Wiki ya maji ianze kutatua kero

19Mar 2017
Beatrice Bandawe
Nipashe Jumapili
Tuzungumze kidogo
Wiki ya maji ianze kutatua kero

WAKATI wiki ya maji ikizoeleka kuadhimishwa kwa sherehe mbalimbali na maonyesho ya kila huduma zinazohusiana na sekta hiyo, mwaka huu maadhimisho hayo hayatakuwa na shamrashamra kama ilivyozoeleka, badala yake zitafanyika shughuli za uwekaji wa mawe ya msingi na kutembelea vyanzo vya maji.

Uamuzi huo ulitangazwa na Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya wiki ya maji ambayo yatafikiwa kilele chake wiki hii, Jumatano Machi 22.

Miaka ya nyuma kulikuwapo na utaratibu wa wizara hiyo kuendesha shughuli za maadhimisho hayo kwa kufanya sherehe na maonyesho katika maeneo mbalimbali.

Kwa wananchi wengi sherehe hizo walikuwa wanaziona ni kupoteza fedha ambazo zingesaidia kupunguza kero mbalimbali za maji zinazowakabili wananchi.

Ni kweli fedha zilipotea katika kuandaa fulana, kofia, kulipana posho na kusafiri nje na ndani ya mikoa kushiriki sherehe na maonyesho lakini mabomba yakikauka na wananchi wakichafua na kukausha vyanzo vya maji.

Kwa mfano, zingeweza kuboresha miundombinu chakavu ambayo inasababisha maji mengi kupotea njiani kutokana na mabomba kuvuja.

Sherehe hizo zilikuwa zikitumia mamilioni ya fedha kwa ajili ya maandalizi ya wiki hiyo wakati maeneo mengi hasa ya vijijini yakikosa huduma ya maji safi na salama, hali inayosababisha wananchi wa maeneo hayo kupata madhara ya magonjwa ya matumbo na hata kipindupindu.

Ukitembea sehemu mbalimbali hata mijini, bado wananchi wanahangaika kutafuta maji na wengine kulazimika kutumia maji ya
visima yenye chumvi. Wapo wanaoshirikiana maji na wanyama wa porini na mifugo yao. Inatokea kwa sababu huduma hiyo inapatikana katika malambo au madimbwi.

Tatizo la maji limesababisha wanawake kupoteza maisha kwa vile wanaliwa na fisi porini, lakini pia kuna walioliwa na mamba na hata kujeruhiwa viboko mtoni au ziwani.

Wananchi wengine hutumia fedha nyingi kununua maji yanayotembezwa na mikokoteni bila kujua usalama wake.

Nyumba za wakazi wengi jijini Dar es Salaam na maeneo mengine ya nchi, zimejaa ndoo na madumu ya kuhifadhia maji kutokana na kero ya kutopatikana maji ya uhakika.

Baadhi ya watu wamekuwa wakipata faida kubwa kwa kuwauzia watu maji kwa kutumia mwanya wa mamlaka husika za kusambaza maji kwa wananchi, kushindwa kutimiza waji wake.

Katika maadhimisho ya mwaka huu, Waziri Lwenge, amesisitiza kuwa shughuli zitakazofanyika ni kuweka mawe ya msingi, kutembelea miradi mipya pamoja na kuangalia vyanzo vilivyokauka ambavyo awali vilikuwa vikitumika.

“Maadhimisho ya mwaka huu yatawalenga sana wananchi, kwani tutatembelea maeneo yao na kujionea vyanzo vya maji vilivyopo
na vile vilivyokauka ili kuwapa elimu ya kutunza vyanzo vya maji viwe endelevu.

Tunaenda na mwananchi kwenye chanzo kilichokauka na akitoka hapo atakuwa amepata somo kubwa.” Wiki ya maji, wananchi watahamasisha wananchi kuhusu upandaji miti na jinsi ya kuvuna maji ya mvua na ujengaji wa mabwawa.

Serikali imeahidi kuwa na mpango wa kujenga mabwawa yatatumika kuvuna maji ya mvua badala ya kuaacha yakipotea bure.

Wiki hiyo pia itatumika kuwapa elimu wananchi ya kujenga mabwawa ambayo yatawasaidia kuvuna maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na shughuli nyingine za kiuchumi.

Kwa sasa wastani wa upatikanji wa maji nchini ni asilimia 72.15 kwa wakazi wa vijijini, asilimia 86 kwa wakazi wa mjini na asilimia 75 kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na waziri.

Malengo ya kitaifa anasema ni kufikia asilimia 85 kwa wakazi wa vijiji na asilimia 95 kwa wateja wa mijini ifikapo mwaka 2020. Ili kufikia muda huo imebakia miaka mitatu

Ni matumaini ya Watanzania wengi kuwa maadhimisho ya mwaka huu, yatafungua mwanga kwa wananchi kujua umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji kutokana na elimu watakayopatiwa na lengo la serikali la kuwafikishia Watanzania wote huduma
bora ya majisafi.

Kadhalika mpango wa kuhakikisha uondoshaji wa majitaka, kwa wananchi waishio mijini na vijijini unafanikiwa.