Wenye malori Mkuranga ajirini madereva wenye uweledi kazini

17Jul 2020
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wenye malori Mkuranga ajirini madereva wenye uweledi kazini

AJALI za barabarani zinapotokea na kusababisha vifo au kuleta ulemavu wa aina yoyote kwa mwanadamu, kunafanyika tathmini kubwa kutoka chanzo hadi kufikwa ajali hiyo.

Tumekuwa tukisikia ajali nyingi zinapotokea, utaambiwa mwendo wa gari ulikuwa sio mzuri au utasikia dereva alikuwa akikimbiza gari na bahati mbaya akasababisha ajali.

Sababu nyingi zimekuwa zikitajwa kuchangia, lakini zipo zinazotokana na miundombinu duni katika kipindi cha mvua, hata kusababisha magari kuachia njia na kutumbukia katika mito.

Hadi sasa kumekuwapo taarifa zinazotolewa zenye madai kwamba, hata madereva nao kuna walikosa sifa na kuendesha magari hayo wakiishia kusababisha ajali.

Sote ni mashahidi wa Polisi wa Usalama Barabarani, kwa kushirikiana na wadau wengine, mbali na kuchukua hatua za kisheria na kinidhamu huko waliko, pia hawachoki kupaza sauti za elimu na tahadhari kuanzia kwa dereva na watumiaji huduma hizo.

Ni hadithi ambayo bado haijafifia, leo hii miaka imetimu miwili wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani, kuwapo mkasa wa gari la kubeba mchanga liligonga gari dogo la abiria aina ya Toyota Hiace na kusababisha ajali ya watu 14 wa familia na kati yao wapo waliokutwa na umauti.

Kutokana na tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Injiani Evarist Ndikilo, alizuia malori ya kubeba mchanga kusafirisha mzigo huo usiku.

Ni maagizo yaliyowataka wachimba mchanga na wasafirishaji wake, kuifanya kazi hiyo mwisho saa 12 jioni, muda wa kuanza saa12 asubuhi. Yaani wanatumika kwa saa 12.

Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Filberto Sanga, anasema utaratibu wa kuruhusu wenye magari ya mchanga kufanya kazi kwa saa 24 unaendelea kuandaliwa.

Sanga anasema, uongozi wa Mkoa wa Pwani unaendelea kuweka sawa utaratibu, ili kuwaruhusu tena wasafirishaji kufanya kazi yao kwa mzunguko wa siku nzima.

Anasema, pamoja na utaratibu kuandaliwa, anawataka wenye malori kuajiri waendeshaji walio na sifa na kuwapo madereva wawili watakaosaidiana muda wote.

Kiongozi huyo mkuu wa serikali katika wilaya hiyo, anasema polisi limejipanga kuhakikisha inatoa elimu sahihi kwa madereva wanaosafiri na magari hayo wawe na sifa kamili.

"Mlishuhudia ajali iliyotokea mwaka juzi na kuua watu 14 wa familia moja. Sababu ya ajali ilielezwa ni lori la mchanga kuigonga (Toyota) Hiace iliyokuwa imebeba familia hiyo," anasema.

Anaongeza kuwa tukio hilo la ajali lilitokea usiku, hivyo Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Injinia Ndikilo alilazimika kuzuia usafirishaji mchanga muda wa usiku.

Sanga anasema, ni muhimu wamiliki wa malori hayo wakahakikisha wanaajiri madereva walio na sifa zinazokubalika.

Mkuranga ni wilaya inayopitiwa na barabara kuu kati ya Dar es Salaam na mikoa ya Kusini, Lindi na Mtwara na kabla ya kujiunga na mkoa Lindi, Mkuranga inatenganishwa na Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani, wakati Dar es Salaam, inapakana nayo katika Wilaya ya Temeke.