Yanga punguzeni matamko, ielekezeni nguvu kiufundi waamuzi si kwenu tu

22Feb 2021
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Yanga punguzeni matamko, ielekezeni nguvu kiufundi waamuzi si kwenu tu

JUZI Jumamosi Yanga ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar. Ni ushindi ambao naona utatuliza munkari ya wanachama na mshabiki wake.

Utatuliza pia presha ya viongozi wa Yanga, ambao waliitisha mkutano na waandishi wa habari kulalamikia kile walichodai kutotendewa haki na waamuzi. Wanadai waamuzi wamekuwa hawawatendei haki, wakitolea mfano kwenye mechi dhidi ya Mbeya City kwa kunyimwa penalti na kwenye mechi dhidi ya Kagera Sugar.

Kabla ya viongozi hao kuitisha mkutano huo, tayari baadhi ya wanachama na mashabiki wa Yanga walikuwa wakilalamika kuonewa na waamuzi.

Viongozi wao wakaenda kuongea kile kile. Ukiangalia jinsi ambavyo viongozi wa Yanga walivyokuwa wakiongea utaona na wao wanaendeshwa na mihemko ya baadhi ya wanachama na mashabiki wao.

Hao hao baadhi ya mashabiki baada ya mechi dhidi ya Kagera Sugar, waliwajia juu baadhi ya viongozi hao.

Wakawatuhumu kukaa kimya, bila kutoa tamko ya kile wanachoona kuwa wanaonewa. Kesho yake kweli viongozi hao waliitisha mkutano na waandishi, nadhani lengo ni kuwapoza kuonyesha kuwa tayari wameongea.

Wale mashabiki ambao hawaamini kuwa wanaonewa na waamuzi, wao walilalamika upangaji wa timu haukuwa mzuri.

Wakadai kuwa Mukoko Tonombe anatakiwa aanze na si Zawadi Mauya. Pia wakidai kuwa Ditram Nchimbi anatakiwa acheze winga na si straika wa kati.

Kwenye mechi dhidi ya Mtibwa Sugar hayo yote yalionekana kufanyiwa kazi. Sijajua kuwa viongozi walimwambia kocha, au mwalimu mwenyewe alisikiliza maoni ya mashabiki na wachambuzi. Hata hivyo, kiufundi si nzuri sana, lakini hili nimeliweka kuonyesha kuwa kuna kitu kama kuogopa baadhi ya wanachama na mashabiki kwenye klabu hiyo.

Sijui kama mechi hiyo ingeisha kwa sare, nini tena kingetamkwa na mashabiki. Mimi nadhani kila mmoja, viongozi na benchi la ufundi ifike wakati wafanye kile wanachoamini na si kupelekeshwa na kile ambacho mashabiki wanasema. Hawa wanachotaka ni ushindi tu. Na kama timu haipati ushindi inabidi litafutwe suala la kiufundi na si kusikiliza wao wanasema nini, kwa sababu ipo siku watawageuka na kusema "Kwa nini mnafanya kazi kwa kutufuatisha sisi mashabiki?"

Kuhusu kile kinachodaiwa kuonewa na waamuzi, hili nalo linafikirisha. Sidhani kama kuna timu yoyote ile ambayo haijawahi kukutana na kadhia ya waamuzi wa Tanzania. Tumekuwa tukiona maofisa habari, makocha na wachezaji wakilalamikia waamuzi kwa baadhi ya mechi.

Lakini baada ya hapo maisha yanaendelea na sijasikia, matamko ya viongozi mpaka kutishia kujitoa. Masau Bwire na Ruvu Shooting yake kuna wakati walilalamika, juzi Malale Hamsini naye akiwa na Polisi Tanzania yake alilalamika.

Ni kweli waamuzi wanafanya makosa kwenye baadhi ya mechi, lakini hii haina maana kuwa hawaipendi timu fulani au wana njama fulani, haya yanakuwa ni makosa tu ya kawaida, wakati mwingine ya kibinadamu, au uzembe.

Ndiyo maana viongozi wa Yanga walipotoa tamko hilo, Kagera Sugar wao wakatoa kumbukumbu ya vipande vitatu vya video, mechi ya mzunguko wa kwanza, beki wa Yanga wakishika mpira ndani ya eneo la hatari, nyingine mbili ni mechi za Kombe la FA msimu uliopita wakati timu hizo zilipokutana, wakionyesha kuwa walinyimwa penalti ya dhahiri na wapinzani wao kupewa penalti ambayo haikuwa halali.

Nadhani walitaka kuonyesha kuwa haya huwa yanatokea na kulalamika ni wajibu, lakini ninavyojua kuna taratibu za kulalamika au kuwasilisha rasmi malalamiko. Hili lililofanywa na viongozi wa Yanga ni kama vile kutaka kupata huruma kutoka kwa mashabiki wao ili wao wasionekane wana matatizo na kuwatupia waamuzi ambao huwa hawakosei kwenye mechi dhidi yao tu.

Kwa baadhi ya mashabiki sijui kwa makusudi au bahati mbaya na wao wamekuwa wakilibeba hili la waamuzi kiasi cha kutoa maneno ya vitisho. Nilichofurahi ni kwamba pamoja na vitisho au shinikizo fulani kuelekea kwenye mechi dhidi ya Mtibwa, lakini waamuzi walichezesha kwa haki, bila presha, wala woga na mshindi alipatikana kwa haki bila malalamiko.

Na si kwamba hakukuwa na makosa ya kibinadamu. Yalionekana, lakini huwezi kusema yalikuwa ya kubeba upande wowote.