Yanga wasilaumiane, wajipange msimu ujao

20Jul 2020
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Yanga wasilaumiane, wajipange msimu ujao

MSIMU ujao klabu kongwe ya Yanga haitoiwakilisha Tanzania kwenye michuano yoyote ile ya kimataifa, kutokana na kuukosa ubingwa na kama vile haitoshi kuchapwa mabao 4-1 na watani zao wa jadi Simba, ikitolewa kwenye harakati za kusaka tiketi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Hali hii imezua mtafaruku kwa baadhi ya wanachama na mashabiki wa Yanga na hasa baada ya kuchapwa mabao 4-1 dhidi ya Simba, Jumapili ya Julai 12 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kila mtu anaongea lake. Kuna wanaoulaumu uongozi. Wapo wanaolaumu wachezaji. Wengine nao wanamlamumu mtu mmoja mmoja, hasa mchezaji wao aliyekuwa tegemeo na kipenzi, Mghana Bernard Morrison.

Inavyoonekana ni kama viongozi wa Yanga nao wameingia kwenye mtego huo na kuanza kulalamika na kumlaumu Morrison, wakati ni wao wenyewe ndio waliyempa kiburi hicho.

Ni mchezaji ambaye baada ya kuonekana ana uwezo mkubwa wa hali ya juu, alianza kupewa malezi tofauti na wenzake. Kila anachofanya alikuwa anachekewa, kwa sababu tu 'anaupanda mpira'. Mchezaji huyo akaifunga Simba kwenye mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga ikashinda bao 1-0.

Morrison akaendelea kudeka, huku viongozi wakimdekeza anavyotaka. Kuna wakati walionekana kama wamemchoka, lakini ghafla ikaja mechi ya Simba dhidi ya Yanga, baada ya timu hizo kushinda mechi zao za robo fainali ya Kombe la FA.

Viongozi wa Yanga wakajua kabisa kuwa mkombozi wao anaweza kuwa Morrison kwa mara nyingine.

Kukariri kwao ndiko kulikofanya kumrudisha tena kundini. Tena wakamsafirisha kabisa kumpeleka mkoani Kagera ilipocheza dhidi ya Kagera Sugar na akafunga bao pekee, lililowafanya viongozi hao kuona walichofanya ni sahihi.

Kituko kilikuwa kwenye mechi dhidi ya Simba, alipotolewa mchezaji huyo na kutoka moja kwa moja nje na hakuonekana tena.

Sijajua kama angekuwa amefunga goli na Yanga ikashinda akafanya kama alivyofanya angesakamwa hivi. Nadhani hii inatokana na Yanga kupoteza mechi hiyo, ndiyo maana gunia la misumari limemuangukia Morrison ambaye ndiye aliyepewa jukumu la kuiangamiza Simba.

Hayo yote yamepita, binadamu siku zote hujifunza kutokana na makosa. Baadhi ya makosa ambayo viongozi wa Yanga waliyafanya msimu huu ni kufanya usajili kwa mihemko.

Nakumbuka wakati msimu unaanza ilikuwa na wachezaji kama kina Juma Balinya, Urkhob Sadney, Issa Bigirimana, Mustapha Selemani na wengine wengi ambao waliachwa kwenye dirisha dogo na kusajiliwa wengine kama kina Yikpe Gnamien, Morrison mwenyewe, Ditram Nchimbi, Tariq Seif na wengineo ambapo hakukuwa na tofauti kubwa kati ya walioondoka na waliopo.

Nafikiri viongozi wa Yanga walifanya haraka sana kuwaondoka kina Balinya kwenye dirisha dogo. Wangekuwa wavumilivu, huenda Yanga isingekuwa kama hivi ilivyo leo, ambapo mashabiki wengi wanalalamika kuwa kikosi hakipo vizuri msimu huu.

Nakumbuka kikosi kile cha kina Sadney, nusura kitinge hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa kama si kufungwa na Zesco ya Zambia mabao 2-1 ugenini, tena kwa bao la Yanga kujifunga wenyewe kupitia kwa Abdulaziz Makame. Na hii ni baada ya kutoka sare ya bao 1-1 nchini Tanzania, tena Zesco wakipata bao dakika za majeruhi.

Ukiangalia kikosi kile cha mzunguko wa kwanza kilionekana ni bora zaidi, lakini ulikosekana uvumilivu tu kwa baadhi ya viongozi wa Yanga.

Cha kufanya sasa si kulaumiana, wala kutumia nguvu nyingi kumlaumu Morrison au kujibizana naye, badala yake kuanza taratibu kujipanga kwa msimu ujao wa Ligi Kuu ambao sina shaka utakuwa mgumu zaidi kuliko huu unaomalizika.

Badala ya kutumia muda mwingi kulalamika, viongozi wa Yanga wangetumia muda huu kuanza kusaka wachezaji bora ambao watakuja kukiongezea nguvu kikosi.

Kama alivyosema mchezaji wa zamani wa klabu hiyo, Boniface Ambani kuwa Yanga inahitaji wachezaji bora wachache ili kufanya timu kuwa yenye ushindani na si kuwa na wachezaji wengi ambao uwezo wao ni mdogo.

Ambani akasema kuwa Yanga si lazima isajili wachezaji 30, bali hata 25 tu na hiyo pesa ya watano iliyobaki, iongezwe kwenye kupata wachezaji wenye thamani na uwezo mkubwa. Naungana na Ambani kuwa Yanga isipangue kikosi chote kwa hasira na kusajili wachezaji wengi wapya la hasha.

Kinachotakiwa kufanywa ni kusaka wachezaji wachache, lakini wa gharama kubwa wanaoungana na wenye uwezo mkubwa waliopo, kutengeneza kikosi imara na si kusajili wachezaji wengi kwa ajili ya kufurahisha mashabiki kipindi cha usajili kinachotarajiwa kuanza Agosti Mosi, mwaka huu.