Zijue dalili za mtu ‘aliyefungwa kimaisha’!

05Nov 2017
Flora Wingia
Nipashe Jumapili
Maisha Ndivyo Yalivyo
Zijue dalili za mtu ‘aliyefungwa kimaisha’!

MPENZI msomaji, bado naendelea na mada yetu kuhusu siri ya mikono, leo nikiainisha baadhi ya dalili za mtu aliyefungwa kimaisha kwenye ulimwengu wa roho, yaani ule usioonekana kwa macho ya kimwili.

Niliahidi wiki iliyopita kuwaletea mada hii ya leo, lakini baada ya kupata ujumbe toka kwa wasomaji wengi ikabidi nizichapishe kwanza ili uone wasomaji wengine wanayo yapi yanayowatatiza na hawajui chanzo chake ni kitu gani.

Kumbuka mikono ninayozungumzia ni ya kiroho (haionekani kwa macho ya kibinadamu) lakini imeficha siri nyingi sana.

Dalili zingine tunaziona lakini hatutilii maanani, tunapuuzia kwa kujiridhisha kuwa ni za kawaida, kumbe ni tatizo kubwa.

Lipo andiko la Mungu lisemalo: Isaya 42:20 “Unaona mambo mengi lakini huyatii moyoni; masikio yake ya wazi lakini hasikii”.

Naam. Hebu sasa nikumegee baadhi ya dalili za mtu aliyefungwa kwenye ulimwengu wa roho lakini haelewi ni kwanini inakuwa hivyo.

Kwanza, huwezi kudumu na kitu kizuri kwa muda mrefu. Inaweza kuwa wewe ni tajiri, una ndoa iliyofanikiwa, msomi mzuri au mfanyabiashara mzuri. Ghafla pasipo wewe kujua, unaona mambo yako yanarudi nyuma. Mikosi na balaa inakuandama, madeni yasiyoisha, magonjwa ambayo hukuwa nayo.

Dalili kama hizo na nyingine unazipuuzia, kumbe zina chanzo ambacho kimepikwa kitambo katika ulimwengu wa roho na sasa kinajidhihirisha wazi kwenye ulimwengu wa macho na nyama. Lakini wewe unaona ni kawaida tu, kumbe yupo adui amesimama kukushambulia.

Dalili nyingine unakuwa na roho za uharibifu kwenye mikono yako. Kila unachogusa kinaharibika. Kila biashara unayoanzisha inakufa na kadhalika.

Dalili nyingine unasikia moto kwenye mikono yako. Huo ni moto wa kiroho wa uharibifu. Unapokuwa na moto huu, kila kitu unachogusa kinateketea, iwe ni fedha, magari, nyumba na kadhalika.

Dalili nyingine unakuwa na matundu yasiyoonekana kwenye mikono yako. Kila kitu kizuri unachapata kinakwenda usikokujua wewe.
Kama umekuwa unawashwa mikono yako na ukadhani hiyo ni bahati ya kupata fedha, na ukaandika kiwango cha pesa kwenye mkono wako, ufahamu hiyo ni dalili ya kuunganishwa na mizimu. Pia ni dalili ya kuibiwa nyota ya utajiri na wachawi.

Dalili nyingine unakuwa na roho ya matumizi makubwa wakati kipato chako hakilingani na matumizi yako. Hata kama utakuwa umejinyima kwa kiasi kikubwa, bado matumizi yanaongezeka.

Kwa mfano, katika makala ya wiki iliyopita, yuko kijana mmoja alitoa kilio chake baada ya kusoma makala kuhusu siri ya mikono. Sehemu ya ujumbe wake ilisomeka hivi;… Kila ninachofanya kinaanza na madeni na fedha zangu hazifanyi maendeleo ingawa ni kiasi kidogo.

Kila nikijaribu kuwekeza napatwa na matumizi yasiyokuwa katika lengo langu. Mikono yangu ni kama ya kuharibu tu na siyo ya kujenga. Inakusanya pengine kwa kiasi lakini kutapanya inakuwa ni kwa kasi sana.

Dalili nyingine unakuwa na roho ya hasara kwenye mikono yako ambapo kila biashara unayoifanya inaishia kwenye hasara. Hasara hii inakuwa siyo ya kawaida lakini bado hujui chanzo chake na wakati mwingine hutilii maanani.

Roho hii ya hasara yaichezi mbali na roho ya umasikini. Kama hupati faida katika kile ukifanyacho, unaishia kuwa masikini kwani husongi mbele. Mtu aliyefanikiwa ni yule anayepata faida inayomwezesha kuanzisha kitu kingine kikubwa zaidi. Utajiri ni kuongezeka siyo kudumaa hapo hapo tu. Watu wa mjini wanasema ‘kujiongeza’.

Dalili nyingine ni mikono yako kuwa inapoteza vitu mbalimbali katika mazingira ya kutatanisha. Unaweza kuwa na fedha kiasi fulani, lakini unapokuja kuzikagua unakuta pungufu au hazipo.

Wengine wanapoteza hata watoto, mali za thamani kitatanishi. Huo ni mkono wa kiroho usioonekana kwenye ulimwengu wa roho ambao hukwapua vitu vyako pasipo wewe kuuona.

Mikono ya kiroho yaweza kuwa ni mapepo, majini, mizimu au wachawi kwani hawa wote ni maajenti wa shetani ambaye kazi yake ni kuiba, kuharibu, kuua na kuchinja.

Mpenzi msomaji, kwa leo niishie hapa. Naamini umepata mwanga kidogo kuhusu dalili za mikono iliyofungwa. Wiki ijayo nitajadili baadhi ya aina za mikono ambayo ni mikono ya kurithi, mikono ya hasara, mikono ya utajiri na mikono isiyo na nguvu ya Mungu.

Usipitwe na elimu hii itakayokusaidia kujua yale yanayokusibu lakini huna majawabu.

Je, una maoni yoyote au suala la kifamilia/ndoa/mahusiano linalokutatiza? Wasiliana nami kwa ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 0715268581 (usipige), au barua pepe; [email protected] au [email protected]