Yanga kuna’ni msimu huu?

02Nov 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Yanga kuna’ni msimu huu?

“MTOTO akililia wembe mpe.” Maana yake mtoto auliliapo wembe, mpe; ukimkata atauogopa.

Methali hii hupigiwa mfano mtu anayeng’ang’ania kufanya jambo ambalo laweza kumdhuru. Ni heri kumwacha afanye atakalo ili ajifunze kutokana na matatizo atakayopata.

Pia “Mtoto mkaidi mngoje siku ya ngoma.” Maana yake mtoto asiyesikia aambiwalo huishia kuzinduka apatapo matatizo. Hutumiwa kumpigia mfano mtu mwenye tabia ya ukaidi na ubishi ambaye aghalabu huishia kufikwa na maafa na dhiki.

Yapo mambo mengi yanayonipa wasiwasi kuhusu kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera, raia wa DR Congo. Mwanzoni, kocha huyu alikuwa kipenzi cha wanachama na mashabiki (watu wenye mapenzi na hamasa kubwa juu ya jambo au kitu fulani) wa Yanga.

Aliingia mkataba na Yanga wakati timu hiyo ikiwa imedhoofika (kitendo cha jambo au hali kupungua nguvu au uwezo wake) kwa hali na mali.

Haikuwa na wachezaji wazuri wa kulinganishwa na Simba; haikuwa na fedha za kusajili wachezaji wazuri na waliokuwapo hawakumaliziwa fedha zao za usajili.

Hata mishahara yao ililipwa kwa mafungu, tena kwa mbinde! Ni kipindi alichoingia kocha Mwinyi Zahera kuifundisha timu ya Yanga.

Alichukua timu ya wachezaji waliokata tamaa kutokana na ugumu wa kuendesha maisha yao. Zahera akaingia kwenye uchangishaji fedha ili kuwanusuru wachezaji waliokata tamaa na matumaini kuendelea kuichezea timu ya Yanga!

Kuna wakati alitoa fedha zake na hata kuchangisha fedha kwa wanachama na mashabiki ili kuwanusuru wachezaji. Alipendwa na kusifiwa kila kona kwa jinsi alivyoijenga timu ya Yanga kiasi cha kuwa tishio kwa Simba iliyokuwa ikitetea ubingwa wake kwa msimu wa pili mfululizo.

Taratibu hali ya hewa ikabadilika pale Yanga ilipofungwa kwa mara ya kwanza msimu huo. M-babe wake ni timu ya Ruvu Shootinga ya Pwani.

Wahenga walisema “Hakuna mume wa waume” wakiwa na maana hakuna mtu anayeweza kuwashinda wanaume wenzake wote.

Ni methali ya kutumiwa dhidi ya mtu anayejitia ubabe au anayejidai kuwa na nguvu kama njia ya kumnyamazisha.

Wanachama na mashabiki wa Yanga wasiokuwa na hekima/busara watadhani mimi niko upande mwingine. Nilijiunga na Yanga Desemba 2, mwaka 1966 kwa kadi namba 447.

Kadi yangu ya nne yenye namba 007887 ambayo ndiyo inayotumika mpaka sasa niliipata Februari 7, mwaka 2008. Imebidi nieleze yote hayo ili kuwanyamazisha wenye shaka (hali ya mtu kuwa na wasiwasi juu ya jambo) na mimi, hasa wasiotaka Yanga ikosolewe! Msimamo wangu ni kwamba

“Kweli ndio fimbo ya kukamata.” Maana yake kweli ni silaha nzuri maishani. Hii ni methali ya kutukumbusha umuhimu wa kusema kweli hata kama kufanya hivyo tutaishia kuchukiwa na wenzetu. Mwinyi Zahera alionekana kuwa ‘mkombozi’ wa Yanga.

Wahenga walikuwa sahihi waliposema “Ngoma ya wana haikeshi.” Kwamba ngoma inayochezwa na watoto au vijana haikawii kuvunjika kutokana na kutoelewana au kutokuwapo kiongozi wa kuwachezesha. Methali hii hutumiwa na wazee kupigia mfano jambo la kitoto lililoishia kuharibika kwa kutokuwapo ushauri au kupuuzwa mashauri yanayofaa.

Pengine kuna waliosahau jinsi Mwinyi Zahera alivyopendwa hata kuwa kama ‘Mwenyekiti Msaidizi’ wa Yanga. Alikuwa kila kitu pale Yanga ingawa viongozi halisi waliochaguliwa na wanachama walikuwapo! Mwinyi Zahera alikuwa msemaji wa Yanga.

Alichangisha fedha ndani na nje ya Dar es Salaam kwa ajili ya wachezaji. Alisaidia kutoa hela zake kuwasafirisha wachezaji nje ya nchi wakati klabu iliposhindwa kukamilisha fedha za nauli. Aliwanunulia chakula wachezaji na kuwapa hela waliofanya vizuri uwanjani.

Alikuwa baba mlezi wa wachezaji. Kabla ya ligi ya msimu huu kuanza, alitoa mapendekezo yake kwa viongozi kuhusu wachezaji anaowataka.

Aliwataja kwa majina na timu wanazochezea. Viongozi wa sasa wakamtimizia kila alichotaka na kumwachia ashindwe mwenyewe.

Magazeti yetu ya michezo nayo yakawa mstari wa mbele kuichafua Yanga! Kwa vipi? Kila mchezaji aliyesajiliwa alisifiwa kupita kiasi.

Kwamba mchezaji huyu akitua Yanga, timu zingine zitakwisha! Ikawa ni kazi ya kumsifu kila mchezaji aliyesajiliwa kuwa ni “moto wa kuotea mbali.” Je, ni kweli? Nionavyo, wachezaji hao ni “moto wa kuotea karibu sana” ndio upate joto lake kwani “Kula uhondo kwataka matendo.” Ikiwa mtu anatamani kula vitamu lazima awe na matendo au afanye kazi kwa bidii.

Twanasihiwa tufanye kazi kwa bidii na juhudi ikiwa twataka mafanikio. Hamna jambo zuri linalojileta; sharti tuwe tayari kufanya kazi kwa bidii na maarifa. Wachezaji wote waliotakiwa na kocha Zahera wamepatikana na kusajiliwa kwa mbwembwe.

Bado hatujaona umahiri wao uwanjani! Wengi wao hawana tofauti na wachezaji wetu na baadhi yao wamepitwa kwa mbali na wachezaji wetu! Ni kocha Zahera yule yule aliyesifiwa kila upande nchini ambaye sasa anasemwa vibaya na wale wale (nikiwamo mimi) waliokuwa wakimpamba kwa maneno na kumpa kila aina ya sifa.

Sasa ni dhahiri shahiri (ni wazi kabisa; isiyoweza kufichika) kuwa umaarufu wa Zahera umekwenda arijojo (hali ya kupoteza mwelekeo).

Ndo maana hata Yanga ilipocheza na Pyramids ya Misri jijini Mwanza na kufungwa mabao 2-1, kwa mara ya kwanza Zahera alirushiwa chupa za maji akiambiwa “tumekuchoka … hatukutaki …!” Jambo pekee la kumwokoa Zahera ni Yanga kuifunga Pyramids kesho nyumbani kwao Misri, kama ilivyofungwa Yanga jijini Mwanza.

Mechi ya marudiano ugenini ndio ya kum-beba au kumfurusha Mwinyi Zahera Yanga kesho. Tusibiri tuone.

[email protected] 0784 334 096