Yanga yaingia kwenye mtihani

06Jun 2020
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Yanga yaingia kwenye mtihani

‘MTIHANI’ ni utaratibu wa kupima maarifa aliyonayo mwanafunzi kuhusu somo alilofunzwa. Msukosuko unaomfika mja katika maisha; majaribu.

Maswali yanayojibiwa chini ya usimamizi maalumu ili kupima maarifa aliyonayo mtu anayepimwa. Tatizo ambalo Mungu humzushia mtu ili kumjaribu imani yake.

Kabla ya uongozi wa sasa wa Yanga kuingia madarakani, klabu hiyo ilikuwa ikiendeshwa vizuri bila matatizo. Baada ya kuondoka ndipo wanachama na wasio wanachama wakabaini umuhimu wao. Klabu iliyumba mpaka ikaitwa ‘watembeza bakuli,’ yaani kuomba fedha ili kuisaidia.

Ni dhahiri kuwa wapo watu na kampuni (sio ‘makampuni’ ) kadhaa zilizokuwa na nia ya kuisaidia Yanga lakini kutokana na viongozi kutokuwa na maono ya muda mrefu wakakata tamaa, hivyo klabu iliyumba sana.

Yanga ilikuwa na wakati mgumu kusajili wachezaji wa maana kwa kutokuwa na fedha. Hata kulipa mishahara ya waliokuwapo ilikuwa shida na baadhi yao kudai fedha zao za usajili!

Ilivyokuwa wakati ule, Yanga ilikuwa ikishinda kwa kubahatisha katika michezo yake. Hali hiyo iliwakatisha tamaa, si wanachama na wapenzi wake tu bali pia wachezaji waliokusudia kusajiliwa na timu hiyo. Mchezaji gani angejiunga na Yanga ilhali waliokuwapo hawakulipwa kwa miezi mitatu na kuendelea?

Kama hiyo haikutosha, baadhi yao na mashabiki wakaacha kwenda uwanjani kuishangilia. Wachache waliojinusuru kwenda uwanjani, hawakujaza eneo la Yanga. Hivyo eneo la Yanga likatwaliwa na idadi kubwa ya wapenzi wa Simba!

Jambo hili likaongeza pigo kwa Yanga ikilinganishwa na Simba iliyokamatwa barabara na kijana bilionea wao, Mohammed Dewji maarufu Mo.

Hii ilisababisha hata wapenzi na wanachama wa Simba waliokuwa wamekata tamaa kwenda uwanjani, wakarejea kila timu yao ilipokuwa na mechi. Wakajaza eneo kubwa la Yanga waliokuwa wamekata tamaa na timu yao!

Katika miaka ya ’60 Yanga iliitwa ‘foo-o-foo’ kwani mara kwa mara ilipocheza, ilifungwa mabao manne! ‘foo-o-foo’ ni aina ya magari yaliyoitwa Peujeot 404.

Sitaki kueleza mengi ya wakati uliopita kuhusu Yanga, kwani hata Wahenga walisema: “Iliyopita si ndwele, tugange yajayo.”

Maana yake ugonjwa uliokwishapita huwa si chochote hata kama ulikuwa mkali vipi; almuradi umeshapita haumshughulishi mtu kama unaokuja. Methali hii yatufunza umuhimu wa kujiandalia matatizo au shida zijazo badala ya kuziwazia zile zilizopita.

Sasa Yanga ina udhamini wa kampuni ya GSM inayoonekana kuwa na mipango mizuri kwa timu hiyo iitwayo ya ‘wananchi.’

Kwa juhudi za GSM, sasa Yanga imewekeana mkataba na kampuni inayoendesha Ligi Kuu Hispania (La Liga) wa udhamini wake.

Endapo mpango huo utafanikiwa, basi Yanga itakuwa na uwezekano wa kupata mafunzo ya wachezaji, makocha na viongozi kutoka klabu ya Sevilla ya Hispania.

Vilevile Yanga itacheza mechi mbili moja Tanzania na nyingine Hispania kwa mwaka kati yake na timu maarufu ya Sevilla. Aidha kutakuwa na fursa ya wachezaji chipukizi wa Yanga kujiunga na shule ya michezo ya timu ya Sevilla yenye historia kubwa.

Wataalamu wa Sevilla watakuwa wakija Tanzania kutoa mafunzo ya uongozi kwa sababu mfumo utakaotumiwa na Yanga ni lazima uendane na ujuzi na uzoefu katika masuala ya uongozi, kwa mujibu wa mkataba uliotiwa saini majuzi.

Makubaliano ya mkataba huo ni kwamba huduma ya ushauri wa Yanga, La Liga na GSM utagharimu Sh. bilioni 2.6 kwa miaka mitatu.
GSM itagharimia shughuli zote za wataalamu wa La Liga watakaokuwa na ofisi yao kwenye jengo la kampuni hiyo barabara ya Samora jijini Dar es Salaam.

Wakati hali ikiwa hivyo, Rais wa klabu ya Sevilla, Jose Castro, Carmona alisema anafurahi Yanga kuwekeana mkataba na La Liga na Sevilla kwani anaridhishwa na ujuzi na uzoefu walionao katika masuala ya kandanda, uongozi na uwekezaji.

Naye Mkurugenzi wa biashara wa kimataifa wa La Liga, Juan Botella alisema wamefurahi kuingia mkataba na Yanga inayokuwa klabu ya kwanza Afrika. Alisema kampuni yao yenye wataalamu wa kimataifa, watashirikiana na Sevilla kuhakikisha Yanga inakuwa na mfumo wa kisasa katika uendeshaji wa klabu.

Kwa upande mwingine, Mkurugenzi wa Kimataifa wa Masoko na Biashara wa Sevilla, Oscar Mayo alisema makubaliano yao na Yanga yanakusudia kuleta maendeleo ya ufundi, masoko na uongozi.

Sasa wanachama na mashabiki wa Yanga wanapaswa kuwa wamoja wakati klabu yao ikijengwa upya. Wasikubali kughilibiwa na baadhi ya viongozi wanaopinga mkataba huo kwa kukosa nafasi ya kuinyonya Yanga. Ikiwezekana wawaumbue hadharani ili watolewe kwenye uongozi. Salaam aleikum jamii.

[email protected]
0784 334 098