Wenye wastani wa D wakisaidiwa wanaweza

23Feb 2021
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wenye wastani wa D wakisaidiwa wanaweza

MFUMO unaotumiwa na baadhi ya shule kujipatia umaarufu kwenye mitihani ili kuvutia wazazi na walezi wa kuchagua wanafunzi wenye alama za juu wanaohitimu elimu ya msingi, ni jambo lililozipa shule nyingi hasa za binafsi majina makubwa.

Kinachofanywa na shule hizo ni chema kwa kuwa kinazifanya kuwa na uhakika wa kupata wanafunzi bora, wanaozitangaza hivyo kushawishi wateja zaidi kupeleka watoto wao huko.

Huo ndiyo ubinifu wa miaka yote ambao unatumiwa na shule hizo, kwa kuwa ingawa zinatoa huduma lakini ziko kibiashara, hivyo ili kuvutia wateja, ni muhimu kuwa na vitu vya kuwashawishi.

Ushiwishi mojawapo ni huo wa kuwa na wanafunzi wenye ufaulu wa alama A na B huku wenye wastani wa D wakiachwa kwa kuwa hawana sifa za kuzitangaza vizuri shule.

Pamoja na hayo, mfumo huo unaotumiwa na shule binafsi ungekuwa ni fursa kwa wadau wa elimu katika shule za umma kuangalia uwezekano wa kuandaa mazingira ya kuwasaidia wanafunzi wenye wastani wa D.

Ni kweli kuna mikakati mbalimbali inayofanywa na serikali ikiwamo kusimamia shule zake ili kuleta mabadiliko kwenye sekta ya elimu, lakini ni vyema hili la kuwasaidia wenye wastani wa mdogo lipewe uzito.

Baadhi ya mambo yanayoweza kufanywa ni pamoja na kuwapo utaratibu wa kuwaanda upya wanafunzi wa aina hiyo ili hatimaye wawe wawe na uwezo mkubwa darasani kama wenzao.

Kila shule ya msingi au sekondari, inaweza kuwa na vipindi maalum vya kuwanoa upya wanafunzi wenye alama za wastani wa D wapande viwango na kufikia ule unaohitajika.

Siyo vibaya kununua vitabu vya kutosha kwa ajili ya wanafunzi, kila mmoja awe navyo vya masomo yote, kwa lengo la kuwaongezea uelewa ili wasiachwe nyuma na wenzao.

Lakini, pia suala la ukaguzi wa shule ni nyenzo muhimu, inaweza kutumika kuhakikisha utendaji shuleni unaboreshwa na mafanikio yake yanategemea ni jinsi gani ukaguzi unafanyika.

Matokeo ya ukaguzi yanatumiwa kama nyenzo ya kuchagiza maboresho ya utendaji wa shule, yanaweza kusaidia kuongeza ufaulu kwa wanafunzi na hata kuondoa kutengwa kwa wale wenye uwezo mdogo darasani.

Hivyo, utendaji wa shule na pia wa wanafunzi kwenye mitihani ukipewa kipaumbele katika ukaguzi, vyote kwa pamoja vinaweza kufanya wanafunzi wakapiga hatua kwenda mbele.

Wakati hayo yakifanyika, wizara husika nayo kwa upande wake inaweza kuanzisha utaratibu wa kufuatilia ufanisi wa program ya ukaguzi wa shule, kwa lengo la kuinua kiwanago cha elimu kwa kila mwanafunzi.

Kwa mazingira ya aina hiyo, inawezakana idadi ya wanafunzi wenye alama za wastani wa D ikapungua na ikiwezekana wasiwepo wanaotengwa kwa sababu tu ya uwezo wao mdogo wa darasani.

Wanafunzi wenye wastani mdogo wa ufaulu, nao wana haki ya kupata fursa ili wanapokwenda katika shule binafsi wachukuliwe, hivyo njia mojawapo ni shule za umma kuwaandalia mazingira ya kuwanoa zaidi.

Lakini pia shule za umma zikiboreshwa, zinaweza kupunguza tatizo hilo, kwani baadhi ya wazazi na walezi hupeleka watoto wao shule binafsi kwa kuwa wanaamini zinafundisha vizuri.

Ufaulu huo unatokana na uchaguzi unaofanywa na shule hizo kwa kuchukua  wale wenye alama za juu na kuacha wengine wenye wastani wa D, hii iwe ni fursa kwa shule za umma kuwanoa wanafunzi wake zaidi.

Miongoni mwa njia za kufikia mafanikio hayo ni shule za umma kujipanga upya na kuweka mikakati ya kuhakikisha wanafunzi wenye alama D wanapungua na hata ikiwezekana wasiwepo kabisa.

Vilevile mwanafunzi anatakiwa kutambua kuwa kusoma si sawa na kubeba mzigo mzito, bali ni kazi inayohusisha akili na viungo, hivyo anatakiwa kusaidiwa kutambua lengo lake anaposoma na si kusoma ili mradi tu.

Yapo mengi yanayoweza kumfanya mwanafunzi akawa na maendeleo mazuri darasani kwa kuhusisha wadau wa elimu, hivyo kila mmoja afanye sehemu yake kuongeza ufaulu.