Yanga halahala mti na macho

11Mar 2017
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Yanga halahala mti na macho

“HAUCHI hauchi unakucha.” Mtu husema hauchi, hauchi, lakini hatimaye jua hochomoza na usiku ukatoweka.

Methali hii hutumiwa kumtia mtu moyo anapokabiliana na hali ngumu kumshajiisha kuwa ni lazima atauona mwisho wa hali hiyo.

Yanazungumzwa mengi kuhusu mechi ya leo kati ya Yanga na Zanaco ya Zambia. Ni mzunguko wa pili wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Magazeti ya michezo yanaipamba mno Yanga badala ya kuikosoa ili ijirekebishe. “Yanga msiogope pesa ipo. Yaishika pabaya Zanaco.” Hakuna sehemu yoyote inayoeleza jinsi Yanga ‘ilivyoishika pabaya Zanaco’ ila ni kutaka magazeti yanunuliwe!

Binafsi sijaridhishwa na uchezaji wa Yanga. Kuna mambo yanayonitatiza. Kwanza ni washambuliaji wake kuwa wachoyo, kila mmoja akitaka kufunga hata kama hayupo kwenye nafasi nzuri ya kufunga. Kinachowazuzua ni ahadi wanazopewa kuwa kila bao litanunuliwa!

Kila mshambuliaji ataka awe mfungaji bora ili apate fedha. Hilo ndilo linalosababisha kila mshambuliaji kutaka afunge.

Wahenga walisema: “Mapaka mengi hayagwii panya.” Maana yake paka wakiwa wengi waweza kushindwa kumkamata panya kwa kutokuwa na mbinu ya pamoja.

Tukitaka kufanikiwa lazima tuwe tayari kushirikiana na wenzetu. Bila ushirikiano wa dhati timu haiwezi kushinda. Mchezaji yeyote atakayefunga si ushindi wake tu bali kwa timu nzima, viongozi, wanachama na mashabiki.

Pili: wachezaji wa nyuma, hususan mabeki, hushindwa kujipanga, hasa jinsi ya kukaba washambuliaji wa timu pinzani. Mabeki na viungo wasiwape nafasi washambuliaji wa timu pinzani. Lazima wajue jinsi ya kujipanga.

Wasiwape maadui nafasi ya kumiliki mpira kwa namna watakavyo huku wao wakirudi nyuma na kuwarahisishia washambuliaji wa timu pinzani kusogelea lango lao na mwishowe kufunga.

Mabao wanayofungwa Yanga mara nyingi husababishwa na uzembe wa mabeki kutojipanga vema huku washambuliaji wa wapinzani wakiachwa peke yao jirani kabisa na lango. Mabeki wa Yanga kurundikana pamoja na kugongana wenyewe kwa wenyewe hata kum-babaisha kipa na mwishowe kufungwa.

Tatu: Wachezaji wa Yanga huridhika mapema wanapokuwa mbele kwa ushindi, hata kwa bao moja! Bao moja halina muamana kwani wakati wowote timu pinzani yaweza kusawazisha .

Mara nyingi timu inayosawazisha huwa na nguvu zaidi huku iliyotangulia kufunga ikicheza kwa wasiwasi. Mfano ni mechi ya watani, wakati Simba ikiwa nyuma kwa bao la mapema lililofungwa na Simon Msuva. Mavugo wa Simba alisawazisha kipindi cha pili wakiwa pungufu na mwishowe Kichuya akafunga bao la pili na la ushindi dhidi ya Yanga.

Mzunguko wa kwanza hali ilikuwa hivyo. Bao la Kichuya la dakika za ‘lala salama’ liliwanyong’onyesha wachezaji wa Yanga na kuwanyamazisha mashabiki wao waliojihakikishia ushindi wa bao moja dhidi ya Simba, lakini Kichuya akaisawazishia Simba kuwa 1-1 dakika za mwisho.

Mechi ya leo Jumamosi Yanga inaanzia nyumbani. Timu watakayopambana nayo si kama Ngaya ya Comoro wala Kiluvya United.Haitakuwa hivyo kwa Zanaco ya Zambia.

Yanga yapaswa kucheza kwa bidii na tahadhari kwani kutoa sare/suluhu au hata kushinda kwa bao moja au mawili nyumbani itakuwa bado haijajihakikishia ushindi kwani mechi ya marudiano itakuwa ugenini, Zambia. Kama hawatapata ushindi wa maana nyumbani, ugenini itakuwaje?

Iige mfano wa Simba ambayo ilifungwa mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru) na timu ya Mufulira Wanderers ya Zambia. Mechi ya marudiano iliyochezwa Zambia Simba iliishindilia Mufulira Wanderers mabao 5-0, mbele ya Rais Kaunda wakati ule.

Yanga halahala mti na macho.
[email protected]
0715/0784 33 40 96