Zawadi bora kwa watoto ni malezi yaliyokamilika

09Aug 2016
Elizaberth Zaya
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Zawadi bora kwa watoto ni malezi yaliyokamilika

WATOTO wanahitaji mwongozo mzuri tangu wakiwa wadogo ili kuwajengea msingi mzuri na ustawi wa maisha yao ya siku zijazo.

Hii ni kutokana na ukweli kuwa nyumba yenye nsingi imara husimama imara bila ya kutetereshwa na chochote kile.Na wahenga walisema samaki mkunje angali mbichi,kwamba akikauka atakunjika.

Msemo huo, unamaanisha kwamba, msingi wa malezi wa mtoto unatakiwa kujengwa vyema tangu akiwa mdogo ili kuhakikisha kuwa, safari yao ya maisha inakwenda vyema katika maisha yao yote ili kuifanya jamii inufaike na uwepo wake na sio vinginevyo

Usemi huu unatufundisha kuwa watoto wanatakiwa waonyeshwe malezi na njia nzuri wakiwa bado wabichi kwa kuanzia na upendo na kuthaminiwa kikamilifu..

Katika familia au jamii zetu kuna changamoto kubwa linapokuja suala la malezi ya watoto. Baadhi ya wazazi wanashindwa kuwajibika kikamilifu katika malezi ya watoto wao na hivyo kujikuta wakiwajengea msingi mbaya watoto hao ambao ni taifala baadaye.

Wazazi hao wanaacha majukumu hayo muhimu na kujikuta wakitilia mkao majukumu mengineyo yakiwemo kulewa ama kuweka nguvu zao zaidi katika shughuli zao za kujitafutia kipato na mali hata kujikuta wakisahau kuwalea watoto wao hata majukumu hayo kuwaachia wasaidizi wa nyumbani(house girl ama house boy).waifanye kazi hiyo.

Kutokana na aina hiyo ya maisha, watoto hao hujikuta wanakua katika mazingira ya kubahatisha hasa linapokja suala la kulelewa katika misingi inayozingatia maadili kutoka kwa wasaidizi hao ambao baadhi yao maadili yao ni ya kubahatisha hata kukosa upendo na dira halisi ya maisha yao na kujikuta wakiwa na maisha ambayo hayakubaliki kabisa katika zama hizi.

Ni vema wazazi wakatambua kwamba, jukumu la malezi kwa watoto ni la wazazi wote, yaani baba na mama na haliwezi kubadilika hata kama wazazi hao wana mtu au watu wa kuwasaidia kulea nyakati wanazokuwa wamekabiliwa na majukumu mengine.

Malezi ya wazazi kwa watoto, nasaha na miongozo huwa ni kumbukumbu nzuri katika kufanikisha maisha yao ya kuwafanya kuenenda katika njia ipasayo ambayo huifuata hata wakifika uzeeni.

Kabla ya mtoto kufikia katika hatua ya kwenda shule na kujichanganya kwenye makundi, anatakiwa awe tayari amepatiwa msingi bora na imara kutoka kwa wazazi wake, ambao lengo lake ni kumsaidia asitikisike ama kujifunza mambo mengine yasiyofaaa kutoka kwa makundi anayokutana nayo, ambayo yanaweza kumhatarishia ustawi wake wa maisha ya usoni.

Kadhalika, katika kufanikisha ustawi huo katika maisha yao, hawahitaji kuona mpasuko kwa wazazi ama familia zao kwa sababu hizo nazo huchangia kuweka doa katika makuzi yao bora.

Ifahamike kwamba kizuri ama kibaya ambacho kinafanyika katika familia zao, ndicho hicho watoto hao hukichukua.

Japokuwa katika maisha ya kila siku uwezekano wa kukwepa mkwaruzano ni mdogo, lakini kama ikiwezekana ni vema pale mikwaruzano au mabaya yanapotendeka ndani ya familia, kuepusha watoto hao wasishuhudie, labda ikiwa kwa bahati mbaya.

Watoto wanapata majeraha na mipasuko katika mioyo yao wakiwaona wazazi wao jinsi wanavyoishi bila ya upendo na amani ndani ya nyumba hiyo inawasababishia matatizo ya kisaikolojia na kuathirika kiakili na kudhoofika kimwili pia.

Kwa lugha nyingine ninaweza kusema kwamba, wazazi wasio makini wanaweza kuwa ni adui namba moja wa kumharibu mtoto kwa kushindwa kukua vyema hata kuwafanya wazoee ukatili au uhalifu

Yaani mazingira hayo hudiriki hata kuwafanya baadhi kutamka hadharani kwamba mtoto wangu amenishinda.

Hivi karibuni Waziri wa Uwezeshaji wa Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto wa Zanzibar, Moudline Castino, alitoa takwimu za watoto wanaotuhumiwa kwa makosa ya uhalifu wa jinai, waliowekwa katika mahabusu ya mahakama ya watoto visiwani humo.

Alisema ipo idadi kubwa ya watoto wanaofanya makosa ya jinai na kwamba katika kipindi cha 2014/15, watoto 44 waliwekwa rumande za mahakama ya watoto kufuatia kudaiwa kutenda makosa mbalimbali.

Baada ya kutoa takwimu hizo, akawataka wazazi, walezi na jamii kusaidia kuwafunza watoto hao kwa sababu baadhi yao wamekuwa wakifanya makosa pasipo kujitambua.

Pia alisema kitendo cha wana ndoa kutengana kunasababisha watoto kufanya mambo yanayokinzana na sheria ambayo yanasababishwa na kukosa matunzo bora ya wazazi na huduma za msingi.

Ni jambo la kusikitisha kuona watoto wadogo wanajiingiza katika vitendo hivyo, kuwekwa katika mikono ya sheria ni dhahiri kwamba, uwezekano wa kufikia malengo yao ni mdogo kwa sababu hata uwezekano wa kuendelea na masomo yao ni mdogo.

Wito wangu kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuhakikisha wanatimiza wajibu wao ipasavyo wa kuwafundisha yaliyo mema.