Yanga inahitaji muda, waachieni makocha

20Jan 2020
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Yanga inahitaji muda, waachieni makocha

KIPIGO cha bao 1-0 ilichokipata Yanga dhidi ya Azam FC kimeleta mambo na maneno mengi kutoka kwa wanachama na mashabiki wa Yanga. Ni sawa tu na msiba wa 'mswahili' ambao siku zote haukosi sababu.

Hii ni baada ya mfululizo wa matokeo mabaya yanayoyapata. Ilichapwa mabao 3-0 dhidi ya Kagera Sugar, kabla ya kupigwa bao 1-0 Jumamosi iliyopita dhidi ya Azam FC. Ikumbukwe kuwa Yanga ilitoka kupata pointi moja tu, kwa kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Simba, hivyo mechi tatu kuambulia pointi moja tu.

Ni moja ya matokeo mabaya kwenye historia ya klabu hiyo kongwe kabisa nchini. Wanachama na mashabiki wameonekana kila mmoja kutoa lawama kivyake. Wengine wanalaumu waamuzi. Wengine wanailaumu Bodi ya Ligi. Wapo wanaomlaumu Kocha Boniface Mkwasa, sijajua kwa nini. Kuna wanaowalaumu viongozi wao kwa kubadilisha makocha mara kwa mara.

Nimemsikiliza beki wa Yanga, Juma Abdul baada ya mechi hiyo. Kusema kweli maneno aliyoongea mchezaji huyo yalipaswa kuongewa na viongozi wa Yanga.

Maneno yake yanakwepwa kuzungumzwa na viongozi wa klabu hiyo, hivyo kujipa wakati mgumu wao wenyewe mbele ya wanachama na mashabiki wao.

"Unajua sasa hivi Yanga tuko kwenye kutengeneza timu, alikuwa mwalimu Zahera (Mwinyi) alisajili wachezaji, lakini baadaye akaondoka, wakaja wachezaji wapya, tukawa na Master (Mkwasa), muda mfupi tu tukawa naye, akaja mwalimu mpya (Luc Eymael) na yeye anakuja na mifumo yake, kwa hiyo bado saa hizi mwalimu yuko kwenye kutengeneza timu," anasema mchezaji huyo na kuwataka wanachama na mashabiki wa Yanga kuwa watulivu na wavumilivu.

Haya ni maneno ambayo yana ukweli kwa asilimia nyingi na yalipaswa kutolewa na viongozi wa Yanga ili kuwapoza wanachama na mashabiki wao wasiwe na matumaini makubwa sana.

Abdul ameamua kueleza ukweli kuwa kutokana na mabadiliko haya ya kuondoa wachezaji waliosajiliwa dirisha kubwa na kusajili wengine dirisha dogo, pamoja na mabadiliko ya benchi la ufundi, bado timu haijakuwa na muunganiko.

Hicho ndiyo kinachohofiwa kuongewa na viongozi wa Yanga kwa sababu wao wamewaaminisha wanachama na mashabiki wao kuwa kwa usajili uliofanywa basi timu itatwaa ubingwa.

Ina maana kama wakisema kuwa wanatengeneza timu, wanachama na mashabiki watajua kuwa basi msimu huu hakuna ubingwa.

Na wao ndiyo watanyooshewa vidole kwa sababu walifanya usajili mwanzoni mwa msimu na kuwaaminisha kuwa wachezaji waliosajiliwa ni bora wanaoweza kutwaa ubingwa, lakini wengi wao walioonekana watakuwa muhimu kwenye timu wanaondolewa kipindi cha dirisha dogo na kuletwa wengine.

Kama ni kukosea wameshakosea, viongozi wa Yanga wanapaswa kuwaondolea tamaa ya ubingwa mashabiki wao na kuwaambia ukweli kuwa wanatengeneza timu kwa sababu wana wachezaji wengi wapya.

Hapo si tu kwamba wanawashusha presha mashabiki wao tu, lakini hata wacheaji wapya ambao wanalazimika kucheza kwa presha na wasiwasi wakati bado hawajaingia kwenye mfumo wa timu.

Sisemi kwamba Yanga haiwezi kupata ubingwa la hasha, ila presha ya ubingwa ikiondoka kwa mashabiki, makocha na wachezaji wakaachwa watengeneze mfumo na kucheza bila shinikizo, inaweza kuwasababisha kupata matokeo mazuri zaidi na hatimaye kutwaa ubingwa.

Yanga haitakiwi iishi kwa kushindana na Simba na Azam kwa sababu yenyewe imeshabadilisha wachezaji kadhaa, huku wenzao wakiwa na wachezaji wengi wale wale ambao msimu uliopita walicheza Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Mfano Simba bado ina wachezaji wengi ambao waliiwezesha timu hiyo kutinga Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa, wakati yenyewe waliocheza Ligi ya Mabingwa msimu huu tu wameshaachwa.

Umefika wakati kwa Yanga sasa kukubali matokeo yoyote yanayopatikana na kushusha matumaini makubwa ya ubingwa kwa sababu kama alivyosema Abdul kuwa inajenga timu ambayo ni kama mpya tu kwa sasa.

Ila litakuwa ni fundisho kwa viongozi wa Yanga, isiwe tena ligi inaisha wanaacha tena wachezaji wengi na kusajili wengine wapya, badala yake kama waliopo watakidhi, basi wanatakiwa wasajili wachezaji wachache tu wa kuongezea nguvu. Vinginevyo watakuwa hawafanyi kitu, badala ya kusonga mbele wanakuwa hapo hapo tu.