Zijue dalili za mtu aliyebadilishiwa mikono!

22Oct 2017
Flora Wingia
Nipashe Jumapili
Maisha Ndivyo Yalivyo
Zijue dalili za mtu aliyebadilishiwa mikono!

MPENZI msomaji, wiki iliyopita nilikuletea hapa makala iliyouliza; Umewahi kujua mikono yako imeficha siri kubwa? Makala ile iligusa watu wengi ambao walituma ujumbe kuelezea matatizo yao kama utakavyowasikia hapo chini.

Baada ya kuelezea siri iliyoko kwenye mikono, leo nizame kidogo kuelezea aina ya mikono ya kichawi iliyobadilishwa, dalili na ushuhuda.

Mikono ya Kichawi: Mikono ya aina hii kibiblia imetajwa kama mikono ya FARAO. “Mwanangu, nimeuvunja mkono wa farao, Mfalme wa Misri, na tazama hautafungwa ili kuutia dawa, haukuzongwa kwa kitambaa, upate kuwa na nguvu za kushika upanga”.(Ezekiel 30:21).

Maandiko ya Mungu yanapotufundisha kwa habari ya mkono wa Farao, hapo inamaanisha nguvu za Farao. Maandiko ya Biblia mara nyingi yanazungumzia MKONO WA MUNGU, ikimaanisha NGUVU ZA MUNGU. Kuna mikono ya kichawi isiyoonekana ambayo imewafilisi watu wengi na kuwafanya masikini wa kutupwa.

Unaweza kupewa mikono hii ya kichawi (mikono ya Farao) pasipo wewe kufahamu. Na kama umebadilishiwa mikono yako na kupewa mikono ya kichawi, utaanza kuona dalili zifuatazo;-

1. Utaanza kushangaa unapoteza vitu katika mazingira ya kutatanisha.

2. Unaanza kupata hasara kwenye biashara zako kwa namna isiyokuwa ya kawaida hata kama umekuwa mwangalifu sana.

3. Unaanza kuwa na usahaulifu usiokuwa wa kawaida.

4. Utaanza kuona kila biashara unayoianzisha inadumaa na kubakia pale pale.

Unapoona dalili hizi usiogope kwa maana Mungu ametupatia ahadi hiyo hapo juu (Ezekiel 30:21), kwamba mikono hiyo ikivunjwa haitapona tena, kwa maana ni ya kichawi na itakuwa ni mwisho wa kuiba baraka za watu.

Mpenzi msomaji, hebu sikia ushuhuda huu uweze kuinua imani yako katika kushughulikia tatizo linalokusibu.

Dada mmoja alikuwa na tatizo kubwa la matumizi ya pesa. Kila alipopata mshahara, matatizo yalitokea na hiyo pesa ya mshahara ilikwenda kutatua hayo matatizo, hivyo kumfanya dada huyu awe katika mzunguko mkubwa wa madeni.

Dada huyu alipogundua kuwa jambo hilo halikuwa la kawaida, aliingia kwenye maombi makali na Roho Mtakatifu akampa ufunuo wa ajabu.

Mwezi uliofuata alipokea mshahara wake, na aliendelea kufanya maombi ya vita. Alipopata ule mshahara, alichukua panga kwenye mikono yake na akauweka mshahara wake chini, akaanza kusema;

“mkono wowote unaochukua mshahara wangu, ninaukata kwa upanga, kwa jina la Yesu Kristo”.

Kitu cha ajabu kilitokea huko kijijini kwao alikozaliwa. Bibi yake alipoamka asubuhi alikuta mkono wake wa kulia umekatika kabisa. Kumbe mkono wa kichawi wa bibi huyu ulikuwa unachukua pesa za yule dada pasipo yeye kufahamu.

Mpenzi msomaji, hapo ipo siri ya ajabu. Kwanini mkono wa huyu bibi ukatike? Ni kwa sababu kulikuwa na uhusiano kati ya bibi yake na kupotea kwa pesa za huyu dada.

Hili ni tatizo linalowatesa watu wengi, lakini wanalipuuzia. Kumbe ni mikono ya kichawi ambayo ni chanzo cha matatizo ya matumizi mabaya ya fedha.

Hebu sikia baadhi ya wapendwa wasomaji ambao walibahatika kuisoma makala ya wiki iliyopita kuhusu siri ya mikono, kisha kuelezea matatizo yao ambayo kwa hakika yanatokana na mikono ya kichawi. Hebu tuwasikie;-

Kwa mfano mmoja akaandika ujumbe huu; “kiukweli ndugu yangu nimeguswa na habari hii siri ya mikono. Kila nifanyacho kwangu sipati mafanikio, nikishika hela zinayeyuka bila kufanya kitu cha maana. Naomba msaada wako.”(0715301315).

Mwingine anasema ; “habari dada, mie kila nifanyalo napata hasara na kuzidiwa na madeni”. (0754280844).

Mwingine anasema; “Nina matatizo kwenye ndoa. Nilikuwa na mchumba tupo kwenye mahusiano nikashika upauzito mimba nikaenda nayo hadi miezi minne ikapotea sikuisikia tena tumboni. Nilipomwambia mwanaume akadai mimi ni muongo nimeitoa, akaniacha pale pale nilivyomtamkia”. (076863453).

Mwingine anasema; “Mimi biashara zangu zimeenda vibaya, naomba msaada wako”. (0673995565).

Hawa ni wachache, wako wengi wanaoshikiliwa na mikono ya kichawi na wala hawajui wajinasue vipi. Hapa maombi ya nguvu yanahitajika kuvunja mikono hiyo ya Farao ambayo imeangamiza hatma za watu wengi sana.

Watu waliojeruhiwa na mikono hiyo ya kichawi wanapaswa kufanya maombi ya nguvu kukata mawasiliano yote kwenye pesa zao, kuvunja mikono ya mizimu, mikono ya hasara, mikono ya chuma ulete. Baada ya kuivunja, omba mkono wa Mungu uguse mikono yako kuibadilisha na pia kuitakasa kwa damu ya Yesu (kwa Wakristo).

Wiki ijayo nitaelezea mikono iliyofungwa, maeneo iliyofungwa, dalili za mtu aliyefungwa kwenye ulimwengu wa roho na shuhuda. Baadaye nitakuelezea mikono ya kurithi, mikono ya hasara, ya utajiri.

Usikose NIPASHE Jumapili.

Je, una maoni yoyote au suala la kifamilia/ndoa/mahusiano linalokutatiza? Wasiliana nami kwa ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 0715268581 (usipige), au barua pepe; [email protected] au [email protected]