Wiki ya Maji ifanyie kazi mabomba kupasuka

22Mar 2019
Salome Kitomari
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wiki ya Maji ifanyie kazi mabomba kupasuka

KAULIMBIU ya maadhimisho ya Wiki ya Maji mwaka huu ni: “Hakuna atakayeachwa; kuongeza kazi ya upatikanaji huduma ya maji na usafi wa mazingira kwa wote katika dunia inayobadilika kitabianchi”.

Kuongeza kazi ya upatikanaji huduma ya maji na usafi wa mazingira, inaendana na udhibiti wa maji yanayotiririka ovyo mitaani, ambayo yangewafikia wananchi, ingeongeza idadi ya wanaopata huduma ya majisafi na salama.

Usafi wa mazingira unaendana na kuhakikisha majitaka yanaondoshwa kwa wakati, mifumo ya majitaka inadhibitiwa, kuhakikisha hakuna majitaka yanayotiririka ovyo mitaani na kusababisha magonjwa ya mlipuko au uharibifu mwingine.

Licha ya jitihada zinazofanywa na Mamlaka ya Majisafi na Majitaka nchini, bado kuna maeneo yenye changamoto kubwa ya kudhibiti upotevu wa maji, ambayo wakati mwingine haihitaji rasilimali fedha nyingi au muda.

Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa), kila mwezi inatuma madai ya ankara za maji kwa wananchi na baada ya siku kadhaa, inawakumbusha kuhakikisha mhusika analipa deni lake.

Ujumbe huo hueleza kiasi cha maji ulichotumia na fedha unazodaiwa kulipa. Baada ya siku kadhaa unakumbushwa, kuwapo operesheni ya kukata maji nyumba kwa nyumba na kumtaka mhusika kulipa ankara kabla ya kukatiwa huduma hiyo.

Utaratibu huo ni mzuri sana kwa kuwa umerahisisha ulipaji wa ankara za maji na unamkumbisha mhusika, kila inapofikia hatua ya kukatiwa huduma, hakuna wa kumlaumu.

Kwa ujumla, mamlaka hii na nyingine zinafanya kazi nzuri kwa kuwa, sasa kiwango cha upatikanaji maji jijini Dar es Salaam, hakifananani na miaka iliyopita. Wananchi hawakuwa na huduma hiyo na maji kugeuka kuwa bidhaa adimu na ghali.

Kwa nguvu hiyo ya kudai ankara za maji, nilitarajia uwajibikaji, kwa maana ya kuhakikisha mabomba yanayopoteza maji ovyo yanadhibitiwa, siyo mitaa kuwa na madimbwi ya maji, ambayo yangetumiwa na wananchi, kupitia mabomba.

Jijini Dar es Salaam, ni kawaida kukuta maji yanatiririka ovyo kwa muda mrefu, pasipo udhibiti yatumiwe na watu na mwishowe mamlaka husika zinapata fedha.

Unaweza kupita mitaa ukadhani mvua ilinyesha siku hiyo, lakini kitakachokuonyesha kuwa mvua haikunyesha, ni maeneo mengine hayajalowa, ila kuna madimbwi ya maji katika makazi ya watu, ambayo maji yake yangetumiwa na wahitaji wengine.

Wakati mwingine, cha kushangaza wakati maji yanamwagika wananchi walioko katika mtaa wa pili au wa tatu hawana maji, kwa kuwa yanafunguliwa kwa awamu.

Waswahili wana usemi, hoja kwa vielelezo. Nami nitumie kielelezo. Katika eneo la uwanja ulioko karibu na Kanisa Katoliki Salasala, kuna mahali maji yanatiririka utadhani ni mfereji wa mvua.

Ni muda mrefu hali hiyo imedumu na siyo eneo lililojificha. Lakini, wananchi wanashangazwa kukosekana jitihada za haraka kuzuia upotevu huo wa maji.

Wakati yanatiririka, wananchi wa mitaa kadhaa hawana huduma ya maji kwa takribani wiki mbili, kwa kuwa tu anayepaswa kufungua hajaamua kufungua, jambo linalowafanya watu wajiulize maswali; maji yanaachwa yakimwagika kiasi hicho, maana yake yangedhibitiwa yangewafikia wananchi ambao wangelipa ankara na serikali kupata fedha.

Pia, eneo la Barabara ya Salasala, kuna mahali maji yanavuja kama vile ni mfereji wa maji, lakini kwa muda mrefu hakuna jitihada za kukabiliana na hali hiyo, kuhakikisha maji yanawafikia wananchi walipaji wa ankra.

Eneo la Sinza, nako ni kawaida kuona maji yanamwagika kwenye mitaa mbalimbali, jambo linaowafanya wananchi wajiulize, kazi nzuri ya kuboresha miundombinuna huduma ya maji, inashindwa kufanyika kudhibiti upotevu wake.

Kama kaulimbiu inavyosema, hakuna atakayeachwa katika kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji, basi jitihada zifanyike kudhibiti maji yanayopotea, ambayo yangewafikia wananchi, wangefurahi sana na mamlaka ingepata fedha.

Eneo jingine lililopo kwenye kaulimbiu, ni usafi wa mazingira, imekuwa tatizo jingine kubwa la majitaka kusambaa mitaani bila ua udhibiti. Mfano halisi, ni eneo la Mwenge madukani, kuna tatizo la chemba kumwaga majitaka na udhibiti wake unasuasua.

Yapo maeneo mengi yenye matatizo ya aina hiyo, hivyo katika kutekeleza kaulimbiu ya mwaka huu, ni vyema hatua zikachukuliwa kudhibiti upotevu wa maji na majitaka yanayosambaa ovyo mitaani.