Zinahitajika hamasa kujenga miundombinu wenye ulemavu

30Jun 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Zinahitajika hamasa kujenga miundombinu wenye ulemavu

KATIKA kuhakikisha wanafunzi wa kike wa shule za msingi na sekondari wanasoma bila kupata changamoto ya kukosa masomo wakati wa hedhi jitihada mbalimbali zimefanyika zikiwamo kutoa hoja binafsi bungeni kuomba punguzo la gharama ya taulo za kike.

Miongoni mwa jitihada hizo au kampeni za kuchangisha fedha kutoka kwa wadau mbalimbali kwa ajili ya kununua taulo hizo ambazo zinatajwa kuwa suluhisho la tatizo hilo kwa wanafunzi wa kike zimefanyika hivi karibuni na huenda zitaendelezwa.

Kampeni ya kuchangia taulo hizo iliwahi kufikishwa bungeni na Mbunge wa Viti Maalum CHADEMA, Upendo Peneza na kuungwa mkono na wabunge wengine.

Lakini pamoja na hayo, ipo haja sasa kampeni kama hizo kuhamia kwenye miundombinu ya walemavu katika shule ili nao waweze kusoma bila changamoto ambazo ziko ndani ya uwezo wa jamii.

Ninasema hivyo kwa sababu elimu inatakiwa kutolewa kwa kila mtoto bila kujali tofauti za jinsia na kimaumbile, hivyo kuna haja ni muhimu kuondoa vikwazo vya baadhi ya shule kutokuwa na miundombinu ya kuwawezesha wanafunzi wenye ulemavu kupata elimu bila tatizo lolote.

Wanafunzi wenye walemavu wa viungo hukutana na changamoto hasa wakati wa kwenda chooni, kutokana na kujengwa bila kuzingatia mahitaji yao na kusababisha watembea juu ya vinyesi na maji machafu ya chooni.

Lakini wanahitaji viti mwendo ili kutembea hasa kwa wale ambao muda wote wanalala au kukaa chini kutokana na matatizo ya miguu na uti wa mgongo.

Tatizo lipo pia kwenye baadhi ya madarasa ambayo nayo ni vyema yajengwe kulingana na mahitaji ya walemavu hasa wa viungo vya miguu, kwani wapo wanaotembea kwa kusota chini.

Kwa ujumla ulemavu si dhambi wala laana bali ni hali inayompata yeyote na inayotakiwa anayepata shida hiyo kuwezeshwa kwa kuangalia mahitaji ya msingi ikiwamo elimu na miundombinu rafiki ya kupata elimu.

Hivyo, katika kujenga jamii yenye usawa na kujali makundi yote, ni vyema kutambua kuwa si jukumu la serikali tu kuboresha miundombinu ya shule kwa ajili ya wanafunzi walemavu bali nayo inahusika.

Karibu shule zote zina uhaba wa madarasa na vyoo, hivyo vinapofanyika juhudi za ujenzi ambao kimsingi unahusisha jamii, ni muhimu kuzingatia miundombinu ya wanafunzi wa aina hiyo.

Inawezekana katika mazingira hayo ya kutokuwapo kwa miundombinu ya walemavu shuleni, wapo baadhi ya wanafunzi ambao wameacha shule na kushindwa kufikia malengo yao ya baadaye waliojiwekea.

Jamii ihamasishwe kushiriki ujenzi wa madarasa na vyoo, lakini kikubwa ikiwa ni kuzingatia kuwapo kwa miundombinu inayogusa walemavu wa viungo ili nao wajione kama wanathaminiwa.

Kampeni zisiishie katika kuchangia taulo za kike tu, bali zihamie pia kwenye ujenzi wa miundombinu ya shule kwa ajili ya wanafunzi walemavu wakiwamo wa kike na wa kiume.

Ukweli ni kwamba ukosefu wa miundombinu ya shule kwa makundi yote ni kikwazo kwa wanafunzi wenye ulemavu kupata elimu, hivyo wadau wote wa elimu hawana budi kuliona tatizo hilo na kushiriki kikamilifu kulimaliza.

Kuwapo kwa miundombinu ya walemavu katika shule kuna mchango mkubwa hasa kufanikisha jitihada za serikali za kuwa na elimu jumuishi ambayo inahusisha wanafunzi wote wakiwamo wazima na wenye ulemavu.

Hivyo ni wakati sasa shule zote, kwa dhana ya elimu jumuishi iwekwe miundombinu ya kuwawezesha wanafunzi wenye ulemavu kujumuika na wenzao wazima ili kuzoeana na kuweka usawa.

Ninaamini kwamba hilo litawezekana, hasa zikifanyika kampeni maalum za kuhamasisha jamii kushiriki kwa hali na mali katika ujenzi wa madarasa na vyoo vinavyozingatia mahitaji ya kundi hilo.

Ikiwa kila mmoja atashiriki katika jambo hili, atarahisisha safari ndefu ya kuelekea katika lengo la kuwa na elimu inayofikiwa na watoto wote bila kujali ni wazima au ni walemavu wa viungo ili wote wafaidike na elimu.

Ikumbukwe hata Mpango wa Umoja wa Mataifa (UN) unaozitaka nchi wanachama kuhakikisha elimu inatolewa kwa kila mtoto bila kujali tofauti za jinsia na kimaumbile.

Vilevile mkakati huo uliosimamiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) na kuishia mwaka 2015, ulilenga kuimarisha mpango wa elimu kwa wote katika ngazi ya kitaifa na kimataifa kwa watoto wote, vijana na watu wazima, hivyo kuna haja ya kutafakari tulikofikia na kuchukua hatua.