Yanga bado haijakaa sawa!

12Oct 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Yanga bado haijakaa sawa!

“SIHADAIKE na rangi, tamu ya chai ni sukari.” Maana yake usidanganyike na rangi ya chai, utamu wake ni sukari.

Methali hii hutumiwa kumzindua mtu asipumbazike au asivutwe na sifa za kitu ila akichunguze kwa undani hakika ya kitu au kitu cha kushangaza ni kujionea mwenyewe. Ndio makala yangu ya leo.

“Kusifiwa si kuona, shani (jambo au kitu cha kushangaza) ni kujionea mwenyewe.” Hata ukasifiwa jambo na mtu aliyeshuhudia, haiwi sawa na kujionea mwenyewe. Heri kushuhudia jambo mwenyewe badala ya kuelezwa na aliyeshuhudia.

Kabla ya kuendelea, najitambulisha kwanza nilivyo. Nilijiunga na Yanga Desemba 2, 1966 na kukabidhiwa kadi namba 447 yenye picha ya mkono ulioshikilia mwenge. Mashabiki waliuita ‘mkono wa Kilambo’ (Mungu amrehemu) aliyekuwa beki machachari wa Yanga ya wakati ule.

Kadi zilipobadilishwa na kulipa malimbikizo ya ada za mwaka 1976 nilipewa kadi mpya mwaka 1977 yenye namba 01868 iliyoandikwaDaima mbele nyuma mwiko. Madhumuni ya Yanga: 1) Kudumisha na Kustawisha Michezo ya aina zote Tanzania. 2) Kushirikiana na Vyama vyote vya michezo katika Afrika na Ulimwenguni kwa Jumla.

Je, michezo ya aina zote imedumishwa na kustawishwa kwa mujibu wa kanuni ya kwanza? Je, ushirikiano wa Yanga na vyama vyote vya michezo katika Afrika na ulimwenguni kwa jumla umetendeka? Mbona siuoni au umri wangu (81 na miezi miwili) unanipiga teke?

Ahadi ya Mwana-Yanga: 3. Nitakuwa mwaminifu na mtiifu kwa chama na kushirikiana na wanachama wenzangu kukiimarisha Chama. Rushwa na Fitina ni adui wa chama changu nitasema kweli daima.

Wahenga walisema: “Kweli ndio fimbo ya kukamata.” Maana yake kweli ni silaha nzuri maishani. Twakumbushwa umuhimu wa kuusema ukweli hata kama kufanya hivyo tutaishia kuchukiwa na wenzetu.

Tuseme kweli: Sisi ni waaminifu na watiifu kwa Yanga na tunashirikiana na wanachama wenzetu kukiimarisha chama chetu? (Sio chama letu iandikwavyo na magazeti ya michezo!)

Mbona baadhi yetu wamekuwa ‘wanachama’ wa kuinyonya Yanga na kujinufaisha kwa fedha zinazopatikana? Tunashirikiana? Mbona hakuna la maana tulilofanya hata Yanga kwenda arijojo (uendeshaji usio na mwelekeo mwafaka kwa kukosa kuongozwa au kupangiliwa vizuri)?

Mwanachama atakuwa na wajibu ufuatao: (a) kuwa wakati wote mkweli na mwaminifu wa Klabu; (b) Kuwa wakati wote hadaiwi ada zozote za uanachama na (c) Kuhudhuria mikutano ya Klabu inayomhusu.

“Kweli ingawa chungu niambie sinifiche.” Maana yake niambie kweli hata kama mchungu. Methali hii yatufunza umuhimu wa kuwa na tabia ya kusema kweli.

Sasa nazungumzia mechi ya Ligi Kuu baina ya Yanga na Coastal Union iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam Jumapili iliyopita.

Niliitazama mechi ile kwa makini mwanzo mpaka mwisho, lakini sikuwa na amani. Kilichonifanya nisiwe na amani ni namna wachezaji wa Yanga walivyosumbuliwa na wenzao wa Coastal Union kutoka Tanga.

Yanga waliondoka uwanjani na alama tatu dhidi ya Coastal Union kwa ‘ushindi’ wa bao 1-0. Ingawa timu yangu ndio ‘iliyoshinda,’ lazima niwe mkweli. Sikushangilia ‘ushindi’ tuliopewa na refa akisaidiana na mshika kibendera wake. Kwa nini? Sikuona vizuri msukumano uliotokea kwenye lango la Coastal Union!

Kama twataka kujenga timu yetu, twapaswa kujisahihisha na kujihukumu wenyewe bila soni kwani hakuna binadamu asiyekosea. Ili kujikosoa lazima tukubali tunapokosa.

Baadhi ya wanachama wenzangu na mashabiki watanichukia kwa kusema hayo lakini nasimamia neno hili: “Kweli ndiyo fimbo ya kukamata.”

Ingawa ni kweli kuwa Yanga ndio timu iliyotwaa Kombe la Ligi Kuu ya Tanzania Bara mara nyingi kuliko timu zote zilizoshiriki na zinazoshiriki, ni kweli pia kuwa Yanga ya sasa yanipa shaka kama itafika mbali msimu huu!

Waandishi wa michezo walisifu sana usajili uliofanywa na Yanga msimu huu. Walisahau kuwa “mgema akisifiwa, tembo hulia maji.”

Methali hii huweza kutumiwa kuwanasihi watu wasimsifu mtu sana asije akafura kichwa na kuharibika. Pia hutumiwa kwa mtu ambaye asifiwapo huishia kujivuna. Yangu macho.

[email protected]
0784 344 096