Wenye jiji Dar Kivule - Kitunda, mnayofanyia watoto hayavumiliki

30Apr 2021
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wenye jiji Dar Kivule - Kitunda, mnayofanyia watoto hayavumiliki

MATUKIO ya ukatili tumekuwa tukiyasikia yanaendelea kutokea katika maeneo mbalimbali nchini na kuambiwa sababu za kufika huko.

Mazoea yaliyoko ni unasikia tendo la mtoto kabakwa na watu waliokutana naye njiani, au matukio ya mtoto kufanyiwa tohara bila ya ganzi, kapigwa, kakeketwa na ngariba au mwanamke kapigwa. Hayo yote yanaangukia katika jumla ya ukatili.

Hapo ndipo pananisogeza katika Kata ya Kivule, nikimkuta Ofisa Maendeleo wa Kata, anayekiri kuwapo utovu wa maadili na ndoa, akianika sababu moja ni ndoa kuvunjika kunachangia ukatili huo.

Hivi sasa kila anayefanyiwa mtoto na anapofika ofisini kwake, akihojiwa jibu linaangukia ukatili aliyofanyiwa mtoto na baba yake unatokana na mtoto kulala chumba kimoja na mzazi.

Anaeleza suala la ukatili pia unafanywa hata na baba wa kambo, pale mama anapokwenda kuishi na mtoto wake kwa mwanamume wa kufikia.

"Ukatili upo na tatizo ni ndoa kuvunjika. Mtu kuolewa na mwanamume mwingine na anapoenda kuishi na mume huyo, mtoto wake anafanyiwa ukatili,” anaweka wazi.

Pia, kuna la watoto kulala chumba kimoja na wazazi, nao wanapoona matendo yanayoendelea hapo, huenda kuyafanya na watoto wenzao.

Katika kada hizo, wapo ambao ni yatima na wanafanyiwa ukatili wanapokwenda kuishi katika mtazamo wa kufanyiwa hifadhi.

Anasema watoto wengi wanapofanyiwa ukatili, huwa hawasemi na wanapogundulika wanakuwa wameshaharibiwa sana kiafya.

Kinachompa tabu mtumishi huyo wa umma, ni pindi wahanga hao anapofanyiwa mabaya, hawatoi taarifa mapema, ili watuhumiwa wachukuliwe hatua stahiki.

Anasema, moja ya vinavyogundulika sababu ya kusuasua kutoa taarifa, ni wanaofanyiwa ukatili huwa hawasemi, kwa kuhofia kupigwa na hata inapofika hatua ya kugunduliwa, anakuwa wameshaharibiwa kiafya.

Mratibu wa Elimu wa Kata ya Kivule, Urumbi Kitilia, anasema mfarakano kati ya wazazi ni chanzo cha ukatili huo, huku sababu nyingine ni wazazi au walezi kutowapa watoto pesa za matumizi shuleni, hali inayochangia kuwapo mambo yanayohusiana na ukatili kiafya.

Urumbi anasema, inapofika hatua wanawahoji watoto wengi na wanakiri kulala na wageni kwao katika chumba kimoja na wanaofanya ukatili.

"Ukiwahoji watoto wanakwambia kalala chumba kimoja na mgeni na huyo ndio aliyemfanyia ukatili," anasema, akianisha elimu hiyo sasa inatolewa kwa upana.

Anasema watoto wanapofanyiwa ukatili huo nyumbani, nao wanaenda kuwafanyia ukatili watoto wenzao.

Konachofanyika kimsingi, ni elimu ya ukatili wanayoitoa kuwa sawa na bure, kutokana na ukatili kuendelea kufanyika lakini hawatoi taarifa kuwa wamefanyiwa ukatili.

Anaongeza kuwa watoto wanakaa mikao mibaya darasani na wakibanwa kufafanua kulikoni, wanasema.

Pia, kuna changamoto za wazazi kutoshiriki vikao vya shule kila wanapoitwa waelezwe maendeleo ya mtoto wake, msimamo ulio kinyume nao.

Jambo kuu la kuzingatiwa ni namna ya kusimamia malezi na tayari wamefanikiwa kuanzisha klabu katika baadhi ya shule, wakiwafundisha kinga dhidi ya ukatili, ikiwamo wanapofanyiwa ukatili huo wasioge, ili ushahidi kupatikana.

Mwalimu (jina tunalo) kutoka shule mojawapo iliyoko Kivule, Dar es Salaam, anasema mabaya yanayoonyeshwa katika baadhi ya televisheni ni sehemu ya magunu yanayokaribisha matukio kama ya ulawiti katika ukanda huo jijini.

Anasema, kuna watoto wanapotoka majumbani hawafiki shuleni, wanakojificha wanajikita katika machafu. Inatokea kwa shule za msingi na sekondari, ngome zao ni magofu na machimbo mabaya.

Huko njiani nako kuna wahuni wanaojitokeza na kuwapotosha kwa vishawishi kama pipi. Tayari kuna taarifa rasmi na mamlaka zinazohusika zimeshaandika barua sehemu husika, ziweze kuafuatilia kesi za wanafunzi wanaolawitiwa na kubakwa, ingawaje haijajibiwa.

Urumbi anasema wamenuia ufuatiliaji wa kesi hizo kufahamu hatima yake, kwani tayari kuna matukio ya kuyumbisha kesi katika namna, baadhi ya watoto wanahamishwa shule na kuiacha kesi pagumu.

Anashauri cha muhimu sasa, ni mamlaka za shule zinapobaini mtoto kafanyiwa mabaya, muhimu kwao ni kumuita mzazi kumhoji, kwani kunashuhudiwa wazazi wengi baada ya kutokea tatizo, wanawahamisha shule watoto.