Wazazi, walezi ufumbuzi taulo za kike usisahaulike

14Jul 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wazazi, walezi ufumbuzi taulo za kike usisahaulike

UKOSEFU wa taulo za kike kwa baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini ni tatizo, ambalo linabuniwa kampeni mbalimbali kwa lengo la kulimaliza ili waweze kuhudhuria masomo bila kikwazo.

Miongoni mwa kampeni hizo ni ile ya 'mpe mabawa' ambayo imewahi kubuniwa na wadau wa maendeleo ya elimu kwa mtoto wa kike, ili asikae nyumbani kwa sababu ya hedhi.

Kampeni hizi ni wazi kwamba zinaweza kumweka mtoto wa kike katika mazingira salama yatakayofanya asome kwa kuhudhuria vipindi vyote awapo shuleni bila kikwazo.

Suala la uwazi ndilo lililopewa uzito kwenye kampeni hiyo kwa ajili ya kuondoa ukimya ili kuliongelea bila kificho, kuboresha mazingira ya shule kwa kuhakikisha upatikanaji wa vyoo ya kutosha, maji ya uhakika, taulo na sehemu za kujihifadhi na kujisitiri.

Kwa hali kama hii kama itazingatiwa, ni wazi wanafunzi wote wa kike wanaweza kuondokana na tatizo la kutohudhuria vipindi na kulazimika kukaa nyumbani.

Pamoja na hayo, ni jukumu la wazazi na walezi sasa kuwafundisha watoto wa kike kuhusu hali hiyo ili wanapokutana nayo wawe wazi kuwaeleza na kutafuta mbinu za kuwasaidia kuliko kukaa kimya. Kuna haja kwa wazazi na walezi kuweka mazingira ya kuwawezesha watoto wao kujitambua wanapofikia hatua hiyo.

Ninasema hivyo kwa sababu, uhaba na ukosefu wa taulo za kike umekuwa ukitajwa kukwamisha baadhi ya wanafunzi kuhudhuria vipindi shuleni. Hali kama hiyo ni hatari kwa maendeleo ya elimu ya mtoto wa kike, hivyo kuna haja wadau wote wa elimu kuanzia kwa wazazi na walezi, kushiriki kikamilifu katika kumaliza tatizo hili.

Bila kufanya hivyo, watoto wa kike wanaweza kuendelea kubaki nyuma kielimu, kwa sababu ambazo wakati mwingine ziko ndani ya uwezo wa wazazi, walezi na jamii.

Kimsingi ni kwamba kampeni za kuhamasisha uchangiaji wa taulo za kike hufanyika mara kwa mara, lakini tatizo bado lipo, umefika wakati sasa wa kupatia tatizo hilo ufumbuzi wa kudumu.

Ufumbuzi huo unategemea wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kutambua kwamba ukosefu wa taulo za kike ni tatizo kwa wanafunzi kwa kusababisha wakose vipindi kila mwezi.

Hivyo kila mmoja aangalie uwezekano wa kumsaidia mtoto wake na kama hana uwezo wa kifedha, basi awe wazi ili zifanyike njia za kumwezesha kupata taulo hizo kwa ajili ya mabinti zake. Wazazi na walezi watimize wajibu wao wa kuhakikisha watoto wao wanasoma, ikiwamo ni pamoja na kuhakikisha wanapata taulo za kike za kuwawezesha kujihifadhi.

Iwapo kila mmoja atatimiza wajibu, mtoto wa kike atapunguziwa matatizo ambayo yamekuwa yakimkabili yakiwamo ya kukeketwa, kuolewa na kusababisha akatishe masomo.

Ufike wakati kila mmoja aseme sasa inatosha mtoto wa kike kukosa vipindi anapokuwa kwenye hedhi au kukatishwa masomo kwa sababu ya kukeketwa ama kuozwa, kwani wote wana haki ya kupata elimu kama walivyo wa kiume.

Watoto wote wana haki ya kupata elimu bila ubaguzi, hivyo jitihada ziendelee kufanyika ili kuwaonda watoto wa kike kwenye tatizo la kukosa baadhi ya vipindi shuleni, kwa sababu ya hedhi.

Kwa wazazi wenye hali nzuri kiuchumi, wanaweza kuamua kununua taulo za kike kila mwisho wa mwezi na kuzipeleka, katika shule kwa ajili ya kuwasaidia mabinti ambao hawana uwezo wa kifedha.

Aidha, jamii itambue umuhimu wa kutoa fursa sawa kati ya mtoto wa kike na wa kiume, kupewa mafunzo ya stadi za maisha, kumtimizia mahitaji yote ya msingi kwa kuondoa unyanyapaa.