Wazazi na walezi kazi ya kujenga madarasa ni yenu

10Dec 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wazazi na walezi kazi ya kujenga madarasa ni yenu

MATOKEO ya mtihani wa darasa la saba mwaka 2019, yameshatangazwa, huku wanafunzi 701,038, ambao ni sawa na asilimia 92.27, wakiwa wamefaulu kuanza kidato cha kwanza mwaka 2020.

Katika ufaulu huo, kuna mikoa 13 ya Geita, Morogoro, Dodoma, Njombe, Katavi, Singida, Ruvuma, Tabora, Kilimanjaro, Kagera, Mwanza, Shinyanga na Mtwara ambayo wanafunzi wake wote wamefaulu kwenda sekondari.

Pamoja na ufaulu huo, kuna tatizo kidogo ambalo ni muhimu kulijadili na ikiwezekana lipatiwe ufumbuzi wa kudumu, badala ya kujirudia kila mwaka kana kwamba hakuna uwezekano wa kulimaliza.

Ninasema hivyo, kwa sababu wanafunzi 701,038, waliofaulu, wenzao 58,699 wamekosa nafasi, kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa, na serikali imeagiza ujenzi wa vyumba hivyo ufanywe haraka, ili waanze masomo.

Hii ni kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, ambaye alikaririwa na vyombo vya habari akisema hayo hivi karibuni.

Lakini, pamoja na hayo, ipo haja wazazi kumaliza tatizo la uhaba wa madarasa kwenye shule za umma, bila kusubiri wakati wote mkono wa serikali, kutokana na ukweli kwamba shule hizo ni zao.

Ushiriki wao uende mbali hadi kwenye uboreshaji wa miundombinu ya shule, ili kupunguza tatizo hilo ambalo linajitokeza kila mwaka.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari mwaka jana, Jafo alisema wanafunzi 133,747, sawa na asilimia 18.24 ya waliofaulu mtihani darasa la saba mwaka huo walichelewa kuanza kidato cha kwanza kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa.

Sasa tatizo kama hilo limejirudia tena katika taarifa yake ya mwaka huu, hali ambayo inaonyesha kuwa kuna haja ya kuhimiza umma wa Watanzania kuona umuhimu wa kushiriki kwenye maendeleo ya shule za umma.

Ushirikiano wa wazazi usiishie kufuatilia kwa karibu maendeleo ya watoto wao shuleni bali washiriki katika kuboresha miundombinu ya shule ikiwamo ujenzi wa vyumba vya madarasa, ili kumaliza kero hiyo.

Bodi za shule ziweke mikakati ya kusaidia kumaliza tatizo hilo, kwa kushirikisha wazazi kwa kutambua kuwa shule ni mali ya wazazi hawana budi kuzihudumia kwa hali na mali badala ya kuichia serikali tu.

Inawezekana kuwa wapo baadhi ya wazazi ambao hawataki kushiriki katika shughuli za maendeleo ya shule wakiamini kwamba kwa sasa jukumu lote ni la serikali, kwa vile imetangaza kugharamia elimu.

Mawazo ya aina hiyo hayaendelezi taifa kwa yeyote anayejua umuhimu wa elimu, hivyo wasiotambua hilo wasaidiwe ili wabadilike na hatimaye wachangie maendeleo ya shule hizo, ambazo ni mali yao.

Uzoefu unaonyesha kuwa hata zilipoanzishwa kambi za kitaaluma, baadhi ya wazazi waligoma kushiriki kutoa vyakula kwa ajili ya watoto wao, wakidai kwamba serikali imetangaza kutoa elimu bure.

Wazazi wa aina hiyo ndiyo hao, ambao hawaoni na wala hawatambui kuwa shule za umma ni zao, wana wajibu wa kuzihudumia ili kuhakikisha wanapunguza matatizo yanayozikabili bila kusubiri serikali.

Kimsingi ni kwamba wazazi wanapaswa kutambua kuwa shule za umma zinawategemea wao pia, wasikwepe kuzihudumia kwa visingizio kuwa serikali imeshatangaza kutoa elimu bure.

Elimu bure haijazuia wazazi na walezi kuchangia maendeleo ya shule kama, ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakidhani na kukwepa majukumu yao kwa ajili ya maendeleo ya shule na watoto wao kwa ujumla.

Kwa ujumla maendeleo ya shule na wanafunzi vinategemea wadau wote wa elimu wakiwamo wazazi na walezi, kwani wana wajibu wa kushirikiana na serikali kuhakikisha wanamaliza.

Julai mwaka huu Naibu Waziri Tamisemi anayeshughulikia elimu, Mwita Waitara, alisema serikali haijakataza michango shuleni, isipokuwa ya kulazimisha.

Alikuwa akifungua bwalo la chakula lililojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (CDTF), katika Shule ya Msingi Mlimwa, jijini Dodoma.

Alisema wapo watu wanapita mitaani na kutoa tafsiri potofu kuwa serikali imepiga marufuku michango yote shuleni jambo ambalo si kweli.

Kwa maelezo hayo ni wazi kwamba wazazi na walezi wanahusika kikamilifu kuzisaidia shule kupitia kamati na bodi za shule, kwa ajili ya kumaliza changamoto zinazozikabili ikiwamo uhaba wa madarasa.