Ziara ya JPM muhimu utatuzi madai wakulima wa pamba

22Oct 2019
Raphael Kibiriti
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ziara ya JPM muhimu utatuzi madai wakulima wa pamba

KWA walio na maslahi katika ustawi wa wakulima na hasa wale wadogo wadogo ambao ndio wengi nchini ukilinganisha na wakulima wa kibiashara, wataungana na mtazamo wa Muungwana

Ni kuhusiana na ziara za Rais John Magufuli maeneo tofauti nchini ambazo amekuwa akizifanya kwa lengo la kukagua shughuli za maendeleo na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

Hii ni kwa sababu ziara hizo zimeliletea neema kundi hili linalotegemea kilimo kama chanzo kikubwa cha kiuchumi kwa minajili ya kukidhi mahitaji ya kimaisha na maendeleo kwa ujumla wake.

Muungwana anataja ziara ya Rais Magufuli katika mikoa ya Lindi na Mtwara kuhalalisha anachojaribu kukieleza katika safu hii.

Ziara ambayo pamoja na mengine imetatua changamoto ya madai ya baadhi ya wakulima wa korosho, ambao walikuwa bado hayajalipwa fedha zao.

Akiwa wilayani Masasi mkoani Mtwara wakati wa ziara yake iliyomalizika hivi karibuni, Rais Magufuli alibainisha kwamba kiasi cha Sh. bilioni 72 tayari kimeshatengwa na serikali kuwalipa wakulima wa zao hilo waliokuwa bado wanaidai serikali.

Akatoa maagizo kupitia kwa Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, fedha hizo zianze kulipwa mara moja.

Kwamba wakulima wote wenye madai wawe wamelipwa fedha zao kabla ya kuingia kwenye mnada mpya wa zao hilo unaoanza mwisho wa mwezi huu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, malipo hayo yanatarajiwa kuanza kutolewa leo na hivyo kumaliza sakata la madai hayo ya wakulima wa korosho.

Ndivyo pia ilivyokuwa katika ziara yake aliyoifanya mikoa ya Rukwa na Katavi, ambako changamoto mbalimbali za wakulima, wakiwamo wa zao la pamba alizitatua.

Akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara katika uwanja wa Azimio mjini Mpanda, Oktoba 10, Rais Magufuli alitoa siku 14 kwa mawakala wote mkoani humo wanaonunua pamba kuhakikisha wamewalipa wakulima fedha zao.

Agizo hilo lilifuatia malalamiko waliyoyatoa mbele yake kwamba pamoja na kuuza pamba yao na kusafirishwa na wanunuzi kutoka kwenye Maghala ya Vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS), hawajalipwa fedha zao kwa muda sasa.

Kwamba baadhi yao hawajalipwa madai yao kwa zaidi ya miezi miwili hadi sasa, wakati msimu wa kilimo ukiwa mbioni.

Mbali na kutatua changamoto hizo za wakulima, ziara hizo zimeleta neema karibu katika sekta zote kuanzia kwenye miundombinu ya barabara, maji, afya, stendi, masoko, matatizo ya kawaida ya wananchi na maeneo mengine yaliyoguswa kwa njia moja au nyingine na ziara hizo.

Sasa wakati Rais Magufuli akiwa ametatua changamoto hizo ikiwamo ya madai ya fedha za wakulima wa korosho katika mikoa ya Lindi na Mtwara, na ya wakulima wa pamba katika mkoa wa Katavi, anaona ni vyema akawa na ziara mahususi katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Anasema hivyo kutokana na ukweli kwamba bado kuna wakulima wengi wa pamba ambao hadi sasa hawajalipwa fedha zao, wengine ikiwa ni zaidi ya miezi miwili wakati tayari pamba yao imeshasombwa kupelekwa kwenye viwanda ya pamba na wanunuzi kutoka AMCOS.

Wakulima hawa wanaendelea kusubiri wanunuzi wawalipe fedha zao ili pamoja na mengine wazitumie kwenye kilimo kwani msimu wa kilimo tayari umeshaanza katika kanda hiyo.

Wengi wanategemea fedha hizi ili pamoja na mengine waweze kugharimia mbegu, mbolea, dawa, upandaji, palizi, na mnyororo mzima wa kilimo ambao takribani kila hatua unahitaji fedha.

Muungwana anaona suluhu ya haraka kwa wakulima ambao hawajalipwa fedha zao hadi sasa ni ziara ya Rais Magufuli katika Kanda hiyo.

Ninasema hivyo kwa sababu Rais Magufuli atasikia moja kwa moja kilio hiki kutoka kwa wakulima wenyewe na atachukua hatua mara moja kutatua changamoto hii kama alivyofanya katika mikoa ya Rukwa na Katavi na kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara.