Zitafutwe mbinu wanafunzi wasiogope, wasifeli Hisabati

18Jan 2022
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Zitafutwe mbinu wanafunzi wasiogope, wasifeli Hisabati

MATOKEO ya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2021/2022, yametangazwa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), huku Katibu Mtendaji, Dk. Charles Msonde, akisema, watahiniwa hawakufanya vizuri kwenye somo la Hisabati.

Katibu Mtendaji anasema, ufaulu wa somo hilo upo chini ya wastani ya asilimia 19, na kwamba mwaka jana ulikuwa chini ya wastani kwa watahiniwa kupata asilimia 20.12, hivyo, kwa kauli yake, ni wazi kwamba, kuna haja ya kuchukua hatua za kuimarisha kujifunza na kufundisha hesabu ili kusaidia wanafunzi kumudu vyema somo hilo na kuondoa dhana iliyozoeleka miongoni mwao kuwa hesabu ni ngumu.

Ni vyema wanafunzi wakaondolewa fikra hizo, wasiwe  wavivu wa kujifunza hisabati, lakini kuwe na hamasa kutoka kwa walimu ya kuhamasisha watoto shuleni kuliona somo hilo kama la kawaida kuliko kulikimbia na kulichukia.

Pamoja na hayo, bado kuna haja ya kuangalia mfumo wa elimu, kwa kuondoa utaratibu wa mtihani wa hisabati kuwa wa kuchagua, kwani unaweza kuwa unachangia wanafunzi kufanya vibaya katika somo hilo.

Hebu fikiria, katika shule ya msingi, mwanafunzi anapewa mtihani wenye kuchagua majibu, kwa mazingira kama hayo, ni vigumu kufanya vizuri katika somo hilo, kwani huko anakotokana hakuna utaratibu huo.

Akiwa sekondari, itambidi aumize kichwa kufanya mtihani wa somo hilo, wakati awali alikuwa anachagua majibu, jambo ambalo ni vigumu mwanafunzi kuwa na msingi mzuri wa hisabati.

Ninaamini kwamba, somo hilo linamfanya mwanafunzi atafute mbinu za kupata jibu hasa kwa kuzingatia kanuni, lakini anapoelekezwa kuchagua majibu, hawezi kuwa na msingi imara wa kukokotoa na kupata majibu.

Hivyo, ingekuwa vyema iwapo mfumo wa ufundishaji wa somo hilo, hasa katika shule za msingi utaendelea kama ulivyo na hata kwenye mtihani, wanafunzi watumie waumize vichwa kupata majibu badala ya kuchagua.

Yawezekana mfumo wa kazi, swali, jibu umepitwa na wakati, lakini huenda, ulisaidia wanafunzi kumudu somo hilo, kwani sehemu ya kazi ndiyo inayoonyesha jinsi gani amefanya hadi akapata jibu.

Kwenye suala la mtihani wa hisabati kufanyika kwa kuchagua majibu, wanasiasa wamekuwa wakilaumiwa kuwa wameingilia na kusababisha wanafunzi kutoumiza vichwa kufanya somo hilo.

Kama hilo lina ukweli ndani yake, basi ingependekeza siasa zingeachwa pembeni, ili elimu ichukue nafasi yake hatimaye wanafunzi waweze kumudu somo hilo ambalo ni miongoni mwa masomo muhimu.

Vilevile, kuna suala la uhaba wa walimu wa somo hilo, katika shule mbalimbali, jambo ambalo kwa namna moja au nyingine linaweza kuchangia  wanafunzi kutofundishwa ipasavyo.

Kwa maana hiyo, ninadhani kuna haja ya uboreshaji wa upatikanaji wa walimu, ili wawe wa kutosha, ambao wameandaliwa vya kutosha wakaiva na wawe na vitendea kazi ili wafanye kazi yao kikamilifu.

Hatua hiyo inaweza kwenda sambamba na kupunguza wingi wa wanafunzi katika darasa moja ili mwalimu awe na unafuu katika ufundishaji, kwani sidhani kwamba, ni rahisi kufundisha wanafunzi 100 kwa wakati mmoja.

Lakini pamoja na hilo, kuna haja ya wanafunzi kupewa majaribio ya mara kwa mara ya somo hilo, waweze kulizoea hata katika mtihani wasipewe maswali ya kuchagua majibu, bali kila mmoja aumize kichwa kupata jibu.

Pamoja na hilo, si vibaya kukawa na motisha kwa walimu wanaofundisha somo hilo, kwani inaweza kuchochea kasi ya kuwafanya wafundishe kwa bidii na kutoa mbinu zitakazofanya wanafunzi walipende.

Kaulimbiu ya walimu na hata wazazi kwa watoto wao ingekuwa ni 'hisabati ni somo rahisi', ili wawe nayo vichwani, walipende, kwani wakiambiwa kuwa ni gumu, ni wazi watafanya vibaya katika mtihani.