Wazazi, walezi anzeni kubeba gharama hizi

26May 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wazazi, walezi anzeni kubeba gharama hizi

JUMATATU ijayo Juni mosi wanafunzi wa kidato cha sita na wa vyuo vikuu wanatarajia kuanza masomo baada ya serikali kujiridhisha kuwa maambukizo ya virusi vya corona yanapungua.

Kutokana na hali hiyo kuendelea vizuri, imeamua kuruhusu wanafunzi wa kidato cha sita na vyuo vikuu kuanza masomo huku wa shule za msingi hadi kidato cha tano wakitakiwa kusubiri kwanza.

Hatua hiyo ya serikali kutangaza kufungua vyuo, mamlaka zinazohusika na masuala ya taaluma zitawajibika kuandaa mpango ili kuwawezesha wanafunzi kufidia muda wa masomo walioukosa.

Pamoja na hatua hizo za kufungua vyuo, bado wazazi wana wajibu wa kuhakikisha watoto wao wanaendelea kuwa salama, wawapo kwenye masomo, wakati huu ambao maambukizo ya corona yanaendelea kupungua.

Tayari, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) anayeshughulikia elimu, Mwita Waitara ameshaagiza viongozi wa mikoa, wilaya na uongozi wa shule za kidato cha sita kuchukua tahadhari zote za afya ikiwamo wanafunzi wa bweni kulala kwa umbali ili kujiepusha na maambukizo ya ugonjwa wa corona na kukagua mazingira ili yasiwe sababu ya maradhi.

Tahadhari nyingine ambayo inasisitizwa ni kuhakikisha wanafunzi wote na walimu wao wanavaa barakoa na kunawa mikono kwa maji tiririka kwenye maeneo yote ya kuingilia shuleni na madarasani.

Katika hilo, anaeleza kuwa kuna uwezekano wazazi wakaingia gharama kidogo, kwa vile wanatakiwa kuwanunulia watoto wao barakoa na pia vitakasa mikono ili kujikinga na ugonjwa huo.

Kwa upande wa walimu, wanatakiwa kuwaandaa wanafunzi kisaikolojia ili wafanye vizuri kwenye mitihani yao ingawa pia wanafunzi wanaweza kwenda na tangawizi ili kujifukiza, lakini ni lazima wapimwe joto.

Maelekezo hayo yanagusa pande zote, hivyo ni muhimu zihusika kwa ajili ya usalama wa wanafunzi, wanaotarajiwa kuanza masomo mwezi ujao ili waweze kusoma bila changamoto ya maambukizo ya corona.

Wazazi wasiwe wazito katika kuchangaia usalama wa afya za watoto wao kwa kukwepa gharama za kuwanunulia barakoa na vitakasa mikono wakitegemea kwamba watafanyiwa kila kitu.

Serikali imeshaweka wazi kwamba katika hilo, kuna uwezekano wazazi kuingia gharama kidogo, hivyo walipokee hilo na kuanza kulifanyia kazi, kwani uhai una gharama kubwa kuliko fedha.

Jambo jingine la msingi ni wanafunzi wenyewe kutambua na kuzingatia kwamba ugonjwa huo upo, hivyo suala la kuchukua tahadhari ni la msingi kwa ajili ya usalama wa afya zao.

Kwa kawaida penye wengi huwa kuna mengi na pia kuna walimu wengi wakiwamo wa kupotosha, ambao wanaweza kusababisha baadhi ya wanafunzi wakaacha kuzingatia maelekezo wakidhani wako salama.

Yawezekana ukafika wakati wakaacha kuvaa barakoa au kunawa kwa maji tiririka na pia kupata vitakasa mikono kwa kufuata elimu za vijiweni hali ambayo inaweza kusababisha wakajikuta katika matatizo.

Hivyo suala la umakini ni la muhimu kwenye vita dhidi ya corona, kwani ndiyo umekuwa msisitiza serikali, kwamba corona imeanza kupungua, lakini ni vyema Watanzania kuchukua tahadhari.

Ni vyema kuzingatia kwa sababu imekuwa ni kawaida kwa baadhi ya watu mitaani kupingana na maelekezo ya wataalamu wa afya kuhusu kujikinga na ugonjwa huo na kwamba wao ndiyo wanajua zaidi.

Hayo yanaweza kuingia hata shuleni na kusababisha wanafunzi wasiwe makini wakidhani si lazima kunawa kwa vitasaka mikono au kunawa kwa maji tiririka na kumbe wanapotoshwa.

Lakini, kikubwa zaidi ni kwamba wazazi wafanye sehemu yao kwa kuingia gharama ya kuwanunulia watoto wao barakoa na vitakasa mikono ili wakavitumie mara shule zitakapofunguliwa.

Suala la kuingia gharama kidogo kwa ajili ya usalama wa afya za watoto halikwepeki, cha msingi ni kuliwekea mikakati ili kulifanikisha kwani zinahitajika barakoa za kutosha na vitakasa mikono vingi.