Zimamoto wasilaumiwe kwa haya, isipokuwa...

12Jan 2018
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Zimamoto wasilaumiwe kwa haya, isipokuwa...

MAJUKUMU ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, ni kuokoa maisha na mali katika majanga yatokanayo na moto, mafuriko, tetemeko la ardhi, ajali za barabarani pamoja na majanga mengineyo katika jamii. 

Jeshi hilo pia lina jukumu la kutoa huduma kwa jamii katika nyanja mbalimbali, zikiwamo kuokoa maisha ya watu na mali zao, kuzima moto, kutoa elimu ya kinga na tahadhari ya majanga moto na kufanya ukaguzi wa tahadhari na kinga ya moto.

Vilevile, ni kikosi chenye jukumu la kusoma ramani za majengo, kutoa ushauri na huduma ya kwanza katika majanga na ajali barabarani.

Sambamba na hayo, kuna jukumu la kutoa mafunzo ya kukabiliana na majanga ya moto, kufanya uchunguzi kwenye majanga ya moto na kutoa huduma za kibinadamu.

Hata hivyo, kwa upande wa kuzima moto katika nyumba za makazi, limekuwa likikabiliwa na changamoto kubwa, ikiwamo ya ama kushindwa au kuchelewa kufika kwenye eneo la tukio.

Sababu kuu mara nyingi ni kutokana na ujenzi holela wa makazi ya watu wanaosababisha hadi kuziba barabara.

Katika mazingira hayo, wapo baadhi ya watu ambao wamekuwa wakiwalaumu na hata kufikia hatua yakuwarushia mawe askari wa jeshi hilo, eti hawafanyi kazi vizuri, kwa kushindwa kufika kwenye maeneo ya matukio kwa wakati .

Mtazamo wangu ni kwamba, zipo sababu nyingi zinazochangia askari hao kuchelewa kufika kwa wakati kwenye eneo la tukio au ikitokea washindwe kufika kabisa.

Hapo nitadokeza sababu kuu mbili, zaidi nikiligusa jiji la Dar es Salaam nikiwasilisha ujumbe kwa mengine yanayofanana. Kwanza, ni ujenzi holela wa nyumba za makazi hadi ambazo zinaziba kabisa barabara, hivyo linapotokea janga la moto, inakuwa vigumu kwa magari ya zimamoto kufika eneo husika kwenye tukio.

Sababu ya pili, ni msongamano wa magari barabarani, unatokana na uchakavu au kutokaa vizuri kwa miundombinu ya barabara.

Pia, kuna suala la kukosekana njia ya magari ya Zimamoto kuchepuka, ni hali inayosababisha magari yake kutofika eneo la dharura kwa wakati.

Kwa kuegemea sababu hizo mbili, ninaamini kwamba ziko juu ya uwezo wa kikosi hicho. Sidhani kama wananchi wana haki ya kukilaumu au kurushia askari wake mawe, kwa hoja ‘eti wamechelewa kufika au wanaishia njiani.’

Sasa wao Zimamoto wapite wapi, kama nyumba zimejengwa hadi kuziba barabara? Wao wapite wapi kama kwenye barabara kuna foleni kubwa za magari? Jamii itakafari na kisha iwatendee haki.

Bila ya kutambua changamoto hizo, Zimamoto wataendelea kulaumiwa kwa makosa ambayo yako juu ya uwezo wao, ingawa ninajua kuwa yapo mengine kama kufika eneo la tukio bila ya kuwa na maji ya kutosha, hayo ni makosa yao.

Huwa kuna tuhuma nyingine zinazotolewa na wananchi kwamba, Zimamoto wanaweza kufika katika eneo la tukio na kusema kuwa “wamekuja kuangalia ukubwa wa moto na kisha wanakwenda kuchukua maji.”

Kama tuhuma hizo zina ukweli, basi Zimamoto hawawatendei haki wananchi, lakini kwa suala la kujenga nyumba na kuziba barabara au magari kuchelewa kwenye foleni, jeshi hili halipaswi kulaumiwa.

Wananchi watambue kuwa suala la ujenzi holela wa makazi usiozingatia taratibu na pia foleni za magari barabarani, yanapaswa kushughulikiwa na mamlaka husika kwa ajili ya kuondokana na kero hiyo.

Unaweza kukuta gari la Zimamoto linasimama umbali wa mita 100, kwa sababu tu hakuna barabara ya kufika eneo la kuzima moto nyumba inayoungua. 

Sasa hapa kweli wanapaswa kulaumiwa kwa kuchelewa kufika kwenye tukio au vinginevyo?

Kwanza, hakuna mtu mwenye haki ya kumpiga mwenzake. Pia, kabla hawajafanya uhuni huo, ni vyema wakajiuliza kama wanaijua vizuri miundombinu ya barabara za Dar es Salaam.

Katika jambo lolote, ni muhimu kutafakari kwanza kabla ya kuchukua hatua, zikiwemo hizo ambazo baadhi ya wananchi wamekuwa wakizichukua dhidi ya Zimamoto.

Ufike wakati wananchi tujifunze kutafakari, kabla ya kuchukua hatua zinazoshuhudiwa sasa, dhidi ya wana - Zimamoto wanapoenda kwenye majanga yanayowahusu.

Wanaofanya hivyo wasijione hawana makosa, huku wakitambua wazi wamejenga nyumba kiholela na kusababisha magari kushindwa kupita hata pale yanapotokea majanga ya moto kwenye maeneo yao.

Angalizo langu ni kwamba, wananchi wasiwe wepesi wa kulaumu kila jambo, hata lile ambalo wao ndiyo waliolisababisha, kwani katika mazingira hayo, kulaumiana, kushutumiana na kushambuliana hayajengi.

Hivi mtu anapojenga nyumba na kuziba barabara, halafu inapookea janga la moto kwenye eneo lake, magari ya Zimamoto yatafikaje kwake? 

Kwa nini jamii isiwe na utamaduni wa kujenga makazi na kuachana nafasi kwa ajili ya barabara? Wanapowalaumu Zimamoto, ni vyema wakajichunguza binafsi kwanza kabla ya kuchukua uamuzi huo, kwani ni makosa.

Pia, ni aibu wananchi kwa umma kuwarushia mawe Zimamoto kwa kushindwa au kuchelewa kufika kwenye tukio, huku wakijua kuwa wao ndio wamechangua katika kusababisha hilo.

Waachane na malalamiko yasiyo na msingi au kuwarushia mawe Zimamoto, badala yake wajitafakari kama hawana makosa yanayochangia vikosi hivyo kushindwa kutimiza majukumu yake kikamilifu kwa uzembe wa baadhi yao.