Yanga, Azam zicheze kwa tahadhari ugenini

18Apr 2016
Adam Fungamwango
Nipashe
Mjadala
Yanga, Azam zicheze kwa tahadhari ugenini

YANGA inahitaji ushindi wa aina yoyote au sare ya kuanzia 2-2 ugenini ili kutinga hatua ya makundi ya mashindano ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri katika mchezo utakaofanyika keshokutwa Jumatano.

Kwa upande wa Azam inayocheza kesho dhidi ya Esperance yenyewe inahitaji sare yoyote ile iweze kutinga hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kwa vyovyote vile, wawakilishi wetu wana kazi ngumu ya kuhakikisha wanavuka vikwazo hivyo ingawa kwenye soka hakuna kisichowezekana.

Kama mechi hizi zingekuwa zinachezwa nyumbani na matokeo yaliyopo sasa yangekuwa yamepatikana ugenini, shughuli isingekuwa ngumu kama ilivyo sasa.

Nasema hivi kutokana na uzoefu wa miaka mingi kwa timu za Afrika Kaskazini maarufu kama Waarabu zinapocheza mechi za nyumbani na pia ugenini.

Kwa kawaida ya timu za Afrika ya Kaskazini yaani Waarabu hutafuta sare wakiwa ugenini au hata wakifungwa, hujipanga kutoruhusu zaidi ya bao moja.

Lakini pia wana tabia hata kama wakifungwa magoli mawili au matatu, wanasaka bao moja tu la ugenini ili liwarahisishie kazi.

Tuliona kwenye mechi kati ya Yanga dhidi ya Al Ahly, walionekana hawana haraka na walicheza mpira wa taratibu mno na pasi nyingi fupi fupi wakiwa na dhamira ya kupoteza muda ili mechi hiyo iishe kwa sare.

Na hata mpira ulipomalizika, makocha na wachezaji wa timu hiyo walishangilia kuonyesha kuwa lengo lao kwenye mechi hiyo lilikuwa limetimia.Kwa jinsi ilivyocheza Al Ahly ilionyesha kuwa kuna kitu wameficha.

Wameficha mpira wao halisi ambao watakwenda kuuonyesha nyumbani kwao, hivyo benchi la ufundi la Yanga na wachezaji wao inabidi wacheze kwa tahadhari.

Waarabu wana tabia ya kushambulia mfululizo wanapocheza nyumbani, hasa kwa kutumia mawinga na mabeki wao wa pembeni.

Nahodha ya wa Yanga Nadir Haroub 'Cannavaro' anakiri kuwa timu yake inabidi ipambane na washambuliaji wa Al Ahly ambao wanawatarajia watafanya mashambulizi kama 'nyuki' kwenye mechi hiyo ya marudiano.

Mfano ni kwenye mechi yao iliyopita dhidi ya Reacreativo do Libolo zilipotoka sare ya bila kufungana nchini Angola na kushinda mabao 2-0 Cairo.

Yoyote aliyeiona mechi hiyo alikubali kuwa Libolo ilikuwa kwenye wakati mgumu kutokana na kushambuliwa mfululizo, huku kipa wao akiwa nyota wa mchezo, vinginevyo ingefungwa idadi kubwa ya mabao.

Kutokana na hali hiyo, Yanga ijiandae kukutana na soka la kasi na kushambuliwa mfululizo mbele ya mashabiki ambao ni 'vichaa' kama ambavyo tulionjeshwa kidogo kwa wale wachache waliokuja nchini kuishangilia timu yao wiki iliyopita na kuwafunika wenyeji huku wakiwa wamevua mashati.

Kwa siku za karibuni, mabeki wa Yanga wameonakana kujichanganya, hivyo kocha Han van der Pluijm anatakiwa awe amelirekebisha hilo.

Kingine ni nidhamu ya ukabaji. Yanga inakwenda kucheza ugenini, hivyo mabeki wa timu hiyo wawe na nidhamu ya ukabaji, ili kuepuka penalti na hata kadi nyekundu ambazo zinaweza kuwagharimu.

Wachezaji wa Kiarabu ni wajanja sana kumtengenezea mtu kadi nyekundu na hasa wakiwa nyumbani.
Sina tatizo sana na Yanga kwa upande wa ushambuliaji, lakini kwa siku za karibuni wamekuwa wakipoteza nafasi nyingi za kufunga.

Inapokwenda kucheza ugenini ikumbuke ukicheza na timu yenye kaliba ya Al Ahly kupatikana nafasi ni vigumu, hivyo chache zinazopatikana zitumike vizuri kwa kufunga magoli na si vinginevyo.

Azam nayo itarajie pia soka la kasi na kushambulia mfululizo nchini Tunisia, hivyo kazi kubwa itakuwa kwa mabeki.

Benchi la ufundi la timu hiyo lifanye kazi kubwa ya kusuka ukuta wa timu hiyo ili kuhimili mashabulizi ya wenyeji, kwani kwa siku za karibuni mabeki wa Azam nao wamekuwa hawako kwenye kiwango kizuri.

Wamekuwa wakiruhusu magoli ya kizembe kwenye Ligi Kuu, lakini hata kwenye michuano hiyo ya kimataifa hasa ukitazama mechi yao dhidi ya Bidvest Wits FC ya Afrika Kusini iliporuhusu mabao matatu nyumbani.

Wachezaji wa Azam wakumbuke kilichotokea msimu uliopita iliposhinda mabao 2-0 nyumbani dhidi ya El Merreikh ya Sudan lakini ikatolewa kwa kuchapwa mabao 3-0 ugenini mjini Khartoum. Kosa hilo halitakiwi na lijirudie tena.

Ingawa itacheza bila wachezaji wake tegemeo Shomari Kapombe na Kipre Tchetche, lakini naamini watakaobaki wanaweza kuipeleka timu hiyo hatua ya makundi.

Kila la kheri Yanga na Azam ambao ndiyo wawakilishi pekee wa nchi waliobakia kwenye mashindano ya kimataifa.