Zisikike sauti kudai nafasi kwa wanawake

24Feb 2021
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Zisikike sauti kudai nafasi kwa wanawake

UPO msemo kuwa uchaguzi mmoja ukiisha huanzisha mwingine. Kwa hiyo baada ya kumalizika uchaguzi wa Oktoba 2020 yanayofuata sasa ni maandalizi ya uchaguzi wa 2025.

Hoja yangu ni kutaka mikakati iwape nafasi wanawake kwa vile baada ya uchaguzi mkuu sauti za uteuzi wa wanawake kushika nyadhifa mbalimbali zimeanza kupoa moto.

Itakumbukwa mwaka jana ulikuwa msimu wa masuala ya wanawake kuzungumzwa kila upande na zilisikika sauti kuhimiza uteuzi wao kuwa wagombea kwenye majimbo au kata wakati wa uchaguzi mkuu.

Ilikuwa habari kubwa ya vyama kwa sababu ilionekana kuwa kuteuliwa kinamama kushika nyadhifa hizo majimboni au kwenye kata kilikuwa kigugumizi kinachovipata vyama vingi.

Vyama vinaoongozwa na hofu kuwa iwapo watapelekwa majimboni au kwenye kata hawatachaguliwa.

Vipo baadhi ya vyama viliwapa kinamama nafasi za kugombea ubunge, urais na hata udiwani na kimojawapo ni ADC.
Kiliteua kinamama kushika nafasi hizo kwenye majimbo yote ya Dar es Salaam na katika kata pia.

Kampeni za kuhimiza uteuzi wa wanawake zilikuwa zinawahamasisha Watanzania kuwachagua wanawake kushika nafasi mbalimbali za kuongoza taifa kwani wana sifa zikiwamo umakini na utulivu, uadilifu na uchungu kwa watoto na familia zao.

Lakini kampeni kwa vyama zilivihimiza kubeba jukumu la kuwapa wanawake nafasi za uongozi wa kuchaguliwa kwa misingi ya kuheshimu ajenda na usawa wa kijinsia.

Leo inafaa tena ajenda ya kuwatetea wanawake kupewa nafasi tena iwe endelevu hata baada ya miezi mitano ya uchaguzi.

Vyama vinatakiwa kuendelea kuweka mbele ajenda za kuwapa nafasi na kujadili mikakati ya kuwawezesha kinamama kushiriki kwenye uchaguzi bila vikwazo.

Huu ndiyo wakati wa kuanza kuhamasisha tena vyama vya siasa pamoja na Watanzania kubadilisha mitazamo na kufuta mawazo hasi kwamba kinamama hawawezi.

Wanawake wanafanya kazi kubwa na nzuri ndani ya serikali zote kuanzia awamu ya kwanza hadi ya tano.

Kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita na sasa ni jambo ambalo linatosha kuamua kuwapa nafasi kwenye uchaguzi ujao wa 2025.

Baada ya uchaguzi ndiyo wasaa wa vyama kutengeneza uhusiano mwema na wananchi ili uchaguzi ufanyike kwa misingi ya kijinsia, uhuru na wa haki tena unaokubalika.

Hivyo ni lazima vyama vitambue umuhimu wa kushirikisha wanawake na viwe na uelewa kwamba wanawake wamechoshwa na kauli kuwa ukishindwa kubali matokeo.

Kuwaandaa wanawake kuwa wagombea wa majimbo na kata nyingine za 2025 ni jambo linalotakiwa kuanza kuandaliwa sasa na hata kama watajitokeza wagombea wanaume mchujo ufanyike kwa haki.

Lakini, pamoja na kuwapa nafasi ni vyema vyama vianze kuwapa jukumu la kuviongoza.

Kina mama waanze kupewa majukumu ya kuongoza vyama na kufahamika kwa wananchi badala ya vyama vyote kuongozwa na wanaume ambao ndiyo wanaojitokeza na kupewa kipaumbele kwenye uchaguzi kwa kuwa wanafahamika.

Lakini, ili wanawake wapigiwe kura ni muda pia wa kufikiria namna bora ya kufanya siasa ili kila chama kinadi sera zake kwa wananchi na kuwatangaza wanawake badala ya kutegemea muda finyu wakati wa kampeni za uchaguzi.

Ni wakati pia wa vyama visivyo na ruzuku kutafuta njia bora ya kuwaandaa wanawake na kuwafikisha kwa wapiga kura wanaowalenga.

Sababu za wanawake wengi kushindwa kushiriki kwenye kampeni za majimboni na kata ni pamoja na ukosefu wa pesa.

Katika mikakati ya kuandaa uchaguzi wa 2025 vyama vinatakiwa kuunga mkono wanawake kwa kuwa uchaguzi ni gharama na zinahitajika pesa nyingi kwenye kampeni.

Aidha, huu ndiyo muda wa kupata majibu ya maswali ya wapi pa kupata fedha hizo.

Mathalani, mkutano mmoja wa kampeni kwenye jimbo unaelezwa kuwa hugharamia takribani Sh. 1,000,000 nacho ni kiasi cha chini mno.

Vyama vianze kupanga mikakati ya kuwaandaa kinamama ili isiwe ni maneno zaidi kuliko vitendo.