Wazo la kuwapo ‘vyumba vya usiri’ Mabwepande iwe kitaifa

13Jan 2022
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wazo la kuwapo ‘vyumba vya usiri’ Mabwepande iwe kitaifa

TAYARI nchi na zama ilikofika ni haki ya kumtetea mwanamke kuanzia ngazi ya chini aliko, hadi juu katika hatua zingine za umri.

Ni utetezi unaobeba tafsiri pana zaidi, kupitia sura tofauti za madhila ya yanayompata. Huko katika umri wa chini penye hadhi ya usichana, kuna ushuhuda wa mengi sana, maana kuna upungufu wa pili katika umri, mtu hawezi kujimudu vilivyo.

Hiyo ndio moja ya sababu hata shuleni, kunawekewa mkazo huduma muhimu kufikishwa mahali hapo.

Moja ya hatua inayoendelea na kampeni maalum katika sehemu tofauti, ni kuwapo vyumba vya usiri katika shule za msingi na sekondari kusaidia kuwalinda watoto wa kike, dhidi ya namna yoyote ya ukatili dhidi yao.

Inaelezwa, kunapokuwapo vyumba vya usiri kunakozaa tafsiri ya kusaidia kuwatetea watoto wasifanyiwe matendo ya ukatili na hasa wasichana.

Hivi karibuni katika kinachoitwa Bunge la Jamii lililoandaliwa na Kituo cha Taarifa na Maarifa cha Mabwepande, nje kidogo ya Dar es Salaam, baadhi ya wanajamii waliomba kuwapo vyumba hivyo vya usiri katika shule za msingi na sekondari, lengo ni kulinda mabinti wawe mbali na matukio ya ukatili.

Inafurahisha kumsikia Ofisa Ustawi wa Jamii wa Kata ya Mabwepande, Michael Mihayo, anasema kuwapo vyumba hivyo vya usiri kuwasaidia watoto wakike kusema mambo mabaya wanayofanyiwa na wanaume.

Katika kupambana na matukio hayo ya ukatili ambayo baadhi wananyooshewa vidole mahali hapo, ni vijana wa kiume waendesha bodaboda, sasa kukiombwa shule ziwasaidie mabinti kukabiliana na namna yoyote ya ukatili kwao.

"Kuwapo na vyumba vya usiri sio tatizo, tatizo ni kutokuwa na usiri wa watu," anatamka Mihayio, akisisitiza kuwapo maofisa ustawi wa jamii wa kila shule, wanaopaswa kuwa bega kwa bega kuwasaidia wasichana pale wanapofanyiwa ukatili.

Mtafiti wa Masuala ya Elimu wilayani Kinondoni, Dk. Bille Abrahamu, anasema kuwa changamoto iliyopo katika elimu na uzio katika shule zinatakiwa zitatuliwe kwa wakati na kutokuwapo vyumba vya usiri kunachangia hata msichana mwenyewe inapotokea anafanyiwa ukatili, anakosa pa kuwasilisha malalamiko yake.

Pia anaongeza kila shule itakapokuwa na ofisa wa ustawi wa jamii, ni namna itakayowasaidia kuwapo wanafunzi shuleni kupatiwa faragha ya kuwasilisha siri.

Ni jambo ambalo ukimtathmini Dk. Abrahamu, anasema katika utafiti wake amebaini shule zilizoko katika Kata ya Mabwepande, baadhi zina uzio huku na zingine hazina, akilaumu kutokuwapo uzio katika shule kunachangia tabia ya utoro kutoka kwa wanafunzi.

Pia malalamiko yake yanalenga katika Kata ya Mabwepande anakofanya utafiti kukiwa na maoni kwamba kwa jumla ya shule za msingi nne na sekondari shule moja, ambayo ndio pekee yenye uzio.

Anaongeza kuwa changamoto nyingine wanafunzi wanalazimika kutumia usafiri wa bodaboda na kulipa hadi shilingi 6,000 kwenda na kurudi.

Mtoa hoja huyo, ananena kinachotakiwa sasa ni kufanyike utaratibu wa kuwajengea hosteli mabinti wanafunzi, akiamini zitakuwa  mkombozi kwa wasichana hao.

Navutiwa na mtaalamu huyo akisema, serikali ya kijiji inapofanya mikutano ijaribu kuweka utaratibu wa mikutano itakayowasaidia watu kujua kinachoendelea katika kata hiyo. 

Mwajuma Juma, katika nafasi yake anaishukuru Asasi ya TGNP Mtandao kwa kuandaa bunge hilo la aina yake, hata kuibua mambo yaliyokuwa yamejificha.

Kuna changamoto nyingine anazozitaja ni uhaba wa maji ambayo hutumika muda mrefu kinadada kwenda kuchota. Pia bodaboda nao inapofika usiku wanapandisha bei maradufu.

Kilio kingine cha Mabwepande, kinaangukia katika kukosekana kituo cha afya kuwahudumia wakazi. Itapendeza yote hayo yakifanyiwa kazi.