019. Haya yalijiri.

Mshtakiwa alikiri kufanya mauaji hayo akiwa mbele ya polisi huko Biharamulo, na tena mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo huko Biharamulo. Ila mara baada ya kufikishwa mbele ya Hakimu wa Mahakama Kuu mjini Bukoba kwa ajili ya kusikilizwa kesi yake, akakamatwa akakataa .

Kabla ya kwenda mbali katika mazingira kama haya mahakama mara zote katika kuhakikisha haki inatendeka hujielekeza zaidi katika misingi mikuu mitatu ambayo hutakiwa kuthibitishwa na upande wa mashitaka ili kuonyesha kuwa mtuhumiwa ameamua kubadilika lakini alikiri.

Aidha, ieleweke kuwa upande wa mashitaka ndiyo wenye wajibu wa kuitosheleza mahakama kupitia misingi hii kuwa mtuhumiwa alikiri japo sasa anakataa kuwa hakukiri.

Kwa misingi hii ikiwa itatokea ukalazimika kukiri na baadaye kukataa, uweze kujua wanaokushitaki wanatakiwa kuthibitisha nini, au wewe uwahoji uwaulize nini na katika minajili ipi?. Ambapo basi misingi yenyewe ni kama hivi , mosi wanaokushitaki wawe na ushahidi mwingine unaojitegemea unaoonyesha kuwa kweli umetenda kosa (collaboration).

Wasitegemee ushahidi huu wa kukiri pekee kwasababu huo tayari umeshaukataa. Watafute ushahidi mwingine wa kuusaidia huu kuonyesha kuwa hata kama umekataa kuwa ulikiri bado kuna hili na lile linakuingiza kwenye kutenda kosa.

Ni wajibu wako kuwahoji kuhusu uwepo wa ushahidi mwingine tofauti na huu wa kukiri. Wakikosa basi kukiri kwako kunakosa nguvu na hivyo kuleta uwezekano wa kuachiwa huru.

Pili, wanaokushitaki wathibitishe kuwa ulikiri bila kulazimishwa. Hii ni kwasababu kukiri kwa kulazimisha au kushawishiwa ni sawa na kuwa hujakiri au hukukiri. Wathibitishe kuwa hakukuwa na kulazimishwa. Hapa pia na wewe unayo kazi ya kufanya.

Kazi yenyewe ni kujitahidi kuonyesha mazingira ya kulazimishwa kukiri mfano alama za kipigo na mateso mwilini mwako, au mazingira ya hatari kama kuzingirwa na wananchi wenye hasira, au kundi na mazingira mengine yanayofanana na hayo.

Ukifanikiwa katika hili basi umefanikiwa kufuta kukiri kwako na umekaribia kuachiwa huru.

Tatu, wanaokushitaki wathibitishe kuwa ulichokiri ulikuwa ukimaanisha hicho na si vinginevyo. Kwa maana kuwa kukiri kwako hakukulenga kitu kingine chochote bali lile kosa uliloshitakiwa nalo. Hii ni kwasababu waweza kuwa ulikiri lakini hukuwa umeelewa kile unachokiri.

Ni kazi yao wanaokushitaki kuthibitisha kuwa ulichokiri ulilenga kosa husika, lakini pia ni wajibu wako kama ulikiri bila kuelewa kuonyesha kuwa hukuwa umeelewa unakiri nini au mazingira hayakuwa rafiki kukupa nafasi ya kuelewa ulichokuwa unakiri.

Kwa ujumla wakishindwa kuthibitisha lolote katika haya matatu niliyoeleza basi ni shaka la msingi katika ushahidi wao hata kama ulikuwa umekiri yafaa mahakama ikubaliane na wewe kuwa hukukiri na uachiliwe huru.

Mwisho, kukiri kunakozungumziwa na makala hii kunajumuisha maelezo unayoandika polisi (cautioned statement) na yale yote unayoandika au kusaini popote nje ya mahakama kabla kesi yako kuanza (extra judicial statement).Hivi ndivyo sheria inavyotaka.