Samatta alibeba 'kizizi' Simba

13Jan 2016
Lete Raha
Samatta alibeba 'kizizi' Simba

KIZIZI cha klabu ya Arsenal kufikia sasa kwenye Uwanja wa Emirates ni kiungo wao, Mathieu Flamini. Katika mechi zote zaidi ya 40 alizocheza kiungo huyo kwenye uwanja huo, Arsenal haijawahi kupoteza mchezo na kwa Simba kizizi chao alikuwa ni Mbwana Samatta, 23.

Mbwana Samatta

Mshindi huyo wa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani ya bara hili, alikuwa ndiyo kete ya bahati ya Simba na African Lyon kwani katika kila mechi ambayo alifunga bao, klabu hizo mbili hazikuwahi kupoteza mchezo.
Hali hiyo imemfanya Samatta kuacha rekodi ya kipekee nchini. Aliifungia Simba jumla ya magoli 7 katika nusu msimu aliowatumikia Wekundu wa Msimbazi, ikiwamo 'hat-trick' katika ushindi wa 4-1 dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Februari 27, 2011.
Katika mechi nne ambazo Samatta alifunga, Simba ilishinda tatu na kutoka sare moja, wakati katika mechi tano ambazo straika huyo alifunga, Lyon ilishinda zote kabla hajahama na kujiunga na Simba.
Lyon ilimaliza ligi msimu wa 2009/10 ikiwa kwenye nafasi ya saba kwa pointi 25, huku pointi 15 kati ya hizo zikichangiwa na magoli ya Samatta. Magoli yake yaliwapa asilimia 60 ya pointi za Lyon za msimu huo.
Akiwa na Simba katika msimu wa 2010/11, mabao ya Samatta yaliwapa Wekundu wa Msimbazi pointi 10, kati ya pointi 49 walizokusanya msimu huo na kumaliza katika nafasi ya pili. Mabingwa walikuwa Yanga ambayo nayo ilikuwa na pointi 49, lakini ilipata ubingwa kwa tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa.